TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Saturday 7 September 2013

Martha Mwaipaja; Natamani waimbaji tungetoa albam moja


Matha Mwaipaja akitumbuiza katika moja ya tamasha

“NINGEKUWA na uwezo ningewakusanya wasanii wote wa muziki wa injili  nikawaambia hebu tuimbe pamoja na kutoa albam ya pamoja, lakini ni jambo gumu kufanya hivyo,”  ndivyo asemavyo  msanii wa muziki wa injili Martha Mwaipaja. 

Ni msanii kijana ambaye amekuwa akifanya huduma ya uimbaji sio tu katika kumnufaisha yeye, akiwa amelenga kuwapa watu ujumbe wa Mungu.

Anasema kwa kusikiliza muziki wa injili watu wengi wamekuwa wakiponywa kiroho na kubadilika matendo yao, kwa kuacha mabaya, na kumgeukia Mwenyezi Mungu.

Hilo kwake linampa faraja kubwa hasa kuona kuwa muziki wake umekuwa ukiwabadilisha watu. Wasikilizaji au mashabiki wake wamekuwa  wakimuunga mkono katika kununua na kusikiliza na hatimaye kuelimika na kubadilika kimatendo.

Anasema alianza kuimba muziki akiwa ni mtoto mdogo. Alilelewa katka mazingira ya kidini ambayo yalimjenga kimaadili.

Msanii huyo  amekuwa akiimba nyimbo zake kwa mtindo wa taratibu na kwa unyenyekevu. Kwa watu ambao wamekuwa wakimfuatilia wanatambua kipaji  cha pekee alicho nacho mwimbaji huyo.


Anasema mara nyingi unaweza kuwa unawaza kufanya jambo fulani lakini lisifanikiwe. Katika historia yake ya muziki jambo ambalo alitamani kulifanya ni kushirikiana na wanamuziki wanzake wa muziki wa injili na kufanya huduma ya pamoja.

Hiyo ilikuwa ni ndoto ambayo bado anahisi kuwa ni jambo gumu kukubalika kwa wasanii wenzake.
Wengi wamekuwa wakifanya kazi peke yao wakitegemea kunufaika, jambo la kufanya pamoja, labda ingekuwa kwa wimbo mmoja lakini kutoa albam moja ni kitu kigumu.

Mwimbaji huyu ambaye ni mwenyeji wa Mbeya anasema hafanyi sanaa bali ni huduma. Akimaanisha kuwa anachokiimba  amelenga kiwaponye watoto, vijana, wazee na watu wote wanaomsikiliza.

Licha ya kuwa alianza huduma hiyo akiwa ni mtoto lakini rasmi alianza kuimba muziki mwaka 2011 na wakati huo alikuwa ni kijana mwenye umri wa miaka 21.

Ndani ya mwaka huo alifanikiwa kutoa albam inayofahamika usikate tamaa yenye nyimbo   nane kama vile wewe ni baba, tulipotoka ni mbali, asante Yesu, Bwana ni nuru, mimi ni mpitaji, na mataifa yote yamshukuuru Mungu.

Anajivunia kuwa albam hiyo imempa matunda makubwa ingawa hakupenda kusema ni matunda gani , lakini zaidi akilenga kwamba watu wengi wamebarikiwa kupitia nyimbo hizo.

Karibu nyimbo zake zote zilikuwa zikifanya vizuri katika chati za muziki wa injili na hivyo kumtambulisha kitaifa na kimataifa. 

“Nashukuru Mungu albam yangu ya kwanza iliweza kufanya vizuri kwasababu nilikuwa nikialikwa kufanya huduma ya injili kupitia uimbaji sehemu mbalimbali hapa nchini, lakini pia, nimefanya huduma Kenya, hii inanipa faraja kubwa kuona kuwa watu wanabarikiwa,”anasema Martha.

Wapo baadhi ya wasanii hasa wanaoimba muziki wa kidunia wamekuwa wakitoa wimbo mmoja mmoja, wakidai kuwa ndio unalipa kwa vile wamelenga zaidi kwenye biashara.

Wengi wanapotoa wimbo mmoja hutegemea kupata shoo ambazo humlipa zaidi. Wanasema albam hailipi, ndio maana hawatoi.

Kwa upande wa muziki wa injili ni tofauti kidogo, licha ya kuwa wamelenga kutoa huduma kwa asilimia  wengi ni lazima watoe albam.

Mashabiki wa muziki wa injili hupendelea kununua albam ya msanii mmoja,mmoja kutokana na kuvutiwa na jinsi anavyoimba na anavyopokea uponyaji.

Martha ana albam ya pili kwa sasa inayofahamika kama ombi langu kwa Mungu ambayo nayo huendelea kufanya vizuri sokoni. Ndani yake kuna nyimbo nane kama jaribu kwa mtu, nabii wa mtu ni wa karibu, Yesu ni mzuri,  kweli nimetambua, kaa nami tena, nani ajuae na sifa zivume.

Anasema “nawomba mashabiki wangu waendelee kuniunga mkono katika huduma hii, kwa sasa albam yangu iko sokoni, natumai kwamba kwa kusikiliza nyimbo zangu mtazidi kubarikiwa,”.

Akizungumzia zaidi kuhusu album yake hiyo mwimbaji huyo ambaye alifunga ndoa mapema mwaka jana  na mchungaji  wa Kanisa la Udhihirisho  John Said, amesema anamshukuru Mungu kwani tayari kila anapoenda kwenye huduma watu tayari wamekuwa wakibarikiwa na kukutana na Mungu kupitia nyimbo hizo mpya kama ilivyokuwa kwa album yake ya kwanza iitwayo ''usikate tamaa'' 

Hata hivyo, kutokana na kuendelea kufanya vizuri katika anga ya kimataifa kwa mwaka huu nyota yake iling’ara baada  ya kupendekezwa kwa mara ya kwanza kuwania tuzo za injili za Afrika ziitwazo Africa Gospel Music Awards(AGMA) ambazo zilitarajiwa kutolewa jijini London. Kitendo cha kupendekezwa kwenye tuzo hizo, zilionyesha kukubalika kwake kwenye ukanda wa Afrika na hata Ulaya licha ya kuwa wakenya wengi na wasanii wa Afrika walionekana kufanya vizuri zaidi.

Martha mwenye sura ya upole anazungumzia suala la kuokoka kuwa si kazi ngumu bali kuutunza wokovu ndiyo kazi. 

Aliwahi kusema kuwa  si jambo la ajabu kusikia mtu amesimama madhabahuni na kutangaza kuwa ameokoka na kupigiwa makofi na waamini kutokana na uamuzi huo. Lakini siri ya wokovu hubaki moyoni mwa mhusika. 

Anasema maisha yake yote anategemea wokovu kwani ndiyo dira yake ya kumwezesha kufanikiwa kwa kila jambo,  atakuwa karibu na Mungu hivyo itakuwa rahisi kujibiwa mahitaji yake atakayokuwa anayomba kutoka kwa Muumba wake. 

“Mungu anasema ukimheshimu naye atakuheshimu, sipendi niwe kama bango la kuwaelekeza watu kwenda kwenye uzima wa milele halafu mimi niende jehanamu. Nawaomba waimbaji wenzangu  tuwe mfano kwa jamii inayotuzunguka,”anasema.

Anawaeleza  waimbaji wenzake kuwa na umoja ili kudhihirisha ukweli kwamba wao ni watumishi wa Mungu wanaositahili kuigwa na  jamii inayowazunguka.

Martha anategemea kupata mtoto wake wa kwanza siku za karibuni hivyo anamwomba Mungu awe pamoja naye katika kuisimamia  na kuitengeneza familia yake mpya.
Mwisho. 




1 comment: