TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Sunday 1 June 2014

STARS RAHA TUPU HARARE, WAINYAMAZISHA ZIMBABWE KWAO NA KUSONGA MBELE AFCON

Na Mahmoud Zubeiry, HARARE
TANZANIA imesonga mbele katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco, baada ya sare ya 2-2 na Zimbabwe jioni hii Uwanja wa Taifa, Harare. 

Kwa matokeo hayo, Stars imefuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2, baada ya ushindi wa awali wa 1-0 wiki iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao pekee la John Bocco na sasa itamenyana na Msumbiji.
Mfungaji wa bao la kwanza la Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' akishangilia leo Harare

Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, wenyeji Zimbabwe wakitangulia na Tanzania wakasawazisha.

Danny Phiri aliwainua mapema tu dakika ya tatu mashabiki wa nyumbani kwa bao zuri baada ya shambulizi la kushitukiza lililozua kizazaa langoni mwa Stars.

Zimbabwe waliuteka Uwanja kwa soka maridadi wakishangiliwa na mashabiki wao waliojitokeza kwa wingi kwa kiingilio cha dola 1 ya Kimarekani, sawa na Sh. 1,600 za Tanzania, lakini uimara wa safu ya ulinzi ya Stars uliwazuia wenyeji kupata bao lingine.

Stars ilizinduka dakika 10 baadaye na kuanza kucheza kwa utulivu ikifanya mashambulizi ya kushitukiza na muda mwingi kuweka ukuta kwenye eneo lao.
Hali hiyo ilizaa matunda dakika ya 21 baada ya shambulizi la kushitukiza na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akamalizia vizuri kona ya Simon Msuva.
Zimbabwe walipoteana baada ya bao hilo kwa takriban dakika tano, kabla ya kuzinduka baadaye na kuanza tena kushambulia, ingawa waliishia kukosakosa mabao ya wazi.

Sifa zimuendee kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyeokoa michomo mingi ya hatari, wakati mwingine akilazimika kuwavaa wachezaji wa Zimbabee kugombea mipira hadi kuumia mara kadhaa.

Kipindi cha pili, Stars iliingia na moto mkali na kufanikiwa kupata bao la pili mapema tu dakika ya kwanza, mfungaji Thomas Ulimwengu aliyetumia uzembe wa mabeki wa ZImbabwe.

Baada ya bao hilo, Zimbabwe wakapoteza mwelekeo uwanjani na Tanzania wakaanza kucheza kwa kujiamini bila woga.

Hata hivyo, Zimbabwe walifanya shambulizi la kushitukiza na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 54, mfungaji Denver Mukamba aliyepiga kona iliyoingia moja kwa moja.   

Baada ya bao hilo, Stars wakaamua kucheza kwa kujihami moja kwa moja ili kuepuka kutoruhusu mabao zaidi.

Zimbabwe ilifanya mashambulizi mengi langoni mwa Stars waliokuwa wakicheza kwenye eneo lao, lakini bahati haikuwa yao.

Kocha Mart Nooij alifanya mabadiliko kipindi cha pili akiwaingiza Mrisho Ngassa, Frank Domayo na Said Mourad kuchukua nafasi za Simon Msuva, Amri Kiemba na Thomas Ulimwengu.

Mashabiki wa Zimbabwe waliwazomea wachezaji wao baada ya mechi na kuwashangilia wachezaji wa Stars.

Kocha Nooij aliwapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri na akasema sasa anaanza kujipanga kwa mchezo ufuatao, lengo likiwa ni kuhakikisha kwanza anaipeleka Stars kwenye makundi.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliyeongoza mwenyewe msafara wa Stars hapa, alikuwa mwenye furaha baada ya mechi akisema sasa wanaelekeza nguvu zao katika hatua inayofuata.

Kikosi cha Zimbabwe kilikuwa; George Chigova, Partson Jaure, Danny Phiri/Pasca Muhanga dk72, Hardlife Zvirekwi,  Edward Sadomba, Ovidy Kaburu, Denver Mukamba/Kudakwahe Musharu dk56, Eric Chipeta, Willard Katsande, Cuthbert Malajila/Tendai Ndoro dk46 na Milton Ncube.

Tanzania; Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mwinyi Kazimoto, Simon Msuva/Said Mourad dk78, Amri Kiemba/Frank Domayo dk62, John Bocco, Thomas Ulimwengu/Mrisho Ngassa dk88 na Erasto Nyoni.
 
Chanzo.Binzubeiry blog

No comments:

Post a Comment