TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday 17 May 2012

Dito apanga kufungua tovuti yake

Msanii wa Bongo Fleva Dito amesema ana mpango wa kufungua tovuti yake ambayo ataweka mambo yake yote huko na itakuwa rahisi kwa mashabiki wake ambao wanataka kufuatilia kwa karibu yale ninayofanya kuyapata kiurahisi.


Dito anasema tovuti atakayofungua ataweka muziki wake kwa maana na video na audio, historia ya maisha yake, shughuli zake ambazo anazifanya na mambo yote yanayomuhusu. Hivyo, itakuwa ni nafasi nzuri kwa mashabiki wake kutembelea tovuti yake mara atakapoifungua siku za karibuni.


Anasema kuwa “Nitakapoifungua ni wazi kwamba nitaitangaza kwa mashabiki wangu wasiwe na wasiwasi, pia sio tu kwa watanzania watakaonufaika bali pia hata kwa marafiki wengine nje ya nchi itawarahisishia kuzifahamu kazi zangu kiurahisi,”.


Dito anasema anataka kubadilika kuendana na wakati hasa ikizingatia kwamba dunia ya leo imebadilika, pia kuna mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Kitendo cha yeye kutaka kuja kivingine ni kwa vile anataka kubadilika kwa kadri dunia inavyobadilika ili kuendana na wakati.


Pamoja na hayo, Msanii huyo anajivunia mafanikio mbalimbali aliyopata kimuziki ingawa anasema sio kwa sana lakini anachokipata kutokana na muziki kinamwezesha kusonga mbele kimaisha.


Anasema sio sawa na kukaa bure kwasababu muziki unamlipa kwa kiasi. Wasanii wengi hutoa wimbo mmoja mmoja ili wapate shoo kwasababu wanaamini ndio inayolipa zaidi kuliko albam. 


Dito anasema kama Rais angempa nafasi ya kuzungumza kero yake ambayo angeizungumza ni wizi wa kazi za wasanii. Sio kwamba msanii huyu ni kwanza kuzungumzia tatizo hili bali karibu wasanii wote wamekumbwa na tatizo hilo nab ado wanalia kubiwa.


Anasema kuna haja kubwa ikatolewa elimu kwa wasanii na jamii kwa ujumla kuhusiana na tatizo hili. Wasanii wengi hawanufaiki ipasavyo kwasababu ya kazi zao nyingi kuibwa.


Dito anaamini elimu pekee inaweza ikaleta mabadiliko makubwa kwa jamii. Anasema inahitaji kuelimishwa ili isiendelee na tatizo hilo la kuiba kazi zao. 


Pamoja na hayo, Msanii huyo kwa sasa ameachia kibao kingine kikali kinachoitwa ‘niamini’ ila bado hajakiachia mtaani kwani anaendelea kukitengeneza na siku ikifika wakati wowote kitasikika.


Hivyo, anawaeleza mashabiki wake kuwa mwaka huu wataona mambo mengi mapya ikiwa ni pamoja na kuwaletea nyimbo kali kama ilivyo kawaida yake. 



Mwaka  2007 Dito alivuma katika singo ya Ulibisha Hodi na kutoka tena 2009 akiwa katika kundi la Lafamilia lililokuwa chini ya Chid Benz katika wimbo wa Dar es Salaam Stand Up.

Dito  tayari ana albam yake  ya kwanza yenye nyimbo 10 ambazo ni pamoja na Wapo, Kwa Pamoja, Si Ulisema, Mdomo ft Linah, Kidogo ft Mh Temba , Sikumwelewa, Kaluma ft Koba, tushukuru na nyingine.  


Kwa wale wanaofuatilia muziki wa bongo fleva kwa muda mrefu watakumbuka kuwa mwanamuziki huyo alianza  kusikika kwa mara ya kwanza aliposimama na mfalme wa Rhymes Afande Sele katika wimbo wa Darubini kali ikiwa ni miaka ya 2004. 


Wimbo huu ulivuma na kumpa umaarufu enzi hizo alikuwa akifahamika kama Dogo Dito mpaka pale alipokuja kutoa Dunia ina mambo mwaka 2005 akiwa na tena na Afande Sele. Ni mwanamuziki ambaye sio tu ni mzuri katika kutunga mashairi bali pia anajivunia kuwa na sauti nzuri inayowavutia wengi pale ambapo yuko stejini akiimba.

No comments:

Post a Comment