TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 18 September 2013

Serikali itaendelea kushirikiana na wabia wa maendeleo

18 Septemba, 2013.    
                                                     
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
WAZIRI MKUU: SERIKALI KUIMARISHA UTAWALA BORA  
 
 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wabia wa maendeleo ili kuimarisha utawala bora na hatimaye kusaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi walio katika ngazi za chini.
 
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Septemba 15, 2013) wakati akifungua maadhimisho ya siku ya soko la SULGO (SULGO Market Day) yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Ujerumani (GZI).
 
Waziri Mkuu alisema maonyesho hayo yamelenga kujenga uwezo kwenye Serikali za Mitaa ili waweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi kwa kuwapatia mafunzo yatakayo wawezesha kuwa na vyanzo vya fedha, kuwekewa mifumo ya kupata fedha hizo, kuwezeshwa kusimamia matumizi ya fedha zao na kujengewa ushikishwaji wa wananchi kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya Taifa.
 
“Serikali za Mitaa ndiyo nyenzo kuu ya Serikali katika utekelezajiwa shughuli za serikali, na fedha nyingi zinapelekwa huko ambako miradi ya maendeleo iko. Utaona kuwa kuwa na fedha ni jambo moja lakini kuweza kusimamia matumizi ya zile fedha ni jambo jingine   kwa hiyo wametoa mafunzo kwa watendaji wa vijiji na kata juu ya suala hili,” alisema.
 
Akizungumza na waadhishi wa habari mara baada ya kukagua maonyesho hayo, Waziri Mkuu alisema amefurahi kuona kwamba katika ngazi ya chini kabisa wananchi wamejengewa uwezo wa kutambua sheria ndogo zinatungwa vipi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Waziri mwenye dhamana anapokuja kusaini sheria hiyo.
 
Aliishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia taasisi yake ya GIZ ambayo imetoa Euro milioni 9.8 kwa ajili ya kusaidia mradi huo unaotekelezwa kwa majaribio kwenye wilaya nane za mikoa ya Tanga na Mtwara. Wilaya hizo ni Mtwara, Nanyumbu, Tandahimba na Masasi kwa mkoa  wa Mtwara wakati Mkoani Tanga unatekelezwa katika wilaya za Handeni, Muheza, Jiji la Tanga na wilaya ya Tanga.
 
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua maonyesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bibi Hawa Ghasia alisema soko la SULGO ni dhana ya ushirikishwaji wa wananchi katika kutoa maamuzi kuanzia ngazi ya chini, ngazi ya wilaya na hatimaye ngazo ya Taifa au Serikali Kuu.
 
Alisema dhana hiyo imekuwa ikiendeshwa chini ya Mpango wa Serikali wa Maboresho ya Serikali za Mitaa (LGRP). Alisema mradi huo wa soko la SULGO ulianza Januari 2008 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 2014.
 
Naye Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ujerumani, Bibi Claudia Imwolde-Kraemer alisema mradi huo umelenga kuimarisha utendaji wa serikali za mitaa kwa kufuatilia ukusanyaji wa mapato na kuweka mifumo ya uwajibikaji kwenye masuala ya fedha.
 
“Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya ugatuaji wa madaraka katika ngazi ya vijiji, wilayani na mikoani,” alisema.
 
Alisema anathamini sana muda ambao umetumika katika kuwaelimisha watendaji wa ngazi mbalimbali na ushirikishwaji uliofanyika katika ngazi hizo kwamba vitakuwa chachu ya kuleta mabadiliko kwenye ngazi tofauti za kijamii.
 
(mwisho)
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, SEPTEMBA 18, 2013.

No comments:

Post a Comment