TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Saturday 26 September 2015

BASATA kurudisha hadhi ya muziki wa Reggae

Katibu Mkuu wa BASATA Geofrey Mwingereza
 Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Kampuni ya Reggae Production House iliyo chini ya Msanii Mkongwe wa reggae Innocent Nganyagwa limeandaa programu maalum kwa ajili ya kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini.

Programu hiyo ambayo itafanyika makao makuu ya BASATA yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam Jumatatu ya Tarehe 28/09/2015 kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:30 

Mchana kupitia Programu ya Jukwaa la Sanaa, itakuwa mahsusi kwa ajili ya kuurudisha muziki wa reggae jukwaani, kujadili mwelekeo wa muziki huu na kuja na mikakati bora ya kuurudishia hadhi yake. 

Ieleweke kwamba katika siku za karibuni muziki huu wa reggae umekuwa umeganda na kutokupiga hatua kubwa hali ambayo imewafanya wadau wa muziki kukosa burudani ambayo wamekuwa wakiipata huko nyuma kupitia kwa wasanii wakongwe kama Innocent Nganyagwa, Innocent Garinoma, Justine Kalikawe na wengineo. 

Changamoto kubwa si tu ni muziki huu kutochezwa kwenye vyombo vya habari bali pia kuna changamoto ya wasanii wenyewe kutokubadilika na kutengeneza muziki unaokwenda sambamba na soko pia hitaji la mashabiki. 

Ni nia ya BASATA kuona wasanii na wadau wote wa muziki nchini wanahudhuria programu hii mahsusi kwa lengo la kujadiliana kwa pamoja hatma ya muziki wa reggae, kupata historia ya jinsi ulivyokuwa huko nyuma, kutazama na kuburudika Jukwaani na muziki wa mmoja wa wasanii wakongwe wa muziki huu.

BASATA linaamini kwamba baada ya programu hii wasanii wa reggae na wadau kwa ujumla watakuwa na mwanzo mpya katika kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini na kuhakikisha unaendelea kudumu.

Sanaa ni Kazi, tuikuze, tuitunze na kuithamini

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI BASATA

No comments:

Post a Comment