Moja ya
changamoto ambazo hukumbuka vikundi vingi vya uigizaji ni kukosa ufadhili ambao ungewezesha vikundi husika kutimiza ndoto
na malengo waliyojiwekea ya kuendeleza sanaa ya uigizaji ili hatimaye kuwa
ajira rasmi kwa vijana wanaotegemea.
Wiki hii
nilifanikiwa kukutana na Kikundi kinachojulikana kama Kibaigwa Taijquan ambacho
hujihusisha na uandaaji wa filamu,
mchezo wa karate, muziki na ngumi. Ni kikundi ambacho kilianza kazi zake rasmi
miaka 9, iliyopita.
Kikundi
hicho kiko Mbagala Zakeem katika mtaa wa Kibaigwa ambapo hufanya kazi na vijana
mbalimbali wa mtaani na tayari kuna
filamu kama tatu ambazo wameshazitengeneza nyingine zikiwa tayari sokoni na
nyingine zikiwa njiani kuelekea sokoni.
Katika
mazungumzo na Mratibu wa kikundi hicho Yassin Kanyama anaeleza kuwa licha ya
jitihada za kutoa filamu tatu hadi sasa hakuna mafanikio makubwa waliyoyapata kutokana na mauzo ya filamu
hizo.
Filamu ya
kwanza waliitoa mwaka 2010 ilikuwa ikijulikana kama ‘The killing of campsite’
ambayo ilichezwa ikiwa na mtindo wa kareti. Walifanikiwa kufanya kazi na Zena
Video na fedha walizopata zilikuwa ni kiasi hivyo waliweka katika mfuko wa kuendeleza
kikundi.
Filamu ya
pili waliitoa mwaka 2011 ilikuwa ikijulikana kama kahaba wa mapenzi ambapo pia
mtindo waliotumia ni ule wa kareti, wakati filamu yao ya tatu inaitwa Jitu na
ilifanikiwa kufanya vizuri na
kuwatangaza kwa kiasi kikubwa ambapo ilisambazwa na kampuni ya Splash iliyoko
chini ya Step na nyingine ambayo iko jikoni inapikwa inaitwa bakora ambapo
watamalizia mkataba wao na Splash.
Anasema kwa
jinsi ambavyo wanatoa filamu moja ndipo wanapojifunza mambo mengi kwani kila
moja hujifunza kulingana na makosa wanayofanya hivyo pia huboresha yale
mapungufu ili kutoa filamu ambazo ni nzuri zaidi ya nyingine na kuweza
kukubalika katika soko.
Baada ya
kugundua kuwa kufanya kazi na Kampuni za usambazaji kunachangia mapato kidogo
sana, mipango iliyopo wanataka kuhakikisha wanasambaza wenyewe ili hatimaye
waweze kupata faida kwa manufaa yao na kikundi kinachowategemea.
Lakini bado
wanatamani wangepata mfadhili mwenye masharti nafuu ili aweze kufanya nao kazi
kwani wanaamini wakipata mtu muelewa pengine anaweza kuwakomboa.
Sababu kubwa
ya wao kutaka kutafuta mfadhili ni kwa vile bado kipato chao ni kidogo kiasi
kwamba wangepata msaidizi ingewaletea nafuu kubwa. Hilo ndilo jambo ambalo
wanaliamini zaidi.
Kanyama
anasema katika kikundi chao walijiwekea mikakati mingi na mojawapo ni
kuhakikisha kuwa wanakuwa na eneo watakalomiliki ikiwa na maana ya kuhamishia
ofisi na studio zao ambazo watazianzisha kwa ajili ya kuendeleza vipaji vya
uigizaji na fani nyingine wanazozisimamia.
Wapo baadhi
ya vijana wako katika kikundi hicho
wameangukia katika sanaa ya muziki lakini bado hawajaweza kutoka kwa vile bado
wanakabiliwa na ugumu wa kupata fedha kwa ajili ya kurekodi. Lakini hawajakata
tamaa kwani wanaendelea kujipa moyo wakiamini ipo siku watatoka.
Changamoto
nyingine wanayokabiliwa ni jinsi ya kupata runinga ili waweze kutengeneza
tamthiliya ambazo zitakuwa zinarushwa ili kuelimisha jamii kuhusiana na maisha
ya kila siku.
Anasema
wameshazunguka sehemu mbalimbali ili kutafuta runinga lakini tatizo lililopo
wanaelezwa watafute mfadhili ili aweze kuwasaidia maigizo yao kurushwa, na
kwasababu kipato chao bado ni kidogo walijikuta wakikata tamaa ya kile
walichokuwa wanatamani.
“Hatuna mtu
wa kutusaidia ili tuweze kufanya yale tunayoyapenda kwa ajili ya kuelimisha
jamii, kilichopo tunaangalia kwa sasa tufanyeje ili kazi yetu iweze kukubalika
na kuuza wenyewe kwa manufaa yetu,” anasema Manyama.
Hata hivyo,
makundi mengi yamekuwa yakianzishwa yakiwa na malengo ya kujikomboa wengi
huishia njiani namna hii kwasababu ya kipato. Lakini kwa upande wa kundi hilo
linajivunia wachezaji wake kuwa ni wavumilivu licha ya kutonufaika ipasavyo.
No comments:
Post a Comment