|
Mabalozi tisa wa Umoja wa Ulaya pamoja na mwenzao
kutoka Norway walitembelea mkoa wa Mtwara ambapo walifanya mazungumzo na wadau
wa maendeleo kuhusu mambo mbali mbali yahusuyo mkoa huo pamoja na shughuli na
matarajio ya baadae katika sekta ya gesi asilia.
Ziara hiyo iliongozwa na Balozi Filiberto Ceriani Sebregondi,
ambaye ni mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania, ambaye pia alikuwa
mwenyekiti wa kundi hilo. Ilijumuisha wanadiplomasia kutoka katika balozi
zilizopo Tanzania za nchi za Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani,
Hispania, Sweden na Uingereza. Balozi wa Norway pia alishiriki pia katika ziara
hiyo.
Wakuu hao wa balozi za nchi zao hapa Tanzania
walitembelea Bandari ya Mtwara, Kisima cha kuchunguza uwepo wa mafuta baharini,
mtambo wa kutengeneza gesi na mtambo wa kuzalisha nishati kwa kutumia gesi
uliopo jirani na bandari hiyo. Pia walifanya mikutano na maofisa wa serikali
mkoani humo akiwemo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bi. Hasna Mwilima, na wadau
wengine.
Akizungumza punde baada ya ziara hiyo, Balozi Sebregondi
aliainisha umuhimu wa ugunduzi mpya wa rasilimali asilia nchini Tanzania kwa
ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kuitaka serikali kuchukua hatua za
kukabiliana na changamoto ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na ugunduzi huo.
"Dalili njema katika sekta ya gesi ya Tanzania
zinatoa fursa ya kipekee kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ambayo yanaweza
kuleta faida kubwa kwa watu wa Tanzania," alisema huku akidokeza kuwa
uzoefu kutoka maeneo mengine duniani umeonesha kuwa hili huwa linakuja na
changamoto nyingi ambazi zinahitaji kufanyiwa kazi.
"Hii inatoa fursa kwa Umoja wa Ulaya na wabia
wengine kufanya kazi kwa njia zenye ubunifu na serikali pamoja na sekta husika
kupunguza hatari zinahusiana na maendeleo haya ili kuiwezesha Tanzania kuongeza
kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini," alisema.
No comments:
Post a Comment