TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 14 May 2012

Wafanyakazi wa Korosho waandamana hadi Ofisi ya Bodi ya Korosho kudai mafao


Wafanyakazi wa viwanda vya kubangua korosho vya Lindi, Mtwara, Pugu na Kibaha wamevamia Ofisi za Bodi ya korosho kwa mabango na nyimbo za kudai haki zao wakitaka Bodi hiyo iwalipe mafao yao wanayodai kwa muda mrefu.

Wafanyakazi hao walikuwa wakiimba “tunataka haki zetu, tunataka haki zetu huku wengine wakizungumza kwa hasira dhidi ya madai yao wanayodai kwa miaka 20 sasa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Kamati ya wafanyakazi hao Stumai Mohamed alisema anashangazwa na kitendo cha Bodi ya Korosho kuwazungusha kwa muda mrefu kwa kutowalipa fedha za mafao wanazodai toka mwaka 1997.

Alisema wengi wa wafanyakazi hao walianza kazi mwaka 1988 hadi mwaka 1992 baadhi ya viwanda vilibinafishwa na mashine zikauzwa. Wakaanza kudai fedha zao za mafao ili ziwawezeshe kuwasomesha watoto na majukumu ya familia.

“Lakini jambo la ajabu tunashangaa toka tuanze kudai walitulipa fedha kidogo yaani laki moja na sabini tu kati ya milioni 9 tunazodai kila mmoja,”alisema.

Alisema kutokana na Bodi hiyo kuwapa usumbufu walienda mahakamani katika mahakama ya kazi kuishtaki Bodi hiyo na wakashinda kesi mwaka 1996 hivyo mahakama iliamuru walipwe haki zao.

Bi. Mohamed alisema kitu kingine cha ajabu ni kwamba bado wana barua za ajira na hadi sasa hawajapewa notsi ya kuachishwa kazi hivyo gharama zinazidi kuongezeka.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Bodi hiyo Ugumba Kilasa alidai kuwa kwa vile hawana wanachokijua kuhusu madai yao akawataka wapeleke kopi za hukumu ya kesi yao inayoonyeshwa kwamba wanahitajika kulipwa mafao yao ili yaweze kufanyiwa kazi.

Hata hivyo, pamoja na Mwanasheria huyo kujitahidi kujitetea kwa kila njia bado wafanyakazi hao walidai kuwa leo hawataondoka katika Ofisi za Bodi hiyo na kwamba watalala hapo hadi walipwe fedha zao.

No comments:

Post a Comment