TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday, 7 May 2012

TCIB yatoa Hati ya Uchaguzi kwa Tume ya Uchaguzi


 Na Mwandishi wetu
 Kituo cha Utoaji Taarifa (TCIB) kimetoa hati ya uchaguzi huru na haki kwa asilimia 70 kwa Tume ya Uchaguzi  nchini kutokana kufanikiwa kusimamia uchaguzi kwa uhuru, amani na haki katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni katika jimbo la Arumeru Mashariki .

Wakizungumza na waandishi wa Habari viongozi wa Kituo hicho walisema wametoa asilimia 70 kwa tume hiyo pia kutokana na kuboresha baadhi ya mapungufu yake ikiwemo ni pamoja na maboresho ya mfumo wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho Deus Kibamba alisema Tume ya uchaguzi imefanya maboresho katika daftari la kupiga kura nab ado imeonyesha mipango yake ya kuboresha ambayo itatangaza siku za karibuni.
Pamoja na hati hiyo, kuna mapungufu ambayo wameyaeleza kwamba yametokea wakati uchaguzi unafanyika kuwa ni pamoja na rushwa, vitisho kwa viongozi wa kisiasa na  lugha za matusi.

Akizungumzia mapungufu hayo Afisa Tawala wa Kituo hicho Debora Mushi alisema wakati wa uchaguzi kulikuwa na magari yanayokimbizana ili kutoa rushwa hivyo kuitaka  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwajibika ipasavyo dhidi ya watu hao.

Pia, alisema kuna baadhi ya boda boda zilikuwa zinafuata msafara wa wanasiasa lakini jambo la kushangaza walikuwa wakifika eneo la tukio wanadai fedha kitu ambacho kilikuwa sio sahihi kwasababu hawakulazimishwa kujiunga kwenye msafara.

Vile vile, alisema lugha ya matusi ilikuwa ikitumiwa na wagombea wa vyama nane ambavyo vilikuwa vikipiga kampeni, kwani badala ya kuzungumzia changamoto zinazoikabili Arumeru wanazungumza matusi kwa wananchi hivyo wanahitaji kuwajibishwa.

 Alisema katika vyama vyote hakuna mwanamke aliyejitokeza kugombea na wengi walikuwa wakiulizwa wanadai kuwa hata kuchaguliwa nguvu ya pesa ndiyo ilikuwa inatumika kwa asilimia kubwa na wengi wenye nia hawana kipato cha kuwafanya wachaguliwe

No comments:

Post a Comment