TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 29 October 2012

Dini zinavunja mipaka kuingilia sheria za nchi

Mimi kama Mtanzania nadhani sasa Dini zinavuka mipaka kuingilia Serekali na sheria za nchi. Serekali iliyopo madarakani iliekwa na Watanzania kwa kupiga kura Kikatiba na Rais akapatikana na akaapishwa kuiongoza Tanzania kwa ridhaa ya Watanzania. Kitendo cha Rais kuapishwa ni kwamba hata mwenyezi Mungu amebariki uteuzi wake na kuikubali Serekali iliyopo madarakani.

Kinachonishangaza ni kuona Dini sasa zinavunja Katiba ya nchi na sheria za nchi kwa kuingilia majukumu ya Serekali na Mahakama ambazo kikatiba ndizo zinatoa haki kwa kila mtu. Haki ya kisheria za uhalifu haitolewi Makanisani wala Misikitini. Mhalifu anapofanya makosa ya jinai au uhalifu wa aina yoyote ile haki yake inapatikana Mahakamani na sio Kanisani wala Misikitini.

Watu wanaolalamika kuwa Mtoto kakojolea Msahafu walikuwepo wakati kitendo kinafanyika na hawakuchukua hatua yoyote kufanya vikao vya pamoja kufanya maamuzi yaliyo sahihi kulingana na sheria za Dini wala Sheria za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati watu wanajichukulia sheria mikononi mwao kuchoma Makanisa na kuharibu mali za watu sikuona Mzee wa Kanisa, Shehe wa Msikiti, wala Mkuu wa Wilaya wala Mkuu wa Mkoa aliyetoka kuwaomba vijana wasiharibu mali. Wengi wa watu hawa walikaa majumbani mwao kuangalia Television huku wengine wakicheka na kushangilia na Wangine wakilia na kusononeka. Mimi nawajua wanadamu ndivyo ilivyokuwa siku hiyo.


Mimi nilichoona ni Jeshi la Polisi kuingilia kati sakata hilo na kufanikia kuzima vurugu hizo kwa maana hiyo Jeshi la Polisi liliona ni jukumu lake kuingilia kati uvunjifu huo wa amani na uharibifu wa mali za Watanzania waliojinyima kuzitafuta ili kujiendeleza na kuipatia Serekali kipato. Hili ni kosa la jinai kisheria na Watanzania wanatakiwa wawe watulivu wakati Serekali na Mahakama zinafanya kazi yake Kikatiba ya kutoa maamuzi. Endapo Kanisa au Msikiti utakuwa unaingilia sheria za nchi mimi sioni sababu ya kuwa na Serekali, Katiba, Sheria na Mahakama. Hivyo naiomba Serekali hivi vikao vinavyofanyoka sasa katika Makanisa yetu na misikiti kuzungumzia watu waliopo chini ya mikono ya Serekali, chini ya mikono ya Sheria wachunguzwe na waunganishwe kwenye makosa yale yaliyotokea. Ilianza hivyo kidogo kidogo ndio ukatokea uvunjifu wa amani. Serekali ya mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete itafute mda ikae na wakuu wote wa Serekali za Wilaya, Mikoa, wakuu wa Misikiti, na Makanisa kuinya hilo. Ili kesho hivyo vikao hivyo vya usiku visije kutuletea balaa. Hakuna mtu yuko juu ya Serekali, Katiba ya nchi na Sheria za nchi. Hivyo vikao vya usiku vya kutetea wahalifu ni uhalifu vile vile. Kwa hili naomba Serekali na Jeshi la Polisi wajipange. Usipoziba ufa utajenga ukuta.

Katiba ya nchi inaeleweka, na Sheria za nchi pia zinaeleweka. Anayefanya maamuzi ya kesi zote za jinai na uhalifu wa aina yoyote ile ni mahakama na sio Kanisa wala Misikiti. Mimi nawashauri watu wanaojaribu kuingilia mihimili ya sheria za nchi wachukuliwe hatua za haraka sana bila kujali Dini zao. Nchi inaendeshwa na utawala washeria na sio Makanisa na Misikiti. Kila muumini najua Sheria za nchi na sheria za Dini yake. Kama wewe ukijaribu kuvunja Katiba ya nchi na sheria za nchi kwa kutegemea kuwa Waislamu au Wakristo wataandamana ili utoke imekula kwako. Hatutavumilia nchi iingie kwenye vurugu za kidini na machafuko eti kwa kuwa Mkristo au Muislamu kawekwa rumande kwa ama kuua, kuharibu mali, kukashifu Serekali au vinginevyo.

Kwa hili naishauri Serekali ikae na hawa wakuu wote wa Dini na kuweka bayana kwao kuwa Serekali na Sheria za nchi ni namba moja Dini inafuatia. Kama hakuna Serekali na sheria nchi haitatawalika. Serekali ikiruhusu kila mtu, kila Dini au kila muumini kufanya maamuzi yake hii nchi itakuwa Somalia. Mwisho naiomba Serekali ichangie kwa hali na mali kujenga Miundo mbinu, Makanisa, Misikiti, na kila eneo lililoharibiwa na vijana wetu kwani sisi ndio tunachelewa kutoa somo la malezi kwa jamii. Kama Makanisa na Misikiti haitakuwepo tutaanzisha vijiwe haramu. Sisi ndio tunalea uozo katika familia zetu. Serekali ikichangia ni kila Mtanzania atakuwa amechangia hivyo kila mtu itamuuma na sio rahisi tena Wazazi kuruhusu au kuachia watoto kuwa waharibifu. Mimi narudia tena kwa hili la vikao vya usiku vya kuijadili Serekali, Katiba ya nchi, na Sheria za nchi IGP Mwema usicheke nao watakupaka kinyesi. Wewe ni Kamanda uliyepewa rungu la kuchunga Raia na mali zao usifanye masihara. Kila anayevunja Katiba na Sheria za nchi lazima aende lupango, hakuna cha mototo wa Tumboni wala Mgongoni. “MCHELEA MWANA KULIA HULIA YEYE”
Mkereketwa.
Lengai Ole Letipipi

No comments:

Post a Comment