Kwa mara nyengine tena Rais Barack Obama
ametajwa kumbwaga Mitt Romney katika mdahalo wa televisheni, ambao licha ya
mada yake kuu kuwa siasa, masuala muhimu kwa wapiga kura, yaani uchumi na
ajira, yalitawala mjadala.
Pakiwa pamebakia wiki mbili tu kabla ya
Siku ya Uchaguzi, Romney aliutumia mdahalo wa jana kushadidia hoja yake kwamba
Obama ameufuja uchumi wa Marekani
"Ili
tuweze kuendeleza misingi hiyo ya amani, tunahitajika kuwa na nguvu, na hilo
linaanza na uchumi imara hapa kwetu, na bahati mbaya uchumi si imara kiasi
hicho.
Pale
rais wa Iraq- samahani- rais wa Iran, Ahmedinejad, anaposema kwamba deni letu
linatufanya tusiwe tena taifa kubwa, hilo ni jambo la kutisha. Mkuu wa zamani
wa jeshi, Admirali Mullen, alisema kwamba deni letu ndicho kitisho kikubwa cha
usalama wa taifa. Tumeudhoofisha uchumi wetu." Alisema Romney.
Mchuano
mkali
Wagombea urais wa
Marekani wakiwakumbatia wake zao baada ya mdahalo wa tatu kati yao.
Wakiwa wanachuana vikali,
hakuna hata mmoja kati yao aliyeweza kumtoa mwenzake nje ya ulingo haraka,
wakati wakilumbana kuhusiana na masuala ya Israel, Iran, Urusi, na ukubwa wa
jeshi la Marekani, katika mdahalo huo uliofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Lynn,
Boca Raton.
Matokeo ya uchunguzi wa
maoni yaliyotangazwa baada ya mdahalo huo, yamemuonesha Obama akiongoza, ingawa
asilimia 60 ya waliotuma maoni yao kwenye kituo cha CNN, walisema Gavana Romney
ana uwezo wa kuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi, akitimiza jukumu lililowekwa na
wasaidizi wake. CNN imempa Obama asilimia 8 mbele ya Romney.
Kura ya maoni ya kituo
cha CBS inaonesha kuwa asilimia 53 ya watu wanaamini kuwa Obama alishinda
mdahalo wa jana, ikilinganishwa na asilimia 23 ya Romney, huku asilimia 24
wakisema wametoka suluhu.
Kwa kuwa siasa za nje ni
kipaumbele cha chini katika kampeni iliyojikita kwenye uchumi, bado si wazi
ikiwa mdahalo huu utakuwa na athari gani kwenye kinyang'anyiro hicho cha urais.
Wachangiaji maoni kupitia kituo cha CNN, walionekana kugawika juu ya suala
ikiwa mdahalo huo ungeliathiri kura zao hapo tarehe 6 Novemba.
Hata hivyo, picha hii ya
Boca Raton ilikuwa ni moja ya nafasi za mwisho mwisho kabisa kwa wagombea wote
wawili kuwanasihi mamilioni ya wapiga kura waliokuwa wakiifuatilia kupitia
televisheni zao, na ambapo Obama ametajwa kujidhihirisha mtundu zaidi ya
Romney.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf
Mhariri: Saumu Yussuf
Chanzo: DEUTSCHE WELLE swahili
No comments:
Post a Comment