TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday, 25 November 2013

JK, Mkapa, Mwinyi, Mengi watunukiwa nishani

 Na Gazeti la Tanzania Daima

RAIS Jakaya Kikwete, Rais wa Awamu ya Pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi, Rais Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi wametunukiwa nishani kwa kutambua mchango wao katika kuboresha afya ya mama na mtoto nchini.
 Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilali na Dk. Reginald Mengi
 Nishani hizo zilizokabidhiwa jana na Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilali, zimeandaliwa na Taasisi ya Madaktari Waliosoma Vyuo Vikuu nchini (THPI).

Wengine waliokabidhiwa nishani hiyo ni pamoja na mke wa rais, Mama Salma Kikwete kupitia Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), madaktari na wauguzi waliofanya vizuri katika hospitali zao wanazozihudumia.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mery Nagu, alisema kama mama hatakuwa na afya yenye usalama, taifa nalo halitakuwa salama kwa kuwa taifa lenye afya linatokana na mama mwenye afya.

Kwa upande wake, Dk. Mengi alisema Watanzania wana uwezo mkubwa wa kutatua matatizo ya wenzao, hivyo ni vyema kila mwenye uwezo kuelekeza nguvu zake kuwasaidia wasio na uwezo hasa wa kupata matibabu.

“Tuna uwezo mkubwa sana wa kusaidiana, na kama kuna baraka ulizopata wewe unatakiwa uwapelekee na wenzako, na Mtanzania si mnyonge na akiwa mnyonge atakuwa amejitakia, hivyo tunastahili maendeleo na kusaidiana,” alisema Mengi.

Pia aliahidi kusaidia ujenzi wa wodi ya akina mama pindi taasisi ya THPI itakapoanza kujenga.
Naye Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Telesphory Kyaruzi, alisema kuwa taarifa ya jarida la Umoja wa Mataifa, Global Health and Deplomacy inaonyesha kuwa kina mama wajawazito 368,000, hufariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito duniani.

“Vifo vya mama wajawazito nchini kwa mwaka 2005 vilikuwa 578, kwa vizazi hai 100,000, na kufikia 454 kwa vizazi hai 100,000. Kwa mwaka 2012 vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vilikuwa 122 kwa watoto hai 1,000, mwaka 2004 mpaka 81 kwa watoto hai 1,000 mwaka 2012,” alisema Dk. Kyaruzi.

Aliongeza kuwa vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja vilikuwa 68 kwa watoto hai 1,000 kwa mwaka 2004 hadi 51 kwa watoto hai 1,000 kwa mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment