TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Sunday 17 November 2013

Bunge lakataa kubariki ‘Division 5’

 Na Gazeti la Mwananchi
 Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, imevikataa viwango vipya vya alama za ufaulu kwa elimu ya sekondari vilivyotarajiwa kuanza kutumika mwaka huu na kutaka utaratibu na alama zilizotumika mwaka jana, zitumike kupanga matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne wa mwaka huu.

 
Serikali ilitangaza utaratibu mpya wa alama za Mitihani ya Kidato cha Nne na Sita kwa kufuta Daraja  la Sifuri na kuleta Daraja la Tano.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stephen Ngonyani  alisema jana kuwa kamati hiyo ilichukua uamuzi huo kwa kuwa pamoja na udhaifu ulio kwenye alama hizo, kamati yao haikuhusishwa katika mchakato wa kuandaa alama hizo. 
“Mwenyekiti wangu (Margaret Sitta) alisema kile hakiwezekani, kuna viwango ambavyo wameleta havipo kwenye nchi nyingine duniani, tumewaambia wakavifanyie kazi walete tena,” alisema mbunge huyo wa Korogwe Vijijini, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Profesa Maji Marefu.
Ngonyani alisema waliagiza watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha wanaishirikisha kamati yao kwani imejaa walimu wanaoweza kushauri vizuri.
“Hatutaki watuletee mambo ambayo yamewashinda baada ya kuyapeleka kwa wananchi,” alisema Ngonyani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome akitangaza uamuzi huo mapema mwezi huu, alisema uamuzi wa kubadilisha mfumo huo umechukuliwa kutokana na changamoto zilizojitokeza mwaka 2012.
Alama zilizokuwa zikitumiwa awali na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), katika kupanga matokeo hayo, kwa Kidato cha Nne ni A=80-100, B=65-79, C=50-64, D=35-49, F 0-34 kwa upande wa Kidato cha Sita, A=80-100, B=75-79, C=65-74, D=55-64, E=45-54, S=40-44 na F= 0-39.
Alama mpya zilizotangazwa ni A=75-100, B+=60-74, B=50-59, C=40-49, D=30-39, E=20-29 na F=0-19. Alama hizo ni kwa kidato cha nne na sita.
Kwa utaratibu huo, A ilitafsiriwa kuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ ni ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.
Katika utaratibu huo, mtihani wa mwisho ulitarajiwa kuwa na alama 60 na alama 40 zitokane na alama za Maendeleo ya Mwanafunzi Shuleni (Continuous Assessment-CA).
Mwaka jana baada ya Serikali kufuta matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne, Necta ilitumia CA ya 30 huku mtihani wa mwisho ukiwa na alama 70.

No comments:

Post a Comment