TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday, 20 August 2012

Na Gazeti la Tz Daima:Masheikh wamgomea Mufti

•  Wasambaza tamko la kutotambua uteuzi wake wa makadhi

Na Waandishi wetu 
WAKATI waumini wa dini ya Kiislamu wakisherehekea Sikukuu ya Idd el-Fitri, baadhi ya masheikh, wanaounda jopo la masheikh 25 kutoka taasisi na jumuiya mbalimbali za Kiislamu Tanzania wamesambaza tamko la kumpinga Mufti wao, Sheikh Shaaban bin Simba.

Katika tamko hilo ambalo lilisomwa katika misikiti mbalimbali jana wakati wa swala ya Idd el-Fitri, masheikh hao wanawahimiza Waislamu nchini kutotambua nafasi za makadhi walioteuliwa hivi karibuni na kiongozi huyo, kwa madai kuwa uteuzi huo ni batili.

Wakizungumza wakati wa swala za Idd el- Fitri katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, masheikh hao walidai kuwa kitendo cha Sheikh Simba kuteua makadhi wakati mazungumzo baina yao na serikali yanaendelea ni sawa na ‘usaliti’ kwa umma wa Kiislamu.

Akisoma tamko hilo katika ibada iliyofanyika katika Uwanja wa Tip Top eneo la Sinza Darajani, Katibu wa umoja huo, Sheikh  Ibrahim Ghullaam, alipinga uteuzi huo akisema kuwa masheikh walioteuliwa na Sheikh Mkuu wa BAKWATA kuwa makadhi, waliteuliwa bila kufuata misingi ya kisheria ya namna ya uteuzi wa makadhi.
Tamko kama hilo pia limesomwa na Mkuu wa Taasisi ya Istiqama, Sheikh Nassoro wakati wa ibada ya Idd kwenye Msikiti wa Ibaadh uliopo Kitumbini, likisema kimsingi Sheikh Simba hana mamlaka ya kuteua  makadhi kwa kuwa yeye ni kiongozi wa taasisi moja ya BAKWATA.

“Yeye ni kiongozi ambaye ana upande wake anaouongoza, zipo taasisi nyingine za Kiislamu 25, inakuwaje mtu mmoja anafanya uteuzi kwa niaba ya wenzake? Tunasema uteuzi huu ni batili na tunawaomba Waislamu wote tusiuunge mkono,” alisema Sheikh Ghullaam.

Katika tamko hilo lenye vipengele vinne ambalo nakala yake Tanzania Daima linayo, viongozi hao walisema inashangaza kuona uteuzi huo unafanywa wakati huu ambapo mazungumzo na serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu yakiendelea.

Kwamba makadhi hao walioteuliwa hawana ‘mashiko’ kisheria ambapo hawatakuwa na uwezo wa aina yoyote katika maamuzi, hivyo kufanya matatizo mengi kupelekwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Ghullaam, taasisi zote 25 zinazounda umoja huo zikiwamo ya Umoja wa wanazuoni Tanzania, Shura ya Maimamu Tanzania, Baraza Kuu la Taasisi ya Kislamu, jopo la masheikh 25 waliokuwa  wakifuatilia Mahakama ya Kadhi, pamoja na Jumuiya ya Baraza la Sunna Tanzania na nyinginezo, wanapinga uteuzi huo.

Pia Amiri Mkuu wa Taasisi ya Enser  Sunneh, Sheikh Juma Omary Pori, alisoma tamko hilo wakati wa swala iliyofanyika katika viwanja vya Kinondoni pamoja na Imamu Mkuu wa Msikiti wa Idrissa uliopo Kariakoo, Sheikh Ally Basaleh.
Wakati huo huo, Waislamu wametakiwa kuhakikisha wanauendeleza uadilifu na mafundisho ya dini hiyo ili kudumisha amani na usalama wa Watanzania kusudi waweze kujenga jamii iliyo bora kiroho na kimwili.

