TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday 24 May 2012

TGNP kufanya mafunzo mikoa mitatu


           

TGNP  kufanya mafunzo ya uraghibishi mikoa mitatu
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) utafanya mafunzo ya uraghibishi ngazi ya jamii kwa  mikoa mitatu ya Shinyanga, Morogoro na Mbeya, ambapo  katika mikoa hiyo watajikita katika wilaya za  Mbeya vijijini, Morogoro Vijijini na  Kishapu. Mafunzo haya yataanza tarehe 22 – Mei 2011 – 2 June 2012.

Mafunzo hayo yana malengo ya kuwajengea wananchi uwezo wa kushiriki, kuchambua kwa kina fursa na changamoto zinazowakabili katika mazingira yao na kuyatafutia ufumbuzi  kwa kujenga vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Matarajio ya matokeo makubwa ya  Mafunzo ya Uraghibishi  na utafiti shirikishi wa kijamii,yatawashirikisha wanawake na wanaume   walioko pembezoni  katika kutambua fursa walizonazo katika kudai au kuingizwa kwa madai  yao katika mchakato wa Katiba mpya, kudai mabadiliko ya sera, kimfumo,  na haki ya uchumi kwa makundi yaliyoko pembezoni.

Mafunzo haya pia yatawajengea wanajamii uwezo wa kushiriki ipasavyo katika mchakato wa kutoa maoni kwa Tume ya Kuratibu Mchakato wa katiba mpya, haki ya uchumi, na maisha endelevu kwa wote.

 Baada ya mafunzo haya, wanajamii wataibua vipaumbele vya changamoto zinazowakumba na watajadili namna ya kukabiliana nazo wakiwa na viongozi wa serikali ngazi ya wilaya,kata na vijiji.

 Mwisho TGNP itaendesha warsha  kwa wanajamii namna ya kuanzisha  na kusimamia vituo vya taarifa na maarifa katika wilaya zao ikiwa ni sehemu ya kukutana na kushirikishana uzoefu na kujadili masuala  mbali mbali zinazowakabili.
 Imetolewa na

Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP

No comments:

Post a Comment