TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday, 5 December 2013

Pinda: Mshahara wangu mil. 6/- tu

  http://freemedia.co.tz/daima/wp-content/uploads/2013/12/pinda.jpg
 Na Gazeti la Tanzania Daima
MBUNGE Mohamed Habib Mnyaa (CUF) amembana Waziri Mkuu Mizengo Pinda na kumtaka alieleze Bunge lini litakaa kupitisha viwango vya mishahara ya viongozi pamoja na marupurupu yao kama Katiba ya nchi inavyotaka. 

Mnyaa alimbana Waziri Mkuu jana alipokuwa akiuliza swali kwa Waziri Mkuu katika kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu Bungeni.


Mbunge huyo wa CUF, alisema kwa kuwa suala la viwango vya mishahara kwa viongozi ni la Kikatiba ni bora sasa suala hilo likaletwa bungeni.

“Kwa kuwa suala hili ni la Kikatiba, naomba nisome Katiba Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuna jambo ambalo limeleta mkanganyiko na kwa kuwa jambo hilo ni la Kikatiba lakini kwa kuwa watu wengine hawalifahamu, naomba ninukuu hili jambo halafu nikuulize swali langu.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 43 ya sheria ya 2934 (15) 49 inayozungumzia masharti ya kazi ya rais, rais atalipwa mshahara na malipo mengine na akistaafu atalipwa malipo ya uzee au kinua mgongo au posho kadri itakavyoamuliwa na Bunge.

“Sasa nataka kuuliza swali langu mimi uzoefu wangu ndani ya Bunge ni mdogo lakini nataka kukuuliza ni lini Bunge lako limekaa na kupitisha mishahara ya viongozi wakuu kama rais kwa kuwa jambo hilo ni la Kikatiba?” alihoji Mnyaa.
Akijibu swali hilo, Pinda alikiri kwamba jambo hilo lipo lakini hawezi kulijibu kwani hajawahi kuona linajadiliwa bungeni japokuwa ni suala la Kikatiba.
Alisema kuwa angekuwa amepata swali hilo mapema angeweza kulitafutia majibu mazuri ikiwa ni pamoja na kumsomea sheria pamoja na vifungu mbalimbali pamoja na kanuni ambazo zinaweza kuweka utaratibu wa kupatikana kwa fedha.

Aidha Pinda alisema kuwa katika suala la mishahara ya viongozi, menejimenti ya utumishi wa umma huweka utaratibu ambao utawawezesha kuweka vizuri malipo ya mwisho ya utumishi wa viongozi.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo pia alitaka kujua iwapo mitandao ya kijamii ndiyo inayoruhusiwa kuonyesha mshahara wa Rais na Waziri Mkuu ambapo rais analipwa sh milioni 32 na Waziri Mkuu analipwa sh milioni 26.

Mnyaa alisema kwa kuwa Bunge ndilo linalotakiwa kupanga mishahara hiyo na kwa kuwa suala hilo ni la Kikatiba na kwa kuwa Bunge halifanyi hivyo, mbunge huyo alimhoji Waziri Mkuu kwamba haoni kuwa Bunge limeporwa mamlaka ya kuidhinisha mishahara ya viongozi.

Hata hivyo kabla ya Pinda kujibu swali hilo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimpa mwongozo Waziri Mkuu kwa kumtaka ajibu uongo wa magazeti jambo ambalo lilizua kicheko ndani ya ukumbi wa Bunge.
Akijibu swali hilo, Pinda alisema amekuwa akisikia kuwa analipwa fedha nyingi lakini halikuwa likimpa taabu.

“Mheshimiwa Spika, hata mimi nilikuwa nikisikia lakini haikunipa taabu hata kidogo lakini niliposikia ndugu yangu mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe akiwa Mpanda akisema kuwa Waziri Mkuu anapokea mshahara wa sh milioni 26 wakati Rais anapokea sh milioni 30, ilinishtua kidogo.
“Huku akisema kuwa Pinda anawadanganya kwa kujiita Mtoto wa Mkulima: ‘huyu ni mtoto wa mkulima gani anapata fedha nyingi hivyo?’
“Lakini kusema ukweli mimi nijisemee mshahara wangu ni sh milioni 6 ikiwa ni pamoja na posho za mke wangu.

“Sitaki kumsemea Bwana Mkubwa kwa hiyo anayesema kuwa mimi napata mshahara wa sh milioni 26, siyo sahihi hata kidogo unapoona mtu anakuja na kusema mtu anapokea mshahara wa sh milioni 30 unaweza kuona kuwa ni njama au kutaka kumchafua mtu maana alisema kuwa huyu mtu anajiita Mtoto wa Mkulima wakati anapata mshara mkutwa tu lakini mimi nasema huyu baba huyu namwombea Mungu amsamehe na kumuepusha na balaa linaloweza kumkuta kutokana na kusema uongo,” alisema Pinda.

Pinda alisema ameona vyema alizungumzie hilo yeye bila kumsemea Rais wala makamu na kuongeza kuwa hata hivyo fedha ambayo analipwa Makamu na Rais wala haitofautiani na yeye.

“Tofauti kati ya mshahara wangu pamoja na wa Makamu na Rais hautofautiani hata kwa shilingi milioni moja kwa hiyo fikiria Bwana Mkubwa anapata kiasi gani pamoja na Makamu wa Rais anapata kiasi gani.

“Mimi ninachoweza kusema ni kuwa ni jinsi gani mfumo wa nchi yetu ulivyo mzuri kuliko nchi nyingine; ninawashukuru wale waliofikiria kuwa watumishi wa juu watakaa katika nyumba za bure na watapata chakula bure.

“Mnapata chakula ambacho kimsingi hamlipii gharama yoyote na hilo lilifanyika makusudi kwa ajili ya kuwafanya viongozi hao kutokutumia muda wao mwingi kwa ajili ya kufikiria, kwa hili tunashukuru sana Watanzania walifikiria jambo hilo na mambo mengine na pesa za posho za wabunge, nalipwa sawa na wabunge wengine,” alisema Pinda.

Hata hivyo Pinda alisema kuwa kati ya watu ambao ni mabingwa wa kukopa, yeye anaongoza kukopa kutokana na fursa aliyonayo kwa mujibu wa utaratibu ambao upo.

“Nimekopa NNB nilipoona nimezidiwa na juzi mliporuhusu kukopa kiinua mgongo mimi nilichukua asilimia 50 ya kwangu lakini hayo yote ni kutokana na utaratibu mliouweka ninyi ili tuweze kuishi katika utaratibu na mfumo ambao mimi naamini kuwa ni mzuri sana. Kwa kifupi mimi naweza kusema hivyo tu,” alisema Pinda.


No comments:

Post a Comment