Wakati mahakama hizo zinafikia ukomo hii leo (18-06-2012) serikali ya Rwanda inasema Gacaca zimepata mafanikio kuliko ilivyotarajiwa. Hatahivyo, mashirika ya haki za binadamu hayajaridhishwa na namna ambayo mahakama hizo zimeshughulikia baadhi ya kesi , yakisema kwamba hayakutoa hukumu kwa haki.
Dhima kubwa ya Gacaca ni ipi?
Mahakama za Gacaca zilipoanzishwa mwaka 2002, dhumuni lao kuu lilikuwa ni kutoa haki na kuimarisha mapatano miongoni mwa wanajamii ambao wamesambaratishwa kufuatia mauaji hayo.
Takriban watu laki nane, wengi wao wakiwa wa kabila la Kitutsi na Wahutu kiasi waliuwawa katika kipindi cha siku 100, na kwa kutilia maanani ukubwa wa uhalifu uliofanyika, kulikuwa na watu wengi waliokuwa na hatia hali iliyosababisha changamoto kubwa kuamua kesi hizo kwa haki.

"Sidhani kama kuna mahakama ile duniani iliyotoa hukumu kwa kesi milioni 1.9 katika kipindi cha miaka 10.Kwa hivyo kama mahakama hizi zimefanikiwa kukusanya ushahidi, kutoa hukumu na kuwatia watu hatiani, basi unaweza kusema mahakama za Gacaca zimefanya vizuri kuliko mahakama yoyote ile." anasema Karugarama.
Mahakimu walipatikanaje?
Mahakimu waliokuwa wakiendesha kesi hizo walichaguliwa na watu miongoni mwa jamii, wengi wao kutokana na uadilifu wao. Idadi kubwa ya mahakimu hao hawakuwa na mafunzo yoyote ya kisheria, lakini walipaswa kutoa hukumu katika kesi ambazo ni tata mno.
Katika ripoti yake ya mwaka 2012, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch, lilisema ukosefu wa weledi pamoja na mapungufu mengine yalichangia mahakama hizo za Gacaca kushindwa kufikia viwango vya kimataifa vya utoaji wa hukumu.
Msimamo wa Human Rights Watch
Carina Tertsakian ni mtafiti mkuu wa Kitengo cha Afrika cha shirika la Human Rights Watch na hapa anaeleza "Nafikiri pamoja na nia njema ya dunia, itakuwa ni jambo lisilo sahihi kutegemea watu wasiokuwa na utaalam wowote wa kisheria kushughulikia kesi kama hizo."

"Haihitaji mtu kusomea sheria kuona au kusikia kwamba mtu fulani alifanya jambo hili. Haihitaji mtu kuwa na stashahada ya sheria, haihitaji akili ya ajabu kujua kwamba huu ni ukweli." Anafafanua zaidi Waziri huyu wa Sheria.
Na wakati mahakama hizo zikifikia ukomo wake tarehe 18 mwezi huu, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema utulivu unaoshuhudiwa sasa Rwanda unatokana na nguvu ya serikali, huku maelfu wa watu wakiwa wamekimbilia nchi jirani, wakizikimbia mahakama za Gacaca, ambazo Shirika la Human Rights Watch linasema baadhi ya hukumu zilitolewa kwa kuegemea ugomvi na tofauti za nyuma.
Chanzo cha habari:DW Swahili
No comments:
Post a Comment