Na Grace
Mkojera
Ukatili
dhidi ya wanawake ni ukiukwaji ulionea wa haki za binadamu, ni janga kubwa
katika jamii na kikwazo cha kufikia usawa, maendeleo, usalama na amani. Wakati
wengine wakifurahia amani kuna wengine wanalia kwa kutendewa ukatili.
Inakadiriwa
kuwa mmoja kati ya wanawake watatu duniani atakumbana na aina fulani za ukatili
wa kijinsia katika maisha yake.
Takwimu za
mwaka 2010 za TDH zinaonyesha kuwa robo tatu ya wanawake wa kitanzania wenye
umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 wameshafanyiwa vitendo vya ukatili kwa mwaka.
Utafiti wa
mwaka 2009 unaonyesha kuwa watoto wa Tanzania 6 kati ya 10 wasichana na
wavulana wana uzoefu wa ukatili kutoka kwa walimu hao.
Aidha, siku
16 za kupinga ukatili wa kijinsia zimekuwa zikiadhimishwa na watu binafsi
pamoja na makundi duniani kote wanaotumia mtizamo wa haki za binadamu ili kutoa
mwito wa kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake kwa kuelimisha jamii
na kuishinikiza serikali kutekeleza maazimio ya kisheria yaliyofikiwa kitaifa
na kimataifa.
Katika
maadhimisho yaliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa
kushirikiana na washiriki wa semina za jinsia na maendeleo (GDSS), kuna baadhi
ya wadau mbalimbali ambao walitoa visa mkasa vinavyowanyima usingizi mtaani.
Mmoja wa
washiriki kwenye maadhimisho hayo ni Hadija Rashid ambaye ni mkazi wa Kiburugwa
jijini Dar es Salaam, anaeleza machungu ambayo yamekuwa yakimkosesha raha na
familia yake.
Ni mama wa
familia ya watoto 7 ikiwa ni mchanganyiko wa watoto wa kike na wa kiume. Katika
watoto wake wa kike wawili mmoja anasoma kidato cha pili anayeitwa Amina
Mohamed na mwingine anaitwa Rahma Mohamed ambaye hasomi hawana raha ya maisha
kutokana na vita na majaribu anayokutana nayo.
Mama huyo
anaelezea kuwa watoto wake hao pindi ambapo wako mtaani kuna kikundi cha vijana
katika mtaa wanaoishi ambao wamekuwa wakiwasumbua na kuwatongoza.
Watoto hao
wamekuwa wakiwakatilia vijana hao hasa ikizingatia kwamba mmoja ndio huyo
anasoma bado ni mwanafunzi na mwingine ameamua kujiheshimu hivyo wote
waliwakatalia.
Katika kundi
hilo la vijana zaidi ya 10 ambao hupenda kukaa kijiweni katika jumba moja bovu,
wamekuwa wakitoa vitisho kwa wasichana hao. Kumbe kila mmoja anapowajaribu
wasichana hao na kukataliwa huambizana hivyo hupanga mkakati wa kuwakomesha.
Anaelezea
kuwa watoto wake hao pindi wanapoenda kuchota maji hukutana na kundi hilo
wakiwa wanawasubiri na kuwatukana huku wengine wakiwaeleza wazi wazi kuwa lazima
wawabake waone wanachoringia ni kitu gani.
Maneno
makali ambayo yamekuwa yakitolewa na vijana hao yamekuwa yakiwapa hofu ya
maisha. Ndipo mama huyo alipoamua kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi
Kiburugwa na kupewa RB huku wakiahidiwa kuwa watakuja kuwakamata vijana hao.
Baada ya
wiki moja Polisi hawakutokea kuwakamata vijana hao bali waliendelea kukaa
kimya. Ikawa kila wale watoto wanapotumwa kwenye maji ama kwenda kutafuta kuni
inabidi waende wawili wawili kwasababu tayari walishatishiwa kubakwa.
Anasema kuwa
ili watoto wake wasikumbwe na vitisho hivyo pia aliulizia mahali wanapoishi
vijana wale ili kuzungumza na wazazi wao kuhusiana na vitisho wanavyotoa na
kuahidiwa na wazazi wao kuwa watazungumza na vijana wao.
Lakini
anasema taarifa ile haikusaidia bado wale vijana waliendelea na vitisho mara
kwa mara. Kila wanapowaona wale wasichana wakiwa peke yao hutokea ghafla na
kuwazingira na kuwavutia pembeni bila kuogopa kwamba kuna watu wanaopita
watawaona.
Anasema kwa
bahati siku ya kwanza ambapo kundi hilo la vijana liliwazingira wasichana hao
ili wawabake kulikuwa na mzee mmoja wa kilokole ambaye alikuwa akipita na kuona
lile tukio ndipo kuwaokoa wasichana hao hivyo walinusurika.
Wiki ya pili
baada ya mama huyo kuona hakuna mafanikio anasema akaenda tena kituo cha Polisi
kutoa taarifa dhidi ya tukio hilo lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
“Ndipo
nikaenda tena kwa wazazi wa wale vijana kwa mara nyingine na kupewa RB, lakini
bado hawakukamatwa,”anasema.
Anasema siku
nyingine alimtuma tena mtoto yake ambaye
hasomi aende kununua kuni, ilikuwa ni majira ya saa tisa jioni huku mdogo wake
ambaye ni mdogo mwenye umri wa miaka 9 akimsindikiza.
Wakati
wanarudi mara wakatokea vijana 2 wakawazingira na kumlazimisha Yule dada atupe
kuni chini na kumkamata. Yule mtoto mdogo alifanikiwa kukimbia. Hawakujali bali
waliendelea na Yule mkubwa wakamfunga kamba miguuni na mikononi huku kijana mwingine akisema kuwa “tumvunje
mbavu,”
Anasema
wakati kijana mmoja akisema wamvunje mbavu kwasababu yule binti alikuwa ni
mbishi anajaribu kujinasua ili apate kuokoka, Yule kijana mwingine akasema
“tumpige na jiwe kichwani ili apoteze fahamu ili kuwa rahisi kumaliza kazi ya kubaka,”
Anazidi
kusimulia huku machozi yakimtoka kuwa wakati Yule mmoja akienda kutafuta jiwe,
Yule kijana mwingine tayari alikuwa na wembe ameuweka kiganjani hivyo
aliutumbukiza kwenye vidole na kumpiga nao Yule msichana usoni.
Hata hivyo,
kabla hawajafikia zoezi lao la kumpiga jiwe kichwani ili wamalize kazi yao,
kwasababu Yule mtoto mdogo alikimbilia nyumbani kutoa taarifa kwa wazazi,
waliwahi kuja na kumwokoa.
“Sehemu
alipokamatiwa binti yangu sio mbali sana na nyumbani, tuliweza kuwahi mapema na
kumwokoa,”anasema Bibi Hadija.
Anasema kuwa
wale vijana walipowaona walikimbia, na ndipo mama huyo kukimbilia tena Polisi
Kizuiani baada ya kuona Kiburugwa hawakuwapa msaada wowote.
Kwa bahati
nzuri mkuu wa Polisi kiuziani kwa kushirikiana na wenzake waliona jambo hilo
sio la kuvumilia, walienda kuwatafuta vijana hao na kufanikiwa kuwakamata.
Walifanikiwa
kufungua kesi katika mahakama ya kizuiani, hata hivyo vijana hao tayari
walishaachiwa kwa dhamana wako mtaani, ila kesi bado inaendelea kusikilizwa.
Pamoja na
harakati zote hizo za kuwaokoa watoto wake bado anakabiliwa na changamoto
kubwa, jamii inayomzunguka haijashirikiana naye katika kupambana na vijana hao
hatari.
Anaeleza
imekuwa ni kawaida kwa vijana hao kuwabaka wasichana na kuwapa mimba. Wasichana
wengi wanaoishi katika mtaa wake wamepata mimba na wala hawana msaada wowote.
Na bado
wanaendelea na vitendo vya kikatili na wanakaa kimya badala ya kuweka umoja wao
ili vijana hao wachukuliwe hatua kali za kisheria. Bado baadhi ya wazazi wa
vijana hao wengine wamekuwa wakimlaumu Hadija kwa kuwafungulia wanawe kesi na
wengine walimvamia na kumpiga hadi kupoteza fahamu.
Ukatili huo
hauhitajiki kufumbiwa macho, jukumu ya kupinga vitendo hivyo liingiliwe na
jamii ili kunusuru maisha ya watoto wa kike. Kuendelea kunyamaza bila kusema
chochote wala kuchukua hatua ukatili utaendelea kuongezeka.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment