![]() |
Maria Tarafa akiwa na watoto wake |
MAHAKAMA ya mwanzo Mjini Namanyere, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa
imetoa amri ya kumtaka Ndebile Kazuri kujenga nyumba ya aliyekuwa mke wake
Maria Tarafa iliyopo kijijini Isale ambayo aliibomoa akishinikiza mtalaka wake
aondoke eneo ambalo alikuwa akikaa kabla ya kutengana.
Mwishoni mwa mwaka jana (2013)
Mahakama hiyo ilivunja ndoa ya wanandoa hao wenye watoto wanne baada ya Kazuri
kuwasilisha kesi mahakamani akitaka ndoa yake na mkewe ivunjwe. Hata hivyo
baada ya kuvunjwa kwa ndoa hiyo mke amewasilisha kesi mahakamani hapo akitaka
mali za ndoa hiyo zigawanywe na mume awajibike kuwatunza watoto wake, jambo
ambalo halikuzungumziwa kwenye kesi ya awali.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi juzi, Bi. Tarafa alisema Mahakama ya mwazo imetoa amri ya kumtaka mtalaka
wake kujenga nyumba aliyomvunjia yeye na watoto wake wanne akishinikiza aondoke
nyumbani hapo, bila kupewa haki ya mgao wa mali zilizochumwa wakati wa ndoa.
“…Juzi tumetoka Mahakamani
nilikwenda kufungua kesi nikiiomba mahakama igawe mali ambazo tulichuma na mume
wangu muda wote wa ndoa yetu lakini mume wangu hataki zigawanywe, ila mahakama
imemuamuru kwanza ajenge nyumba ambayo amenivunjia pale nyumbani nikiwa na
watoto akitaka niondoke nyumbani, ameambiwa awe ameimaliza kabla ya Februari
14,” alisema Bi. Tarafa akizungumza kwa njia ya simu.
Alisema Kazuri alivunja nyumba
ambayo mkewe alikuwa akiishi na watoto wake wanne siku chache baada ya mahakama
ya mwanzo wilayani Nkasi kuvunja ndoa yao, jambo ambalo Bi. Tarafa
hakukubaliana nalo kwani alitegemea watagawana mali ya ndoa yao na yeye kupata
nyumba ya kuishi.
“…Katika muda wote wa ndoa yetu
tumefanikiwa kupata mali kama nyumba tatu ambazo zote zipo eneo moja la kijiji
cha Isale, ng’ombe zaidi ya 127, mbuzi 30 pamoja na mashamba zaidi ya hekari 70
mali ambazo hazikuzungumziwa kabisa na mahakama, lakini baada ya ndoa kuvunjwa
nashangaa mwenzangu ananibomolea hata nyumba ambayo nilikuwa naishi mimi na
wanangu…sasa naomba kila mmoja agawiwe haki yake,” alisema Bi. Tarafa.
Kazuri alifungua kesi katika
Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi Oktoba 28, 2013, kesi namba
26/2013 iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa kwa jina la B. Stanley; na Novemba
18, 2013 hakimu huyo baada ya kuisikiliza kesi aliamuru ndoa ivunjwe.
Mahakama ilivunja ndoa hiyo na
kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili kati ya wanne waliozaa na mumewe
kipindi wakiishi kama mke na mume bila kueleza namna watoto hao watakavyo pata
huduma toka kwa baba yao.
Mahakama pia iliamuru watoto wa
miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na wenye miaka chini ya saba kubaki na mama
yao. Mahakama hiyo ya mwanzo pia iliamuru mke apewe magunia 9 ya mahindi kati
ya 10 ambayo walizalisha wote na bati 7 zilizokuwa nyumbani.
Kwa upande wake
Kazuri akizungumzia juu ya mali ambazo mkewe anazilalamikia, alisema mali hizo
alipewa na babayake wakati anaanza maisha hivyo bado ni mali ya babayake mzazi
ambaye alidai yupo hai hadi sasa. Hata hivyo tarifa zaidi zinasema baba yake na
Kazuri (Kazuri Moshi) alifariki mwezi Machi 2004 na mali zake kurithishwa kwa
watoto wake akiwemo Kazuri.
Katika mgao huo
mtalaka wa Kazuri alisema walipewa jumla ya ng’ombe 65 lakini wamezizalisha
hadi kufikia idadi kubwa hivi sasa, ambapo ni zaidi ya ng’ombe 127 pamoja na
mashamba.
*Imeandaliwa na
www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA
No comments:
Post a Comment