TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 16 December 2013

Rais Kikwete Afrika Kusini



THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


Coat of Arms
PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Baba wa Demokrasia ya Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela alikuwa pia kiongozi wa Tanzania, shujaa wa Watanzania na Baba wa wananchi wa Tanzania kama alivyokuwa kwa wananchi wa Afrika Kusini.


Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania na Afrika Kusini zina uhusiano wa kindugu na wa karibu sana kwa sababu ya kazi kubwa iliyofanywa na waanzilishi wa mataifa hayo mawili, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na Mzee Mandela.

Rais Kikwete pia ameelezea historia ya shughuli za ukombozi za Mzee Mandela na jinsi alivyofika Tanganyika mwanzoni mwa miaka ya 1960, safari ambayo ilifungua msingi mkuu wa mahusiano kati ya vyama vya siasa za Tanganyika African National Union (TANU) na African National Union (ANC) cha Afrika Kusini.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza katika mazishi ya Mzee Mandela yaliyofanyika leo, Jumapili, Desemba 15, 2013 kwenye kijiji cha kwao cha Qunu kilichopo kilomita 23 kutoka mji Mkuu wa Jimbo la Eastern Cape wa Mtata.

Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi wachache walioombwa kuhudhuria hatua hiyo ya Mzee Mandela ambaye alifariki dunia siku 15 zilizopita nyumbani kwake mjini Johannesburg, akiwa na umri wa miaka 95.

Katika hotuba yake yenye nguvu na iliyotoa somo la historia, Rais Kikwete ameelezea jinsi Mzee Mandela alivyowasili mjini Dar Es Salaam Januari mwaka 1962 akitokea mjini Mbeya baada ya kuwa amesafiri bila hati yoyote ya kusafiria kutoka Afrika Kusini kupitia Bechuanaland (Botswana) na Rhodesia Kaskazini (Zambia).

Rais Kikwete amesema kuwa safari hiyo ililenga kumshawishi Mwalimu Nyerere kuunga mkono uamuzi wa ANC kubadilisha mwenendo wa mapambano dhidi ya siasa za ubaguzi wa rangi kwa kutumia silaha badala ya kuwania haki za Waafrika kwa njia za amani kwa sababu ilikuwa dhahiri kuwa njia hizo zisingeleta matunda yaliyokusudiwa.

Rais Kikwete amesema kuwa safari hiyo iliyomwezesha Mandela kupata hati ya kusafiria ya Tanganyika ambayo ilimpeleka Ghana, Nigeria, Ethiopia na Algeria, ndiyo ilifungua njia ya mabadiliko ya kidemokrasia yaliyokuja kutokea katika Afrika Kusini mwaka 1994, kuleta uhusiano wa karibu sana kati ya nchi hizo na kumfanya Mandela kiongozi wa Watanzania kama alivyokuwa kiongozi wa Afrika Kusini.

Wageni waalikwa wameanza kuwasili nyumbani kwa Mzee Mandela kiasi cha saa 10 usiku na shughuli zenyewe za Mazishi ya Kitaifa ya Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini zimeanza saa 12 asubuhi ndani ya nyumba ya Mzee Mandela kwa wanafamilia kuaga mwili wa marehemu kwa mara ya mwisho.

Baada ya kuaga mwili, wanafamilia wameshiriki ibada fupi na kuandaa jeneza kabla ya kuanza kwa maandamano ya kupeleka mwili wa marehemu kwenye Hema Maalum kwa ajili ya hatua ya pili ya shughuli za mazishi, hatua iliyohudhuriwa na wageni maalum waalikwa.

Mwili wa Mzee Mandela ulifikishwa kwenye Hema Maalum kiasi cha saa mbili na dakika 13 asubuhi kwa ajili ya Sherehe ya Kwanza ya Mazishi ya Kitaifa katika historia ya Afrika Kusini na kuwekwa chini ya jukwaa kuu ambalo lilipambwa na mishumaa 95 iliashiria umri wa Mzee Mandela wakati anaaga dunia wiki mbili zilizopita Desemba 15 nyumbani kwake mjini Johannesburg.

Mazishi ya leo ambayo yameendeshwa kwa mchanganyiko wa mila na desturi za Kabila la Xhosa naKanisa la Mesthodist ambalo Mzee Mandela alikuwa muumini wake yamekamilisha siku 10 za maombolezo ya kiongozi huyo, maarufu kwa jina la Baba wa Demokrasia ya Afrika Kusini.





Miongoni mwa watu ambao wamezungumza kwenye shughuli hiyo na kuvutia sana watu alikuwa ni Mzee Kenneth Kaunda, Rais wa zamani wa Zambia na Mzee Ahmad Kathrada, mwanasiasa ambaye alifungwa kwenye jela ya Robben pamoja na Mzee Mandela.

Mzee Kathrada ambaye anasema kuwa alikutana na Mzee Mandela miaka 67 iliyopita, alifungwa Robben kwa miaka 26 wakati Mzee Mandela alikaa miaka 27.

“Alipofariki Walter Sisulu nilikuwa nimepoteza baba yangu, sasa kwa kumpoteza Nelson Mandela nimempoteza kaka yangu. Sina mwingine aliyebakia wa kumkimbilia,” alisema Mzee Kathrada katika kauli iliyovutia sana hisia za waombolezaji.

Miongoni mwa wageni hao maalum waalikwa walikuwa ni pamoja na Rais Kikwete na viongozi kutoka nchi mbalimbali chache wakiwemo wa Malawi, Zambia, Nigeria, Zimbabwe, Lesotho, Ethiopia na Mama Maria Nyerere.

Kwenye hatua hii ya pili, wageni maalum wamesikiliza nyimbo za kwaya na hotuba mbalimbali za viongozi wachache waliopewa heshima maalum ya kuzungumza katika shughuli hiyo akiwemo Rais Kikwete.

Wengine waliozungumza ni mwakilishi wa familia ya Mandela Chifu Ngangomhlaba Matanzima, rafiki wa karibu wa Mzee Mandela Bwana Ahmad Kathrada, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam Daselegn, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) Rais Joyce Banda wa Malawi na Rais mwenyeji Mheshimiwa Jacob Zuma.

Baada ya hatua hiyo ya pili, mwili wa Mzee Mandela umehamishiwa kwenye kaburi lake ukiwa unashuhudiwa na waombolezaji maalum ambao ni pamoja na familia yake.




Kwenye eneo hilo la kaburi, Ofisa wa Jeshi la Afrika Kusini ameondoa medali, bendera na heshima nyingine ambazo kiongozi huyo amewahi kuzipata katika maisha yake na kuzikabidhi kwa Mkuu wa Jeshi hilo ambaye naye amezikabidhi kwa Rais Zuma ambaye amezikabidhi kwa mrithi wa Mzee Mandela.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

15 Desemba, 2013

No comments:

Post a Comment