TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 19 July 2013

Mbunge awaomba wapiga kura kumvumilia juu ya ahadi za maji

Na Thehabari.com, Kishapu
MBUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Seleiman Nchambi amewaomba wapiga kura wake kuwa wavumilivu juu ya ahadi ya huduma za maji safi na salama alizozitoa wakati akigombea jimbo hilo katika uchaguzi mkuu 2010.

Nchambi ametoa kauli hiyo hivi karibuni akizungumza na mwandishi wa habari hizi kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya baadhi ya wapigakura wake wa Kata ya Kishapu, ambao wamelalamikia kitendo cha kuendelea kutopata huduma za maji safi na salama eneo lao ilhali mbunge wao aliwaahidi kuwapatia huduma hiyo.

Mbunge huyo alikiri kutoa ahadi ya huduma ya maji jimbo zima la Kishapu na utekelezaji wa ahadi zake unaenda awamu kwa awamu kama alivyopanga. Akifafanua zaidi alisema aliingia madarakani na kukuta sehemu kubwa ya jimbo hilo halina huduma ya maji safi na salama, lakini kwa jitihada zake mpaka sasa tayari amefanikiwa baadhi ya vijiji kuvipatia maji.


"Niliahidi maji jimbo zima la Kishapu yaani jumla ya vijiji 114, wakati naingia madarakani nimekuta hali ni mbaya ya huduma za maji...lakini hadi sasa tunapozungumza zaidi ya vijiji 30 vinapata maji safi na salama huku jitihada zingine zinaendelea," alisema Nchambi akifafanua juu ya kilio cha huduma za maji akizungumza kwa njia ya simu.

"Ahadi yangu mimi ni miaka mitano, ilani ya CCM ni ya miaka mitano, ninaenda kwa awamu yaani vijijini 10 kwa kila mwaka kwa wilaya," aliongeza kusema mbunge huyo.

Awali uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa baadhi ya vijiji vya Kata ya Kishapu, mkoani Shinyanga, vikiwemo vijiji vya Lubaga, Isoso, Mwanuru pamoja na Kishapu ulibaini kuwepo na shida kubwa ya huduma ya maji safi na salama hali inayowalazimu wananchi kutembea umbali mrefu hasa kipindi cha kiangazi kutafuta maji.

Hata hivyo uchunguzi ulibaini mzigo mkubwa wa kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama katika familia unawaangukia wanawake na wanafunzi ambao hutumia muda mrefu kusaka maji kwa ajili ya matumizi ya familia. Chanzo pekee cha maji ambacho hutegemewa na maeneo mengi ya vijiji ni cha Mto Tungu ambao nao hukauka kipindi cha kiangazi na wananchi kuendelea kupata maji kwa shida.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni viongozi wa vijiji vya Lubaga, Isoso, Mwanuru na Kishapu walilalamikia kitendo cha wao kuendelea kuteseka kwa huduma za maji ilhali walipewa ahadi ya kuletewa huduma hiyo na mbunge wao kipindi cha kampeni.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lubaga, Enock Manyenye Shimba alisema mwaka 2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kijiji chao kilipewa ahadi ya kuchimbiwa visima virefu vya maji na Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Seleiman Nchambi lakini anashangaa ahadi hiyo haijatekelezwa hadi leo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, George Kessy alikiri hali mbaya ya huduma ya maji Wilaya nzima ya Kishapu kutokana na eneo hilo kutokuwa na chanzo cha maji cha uhakika. Hata hivyo alisema juhudu zinafanywa kuhakikisha uongozi unaondoa kero hiyo ya huduma ya maji kwa wananchi.

"Ni kweli suala la maji ni Tatizo kwa wilaya nzima ya Kishapu, tena ni kubwa sana…,” alisema Kessy.

No comments:

Post a Comment