TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 16 December 2013

Serikali yaipongeza juhudi za asasi ya ukuzaji sanaa na muziki

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utamaduni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Leah Kihimbi  ameipongeza Asasi ya Ukuzaji Vipaji vya Sanaa na Muziki nchini (UCA-Tanzania) kwa kuja na wazo na kuibua wasanii chipukizi. 

Pongezi hizo alizitoa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na kusema "...Nimeambiwa kuwa asasi hii imesajiliwa kwa lengo la kuwashirikisha na kuwaunganisha vijana wenye vipaji vya sanaa na muziki pamoja na waliokwishafanikiwa katika kuwezesha kukuza vipaji walivyonavyo," alisema Bi. Kihimbi akimuwakilisha Katibu Mkuu.


"Kimsingi hili ni jambo jema la kusaidiana na serikali katika kukuza vipaji na kuongeza viwango vya sanaa, ili kuwawezesha wasanii wetu kukabiliana kikamilifu katika ushindani wa soko la kimataifa," alisema.

"...Nawashauri vijana watumie fursa kama hii kila kila zinapopatikana katika kufanikisha malengo yao kupitia fani za sanaa. Kama sote tunavyofahamu kuwa sanaa ni ajira na inanafasi kubwa ya kubadili maisha ya watu na nchi kiuchumi na kifikra ni vema watu wakaondokana na dhana potofu kuwa sanaa si kazi ya maana na ni kwa wasiohitaji kujifunza," alisisitiza.

Aidha alitoa changamoto kwa baadhi ya watu kuacha fikra finyu za kuichukulia sanaa kama si kazi kama ilivyo kazi nyingine, kwani mawazo hayo hayaitendei haki pamoja na kuzingatia umuhimi wa sanaa kwa jamii.
 
 "...Ninapata furaha kubwa kusikia kuwa tamasha hili litakuwa likifanyika kila mwaka. Ninakupongezeni sana kwa kubeba sura ya uzalendo unaolenga kuikuza, kuiendeleza na kuipa hadhi fani ya sanaa na muziki," aliongeza.

"...Ninatambua kuwa kazi hii kubwa na nzuri mnayoifanya ni utakelezaji wa sera ya utamaduni inayosisitiza na kusimamia maadili ya Mtanzania pamoja na kuzingatia mafunzo na elimu katika fani zetu. Tunafahamu kuwa utamaduni ni mali ya jamii, hivyo ni jukumu la wananchi wenyewe kuupenda, kuuthamini na kuuendeleza utamaduni wetu kwa kutumia kazi za sanaa."

Awali akizungumza kabla ya uzinduzi wa tamasha hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa UCA-Tz, Emmanuel Mushy aliishukuru Serikali kwa ushirikiano iliouonesha kufanikisha tamasha hilo na kutoa shukrani kwa makampuni ya Zantel, Coca Cola- Tanzania, Maezeki, LBGY Media na mtandao wa Thehabari.com kushiriki kuwasaidia vijana wasiosikika kusikika.

Zaidi ya wasanii 25 chipukizi walipata nafasi kwenye tamasha hilo ya kuonesha uwezo wao kwa jamii wakiwemo baadhi ya wasanii chipukizi wanaoanza kunufaika na kazi zao kama Menina, M Rap na Ally Nipishe.

No comments:

Post a Comment