Kauli hiyo ilitolewa kwenye ibada ya swala ya Idd el-Fitri iliyofanyika katika Msikiti wa Mkoa wa Ruvuma uliopo mjini Songea na kuwashirikisha mamia ya waumini wakiongozwa na Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania, Issa Shaaban bin Simba.
Imamu wa msikiti huo, Sheikh Shaaban Mbaya, katika maombi maalumu ya kuliombea taifa na viongozi wake wapate afya njema na uwezo wa kuwatumikia Watanzania ili wawe na amani, alisema kuwa Waislamu hawatakiwi hata kidogo kumbagua mtu yeyote katika maisha yao ya kila siku.

Alisema, mafundisho ya dini hiyo yanasisitiza upendo na amani ili kuenzi uumbaji wa Mwenyezi Mungu, ambaye ni mwingi wa rehema.

Aliwataka waumini hao wafuate mafunzo kutoka kwa kiongozi wao, Mtume Muhammad (SAW), ambaye aliweza kuwatunza mayatima na watu wasiokuwa na uwezo kiuchumi ambao si Waislamu na Waislamu ili wapate furaha ya maisha yao.

Wamsifu JK kuhusu Malawi
Katika hatua nyingine, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Juma Tagalile, amempongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa hatua yake ya kuanza kulitafutia ufumbuzi bila mapingano suala la mgogoro wa mpaka baina ya Tanzania na Malawi.
Sheikh Tagalile, aliwataka Watanzania  pamoja na viongozi wa dini  zote nchini  kuendelea  kuliombea taifa ili  lisiingie  katika machafuko ya vita na Malawi.

Pongezi hizo alizitoa jana wakati akitoa  salamu za Sikukuu ya Idd el- Fitri ambayo katika Manispaa ya Iringa ilifanyika kwenye viwanja vya Samora.

Alisema  kuwa  hatua ya Rais  Kikwete kuanza  kulitafutia ufumbuzi  suala  hilo imepokewa kwa furaha kubwa na Watanzania  kwani kauli za baadhi ya viongozi kuwa anzania iko tayari kwa vita ziliashiria uhasama.

Sheikh Tagalile  alisema  kuwa pamoja na  kuwa  Malawi na  Tanzania  wanagombea mpaka  huo katika  Ziwa  Nyasa, bado viongozi  wa pande zote mbili wanapaswa  kuendelea  kutumia hekima  zaidi katika  kutatua  suala  hilo  kuliko kutaka  kutumia nguvu  zaidi.

Aliongeza kuwa kauli ya  Rais Kikwete  juu  ya suala  hilo imewatuliza  Watanzania hasa wa maeneo hayo ya mpakani, vinginevyo kauli za kujiandaa kwa vita zilizotolewa na viongozi zilikuwa zikitia hofu.

Ushiriki wa sensa 
Kuhusu sensa ya  watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchini kote kuanzia Agosti 26 mwaka huu, Tagalile amewahimiza Waislamu mkoani humo  kushiriki mchakato huo bila  kurubuniwa na mtu yeyote.

Alisema  kuwa sensa ya  watu na makazi  ni  mhimu kwa Watanzania wote  bila kujali itikadi za dini, vyama wala rangi, na  hivyo  kuwataka waumini wa dini  hiyo kupuuza maneno ya mitaani dhidi ya  sensa.

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Juma Luwuchu, aliwataka waumini hao, kuvipuuza vikundi vya masheikh wachache wenye lengo la kuvuruga amani na mshikamano vinavyowahamasisha wasishiriki sensa.

Sheikh Luwuchu alisema kitendo cha masheikh hao kuwahamasisha wananchi wasusie sensa ya watu na makazi ni dhambi kubwa, kwa kuwa kinawaposha wananchi katika kupatiwa haki zao za kijamii baada ya kuhesabiwa.

Habari hii imeandaliwa na Shehe Semtawa (Dar), Stephano Mango (Songea) na Francis Godwin (Iringa).

No comments:

Post a Comment