Na Adrophina Ndyeikiza wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
31/11/2012.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Said Meck Sadiki ametoa tamko
kali la kuwataka Waislam kuacha mara moja kufanya maandamano yao yaliyopangwa
kufanyika siku ya Ijuamaa ya tarehe 02/11/2012 mara baada ya swala ya Ijumaa.
Kwa mujibu wa vipeperushi vilivyoandikwa na kusambazwa na Jumuiya
na Taasisi za Kiislam (Tz),vimewataka waislam kufanya maandamano makubwa
kuelekea katika Ofisi ya Mhe.Waziri Mkuu kwa upande wa Dar es Salaam na Mikoani
maandamano hayo yataelekea kwa wakuu wa Mikoa aidha kwa upande wa Zanzibar
yataelekea Ofisi ya Makamu wa Rais.
Aidha,Sababu ya kuandamana kwao wameelezea kuwa ni
kushinikiza Serikali kutenda haki kwa wananchi wote bila ubaguzi kwani waislam
wanabaguliwa kwa mambo mengi kama vile;-
-Kudhalilishwa Masheikh wao kwa kukamatwa hovyo bila sababu
za msingi mfano,Sheikh Ponda na Sheikh Farid wakati wakristo hawafanyiwi hivyo.
Akijibu hoja hiyo mbele ya waandishi wa habari Mhe.Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Sheikh Ponda
hakukamatwa kama Sheikh Ponda bali amekamatwa kama mtu yeyote yule ambaye
anaweza kutuhumiwa kwa kosa fulani.Ameongeza kuwa Serikali haikumkamata Sheikh
Ponda kutokana usheikh wake/dini yake au uislamu wake bali kutokana na
kutuhumiwa kwake.Hivyo tuache vyombo vya sheria vifanye kazi yake na haki
itazingatiwa tu. “Alisisitiza Mkuu wa Mkoa”.
-Sababu nyingine ni pamoja na Kudhalilishwa matukufu ya
Waislam huku Serikali ikikaa kimya.Akijibu hoja hiyo pia Mhe.Mkuu wa Mkoa amesema kuwa jambo hili si
kweli kabisa kwani Serikali ilikwishachukua hatua stahiki kwa kumkamata kijana
huyo aliyeyekojolea Koran na kumfikisha katika vyombo vya sheria,hivyo kijana
huyo alikwishakamatwa,hata hivyo wale wote waliokwenda kuchoma makanisa,kupiga
vioo vya magari ya watu na kuiba vitu mbalimbali katika makanisa na ndani ya
magari ya watu nao pia wapo katika mikono ya sheria kwani uislam pia hauagizi
hivyo.
-Sababu ya tatu ni kuundiwa chombo cha kusimamia Waislam kwa
nia ya kuwadhibiti na kulazimishwa Waislam kukitii pamoja na ukweli kwamba
kinafisidi Uislam na Wislam.Akijibu hoja hiyo Mhe.Mkuu wa Mkoa amesema kuwa
kamwe Serikali haiwezi kufanya hivyo,kwani kila chombo kinaundwa na wanajamii
husika na wala Serikali haina dini hivyo haiwezi kuunda chombo chochote kile
cha kidini.Hata hivyo zipo taratibu maalumu za namna ya kusajili taasisi yoyote
ile kwani lazima kueleza mbele ya msajili ya kuwa taasisi yenu ni ipi na ina
malengo gani kwa jamii husika na msajili akilizika na maelezo yenu basi huna
budi kuisajili taasisi hiyo.Taasisi yoyote ile lazima isajiliwe na ifuate
taratibu za sheria,na Serikali inazisikiliza taasisi zote kama zinafuata sheria
na taratibu “Alisisitiza Mkuu wa Mkoa”.
Hivyo basi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Said Meck Sadiki
amesema kuwa Waislam wote wapenda amani wasifanye maandamano yoyote siku hiyo
ya Ijumaa mara baada ya swala kwani kwa kufanya hivyo HATUA KALI ZA KISHERIA DHIDI YA WATAKAOHUSIKA KATIKA KUYAANDAA NA KUSHIRIKI ZITACHUKULIWA kwani maandamano
hayo ni BATILI na hayajaruhusiwa na JESHI LA POLISI. Sheria kali zitachukuliwa katika suala hili
“Alisisitiza Mkuu wa Mkoa”.
No comments:
Post a Comment