TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 4 October 2013

WAZIRI MKUU AAHIDI MIZINGA YA KISASA 100 BITURANA

 04 Oktoba, 2013.   
                                                           
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameahidi kutoa fedha za kununua mizinga kati ya 100 na 200 kwa ajili ya wanakijiji wa Biturana, wilayani Kibondo, mkoani Kigoma ambao wanajihusisha na uhifadhi wa misitu pamoja na ufugaji nyuki.
 
Ametoa ahadi hiyo jana mchana (Alhamisi, Oktoba 3, 2013) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kijiji hicho mara baada ya kukagua eneo la hifadhi ya Biturana pamoja na baadhi ya mizinga iliyomo kwenye hifadhi hiyo.
 
Alisema kwa vile mizinga hiyo inatengenezwa kwenye wilaya yao kwa thamani ya sh. 50,000 kwa kila mzinga, atawatafutia fedha za kutosha mizinga 100 -200 kulingana na mahitaji yao ambazo ni kati ya sh. milioni 5/- na sh. milioni 10/-.
 
Waziri Mkuu aliwashauri waanze taratibu kuachana na mizinga ya asili na badala yake watumie mizinga ya viunzi na baada ya muda wakishaizoea itabidi wahamie kwenye mizinga ya biashara.
 
“Mizinga ya viunzi ina kasoro moja kubwa kwani humfanya mfugaji alazimike kukata sega zima, wakati hii ya kibiashara inakupa fursa ya kutoa sega ukafyonza asali na kurudisha tena sega hilo kwenye mzinga ili nyuki waanze tena kutengeneza asali nyingine,” alisema.
 
“Lakini kwa sasa hamuwezi kuanza na mizinga ya kibiashara moja kwa moja, ni lazima kuitoa polepole huku wanakijiji wakijifunza jinsi ya kutumia hii mizinga ya kisasa ambayo ni ya viunzi,” alisema wakati akitoa maelekezo kwa Afisa Nyuki wa wilaya hiyo, Bw. Seif Salum Seif.
 
Akisoma taarifa ya mradi wao mbele ya Waziri Mkuu, Katibu wa Kikundi cha Wafuga Nyuki cha Biturana, Bw. Christopher Ibrahim alisema kikundi chao ambacho kilianzoshwa mwaka 2011, kina wafugaji 52 ambao wana mizinga 4,554 ambao kati yao 44 ni wananume na wanane ni wanawake.
 
“Eneo la hifadhi ya Biturana lina ukubwa wa hekta 407.5 na kati ya mizinga 4,554, mizinga 4,457 ni ya asili na mizinga 97 ni ya kisasa.” Alisema kwenye mizinga ya asili, mizinga zaidi ya 4,000 ina nyuki wakati ile 97 ya kisasa yote ina nyuki ndani yake.
 
Kuhusu uzalishaji, Bw. Ibrahim alisema katika msimu wa mwaka 2012/2013, wanakikundi walivuna kilo 3,550 za asali zenya thamani ya sh. milioni 5.08/- na nta kilo 55 zenye thamani ya sh. 275,000/-.
 
Naye Afisa Nyuki wa Afisa Nyuki wa wilaya hiyo, Bw. Seif alimweleza Waziri Mkuu juu ya mradi wa kuzalisha malkia wa nyuki ambao unatarajia kuanza hivi karibuni na kwamba wameandaa mizinga 15 ambayo itatumika kwa kuzalisha malkia kijijini hapo.
 
“Shirika la Maendeleo la Ubelgiji kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo wameanza mpango wa kuendeleza eneo hili la hifadhi ya Biturane na kuamua kujenga kituo cha mafunzo cha kuzalishia malkia kwa gharama ya sh. milioni 4/-,” aliongeza.
 
Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Kigoma, aliwahakikishia wanakijiji hao kwamba Tanzania inaweza kuwa mwamba wa uzalishaji asali duniani na kuipiku Ethiopia ambayo hivi inaongoza kwa kuzalisha tani 40,000 za asali kwa mwaka.
 
“Tukijipanga vizuri tunaweza kuwa mwamba wa uzalishaji asali duniani kwa sababu uwezo tunao wa kuzalisha tani 100,000 kwa mwaka; misitu tunayo na mito tunayo mingi. Wenzetu wale wana jangwa katika sehemu kubwa ya nchi yao lakini waliiona hii fursa ya ufugaji nyuki wakaamua kuichangamkia,” aliongeza.
 
Katika ziara hiyo ya siku sita mkoani Kigoma, Waziri Mkuu amefuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia, Naibu Waziri wa Maji, Dk. Binilith Mahenge, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu pamoja na Naibu Waziri Nishati na Madini, Bw. George Simbachawene.
 
(mwisho)
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, OKTOBA 4, 2013.

No comments:

Post a Comment