![]() | ||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
Mmiliki wa Bendi ya Twanga Pepeta Asha Baraka akiwa katika pozi na tuzo aliyowahi kuipata miaka ya hivi karibuni |
Baada ya
Bendi ya African Stars kunyakuliwa dansa na mwimbaji wake kwenda katika bendi ya
mashujaa hatimaye sasa imeamua kuja kivingine kwa kuhakikisha kwamba inakuwa na
bendi nyingine yenye vipaji lukuki.
Mchakato wa
kuanzisha bendi ya academy ulianza rasmi mapema mwaka huu ambapo kuna vijana
wengi walijitokeza kuchukua fomu ili kuonyesha vipaji walivyonavyo.
Waliojitokeza
kusaka nafasi ni wengi sana lakini zaidi
vijana 50 ndio waliopatikana na tayari wameanza kujifua na mazoezi ya kuimba,
kupiga muziki na kucheza. Hiyo yote ni katika kuhakikisha kuwa bendi hiyo
haiishiwi na vipaji bali kuongeza zaidi ili baadaye hata wanapoondoka
wanachukuliwa waliopo kuendeleza kurudumu.
Lengo ni
kuhakikisha African Stars Bendi inaendelea kutoa ajira kwa vijana wenye vipaji
sio tu waweze kufanya kazi katika bendi hiyo bali pia wanaweza kufanya kazi
katika bendi nyingine mbalimbali ikiwa watahitajika.
Katika
mazungumzo na gazeti hili Mkurugenzi wa bendi hiyo Asha Baraka ameliambia
gazeti hili kwamba kama ilivyo kawaida kwao wamelenga kuwasaidia vijana wenye
vipaji na wenye nia ya kuwa wanamuziki
watakaoendeleza muziki wa dansi.
Anasema vijana
hao sio tu watakuwa wanaimba bali pia wameanza kujifunza muziki kwa ujumla kwa maana
ya kuimba, kupiga gitaa na vyombo vingine pamoja na kucheza.
“Vijana hao
wanafundishwa vitu vyote na tayari wana
meneja wao ambaye anawasimamia katika kufanya mazoezi, kwa kweli karibu vijana
wote tuliowachukua wana vipaji,”anasema Asha.
Kwa vijana
ambao wataonekana kufanya vizuri wengine watafanya kazi na bendi ya Twanga
Pepeta ili kukuza zaidi vipaji. Hiyo yote ni katika kuhakikisha wanapata ajira
kama ilivyo kwa vijana wengine ambao tayari walikwisha chukuliwa siku
zilizopita na sasa wanaendelea kufanya vizuri.
Vile vile,
anasema vijana hao watakuwa wakichangamsha katika bendi hasa katika muziki wa
dansi ambao unazidi kupendwa kwa kadri miaka inavyozidi kusogea. Ni rahisi kwao
kupata kazi hata katika bendi nyingine cha msingi ni kuonyesha jitihada
kuzingatia yale wanayofundishwa.
Mama Asha
Baraka sio mara ya kwanza kufanya jambo kama hilo, kila mwaka hujitahidi kwa
nafasi yake kutafuta vipaji vipya. Mwaka jana alikuwa akitafuta madansa ambapo
ilikuwa ikifadhiliwa na manywele na hatimaye kupata mshindi ambaye alichukuliwa
na kufanya kazi na twanga pepeta.
Vile vile,
anasema siku za nyuma aliwahi kuwachukua vijana kutoka jumba la sanaa THT na
wengine walichukuliwa kutoka BSS. Wote wanafanya kazi vizuri na hadi leo
wameonekana kung’ara katika anga ya muziki wa dansi.
Katika mitaa
mbalimbali tunayoishi kuna vipaji vingi vya kuimba, kucheza na kuchezea vyombo
bado hawajulikani. Walikuwa wanatafuta nafasi kama hiyo ili waweze kuonyesha
vipaji walivyo navyo. Kwa fursa ambayo mama Asha Baraka amekuwa akiwapa vijana
ni dhahiri wengi waliosikia tayari wamejitokeza ili kukuza vipaji vyao.
Ingawa bado
kuna wengine wako mikoani na wanatamani kufikiwa na fursa hiyo ila wanashindwa
ni kwa vipi watapata ama kupewa nafasi hiyo. Kwa sasa ukichunguza kila nyumba
utaona kuna mmoja ana kipaji cha kuimba, na sio rahisi kuwatambua wote kwa mara
moja.
Jambo muhimu
ni kwamba wale waliobahatika kupata
nafasi hiyo wasiichezee kwa maana kwamba bahati haiji mara mbili, watumie
nafasi hiyo kuonyesha jitihada na bidiii ili hatimaye waweze kutimiza ndoto
zao.
Mama Baraka
anasema hata kwa wale madansa wana nafasi ya kujifunza kuimba na kupiga vyombo
ili waweze kudumu hata pale wanapokuwa ni wazee, kwa vile wakibaki katika
nafasi moja tu ya kucheza wanapokuwa ni watu wazima watashindwa kufanya kazi
hiyo.
“Ninawaambia
madansa pia kujifunza kuimba na kushika vyombo kwa manufaa ya baadaye
wanatakiwa kufikiria mbele je akizeeka ni nini atafanya ili kuendeleza kipaji
chake, wasibaki katika nafasi moja,”anasema.
Hivyo basi
madansa wafanye kazi yao kwa kufikiria maisha ya uzeeni yatakuwaje, wawe na
ujuzi mwingine ili uweze kuwasaidia baadaye kama ambavyo mama Asha anasisitiza.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment