Kazaura katikati akiwa katika maonyesho ya bidhaa zake na wasaidizi wake |
Unajua kuwa simu husaidia kukuza biashara yako?
Wilson Kazaura ni mjasiriamali wa bidhaa mbalimbali ambaye
amekuwa akiuza bidhaa mbalimbali za nafaka ambazo hulimwa mkoani Kagera
zikiwemo maharage, njugu mawe, nyanya chungu ndogo ndogo, mpala, mashasha, senene na Samaki aina ya pina ya
mboju.
Bidhaa nyingine ni pamoja na vikapu ambavyo hutumika kutolea
mahari kwa wahaya, kata ya kubebea kikapu hicho, vibuyu ambavyo hutumika
kunywea pombe za asili, kahawa, pilipili na vitu vingine
Kazaura anaeleza kuwa kabla ya kuanza kuuza bidhaa hizo,
mwaka 2004 alianza biashara ya samaki ambapo alikuwa akisafiri Mwanza, Musoma
na Kagera na kununua bidhaa hiyo kwa wachuuzi wadogo na baadaye kurudi Dar es
Salaam na kuanza kutembeza nyumba kwa nyumba.
Wakati anafanya hivyo alikuwa akiendelea kutengeneza mtandao
kila mahali anapopitisha bidhaa hiyo ya samaki. Anachukua namba za simu za
wateja wake na kuzihifadhi ili anapokuja na bidhaa mpya awajulishe wateja na
hivyo kuwafikishia kiurahisi.
Anasema “kule ambako nilikuwa naenda kuchukua samaki
nilikuwa naendelea kutengeneza mtandao na wale wachuuzi hivyo walianza
kuniamini na baadaye nikaona sasa niagize kwa wale wachuuzi waniletee kuliko
niwafuate kule,”
Kwa vile tayari alikuwa na mtandao mkubwa biashara hiyo ya
samaki ilianza kumwendea vizuri na hivyo kukuza mtaji wake kwani kwa kadri siku
zilivyokuwa zinakwenda nay eye ndivyo alivyokuwa akizidi kutengeneza mtandao wa
kibiashara ambapo alipata wateja wengine wakubwa katika mahoteli mbalimbali
jijini Dar es Salaam waliokuwa wakimwagiza awapelekee samaki.
“Namshukuru Mungu kutokana na juhudi zangu watu waliniamini
nikawa napata oda nyingi ambapo nilikuwa naleta samaki wengi na nilikuwa nafanikiwa
kumaliza ndani ya siku moja, kwani nilikuwa nikipata samaki nawajulisha wateja
wangu na hivyo kuniagiza niwapelekee,”anasema.
Baada ya mwaka mmoja, Kazaura alipata wazo la kufungua duka
ili aweze kuendeleza biashara sio tu upande wa samaki bali pia kuuza bidhaa
nyingine. Lakini mawazo yalikuwa tofauti na wajasiriamali wengine kwani yeye
aliona ni bora auze bidhaa zinazotoka mkoani Kagera ambako ndiko alikozaliwa
ili kuwaunga mkono wakulima wa mkoa huo.
Anasema duka lake
lipo Sinza na wateja wake wakubwa ni wahaya wenzake na wamekuwa wakitoka sehemu
mbalimbali hadi eneo hilo ili tu kufuata bidhaa za kwao ambazo zimeonekana kuwa
kivutio kikubwa.
Utaratibu aliojiwekea katika duka lake ni wa ubunifu wa aina
yake na bado maduka mengi katika sehemu mbalimbali bado hawajaugundua. Kwanza
ukifika katika duka lake unakaribishwa kwa ukarimu na mara unaponunua bidhaa
kuna kitabu kwa ajili ya wateja ambapo unaandika jina lako na kuweka namba za
simu ili kuwa rahisi anapoleta bidhaa mpya kujulishwa.
Anasema simu ambazo huachwa na wateja wake huhifadhiwa kwa
uaminifu, ambapo mara tu bidhaa zinapoingia kutoka Bukoba kila mteja aliyeacha
namba yake ya simu anatumiwa ujumbe mfupi wa kumjulisha kwamba tayari mzigo
umeingia hivyo wanakaribishwa kutembelea duka hilo na kuchagua kile
wanachokitaka kulingana na bei anayoweza mteja.
Na anachojivunia ni kuungwa mkono na wahaya wenzake kwa
asilimia kubwa kwa vile zile bidhaa nyingi hufahamika kwa Wahaya. Na wanapoenda
katika duka lake wanakuwa na uhakika wa kujikumbushia utamaduni wa vyakula vyao
walivyivisahau.
Wateja wake sio tu kwamba wapo Sinza peke yake, bali
wanaishi Mbagala, Kawe, Kimara, Bunju, Kigamboni na karibu sehemu zote za Dar
es Salaam. Wamekuwa wakisafiri kutoka maeneo wanayoishi hadi Sinza bila kujali
kwamba kuna umbali mkubwa wa safari yenyewe.
Lakini Kazaura anasema wateja wake wamekuwa wakilalamikia
ugumu wa usafiri wakati mwingine, hivyo ili kuwaridhisha anajipanga ili
kuhakikisha anafungua matawi manne ambako wateja ndiko wanakotokea kwa wingi ili
kuwarahisishia wateja wake.
“Baada ya miaka miwili ndio nitaangalia uwezekano wa
kufungua matawi manne kwa ajili ya kuwafikishia wateja wangu huduma karibu ili
wasipate shida kwasababu kuna wengine wanalalamikia ugumu wa usafiri,”anaeleza
Kazaura.
Kazaura anasema wakati anaanza biashara alikuwa akijikuta
kwenye wakati mgumu hasa pale ambapo mtaji ulikuwa unakata kutokana na bidhaa
nyingine kuoza. Lakini hakukata tamaa zaidi aliona ni bora akope aendeleze
biashara yake na ndipo kufanya hivyo na hatimaye leo anajivunia kwa mafanikio
anayoyapata.
Kitu anaona ni kikwazo kikubwa katika biashara yake ni
kukatika kwa umeme kila wakati. Anasema kitendo hichi kimesababisha hasa katika bidhaa zake hasa zile ambazo hutegemea
friji zimekuwa zikioza na hivyo kusababisha hasara.
Anachopendekeza ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
kufanya jitihada za kupunguza tatizo la umeme kama ambavyo wameahidi wananchi.
Anasema tatizo hilo iwapo litapungua litawasaidia wafanyabiashara wengi kuokoa
mali zao.
Mjasiriamali huyo anasema
kupitia biashara hiyo amefanikiwa kujenga nyumba ya kisasa, kuwapeleka watoto
wake katika shule nzuri pamoja na kuendelea kukuza mtandao wa biashara.
Anasema hajawahi kushiriki katika maonyesho yoyote ya
kibiashara, kufika kwake katika maonyesho ya Wahaya ni fursa anayojivunia.
Anaamini kuwa huo ni mwanzo kwa vile tayari ameshafunguliwa njia anajipanga ili
aweze kushiriki katika maonyesho makubwa ya bidhaa kama vile Sabasaba ili azidi
kutangaza biashara yake.
Anasema siri nyingine iliyomwezesha kujenga mtandao ni
kwamba sio tu huwajulisha wateja wake kuhusiana na bidhaa mpya, bali pia msimu
wa sikukuu huwatumia wateja wake wote ujumbe mfupi wa maneno kwenye namba za
simu za wateja kuwatakia heri ya
sikukuu. Kwa njia hiyo pia mteja anajivunia na kuvutiwa zaidi.
Vijana wengi huogopa kuthubutu na wengine hawana ubunifu wa
kuwavutia wateja ili kesho aweze kurudi tena. Matokeo yake wanapoanza biashara
huishia njiani na wengine wanakula mtaji na wengine hukata tamaa pale wanapoona
wanapata hasara fulani.
Kazaura anawaeleza vijana kutokata tamaa, jambo la muhimu ni
kuthubutu. Anasema kuna wengine wanaogopa kupitisha bidhaa mtaani kwasababu tu
ni msomi hivyo anaogopa kuchekwa, wengi wanataka kufanya kazi za ofisini.
“Unapotaka kufanikiwa usiogope wala kuchagua kazi, jenga
uaminifu, jitoe muhanga, usitegemee kazi za ofisini ili uajiriwe, kufanya kazi
kwa bidii na kwa uaminifu ni njia pekee itakayokuwezesha kufanikiwa
kibiashara,”anasema Kazaura.
Vijana ambao huogopa biashara wanaweza kujifunza kupitia kwa
mjasiriamali huyu, amepitia vikwazo vingi lakini hakukata tamaa na leo ameweza
kutimiza ndoto yake.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment