TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday 10 May 2012

Wasanii changamkieni fursa hiyoooo ya Umoja wa Ulaya


Balozi wa Umoja wa Ulaya Filberto Sebregondi
 Umoja wa Ulaya umetoa Euro 2.5 sawa na shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kusaidia sekta ya utamaduni na ubunifu nchini ambapo fedha hizo zimekabidhwa kwa serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi.

Baada ya fedha hizo wadau mbalimbali wa viwanda vya ubunifu na utamaduni wameombwa kujitokeza kuchangia fursa hiyo. Watapewa fedha ikiwa tu wataweza kuandika proposal nzuri itakayowavutia waliotoa fedha hizo.

Balozi wa Umoja huo Filberto Sebregondi alisema malengo ya mradi huo ni kutangaza na kuchangia sekta ya utamaduni nchini kwa vile ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi ambazo zinaweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi.

Alisema mradi huo umelenga katika sehemu mbili ambapo ni kuhifadhi na kutangaza urithi na utamaduni na kujenga uwezo dhidi ya ubunifu na utamaduni.

“Umoja wa Ulaya umelenga kusaidia ubunifu na utamaduni hasa kutangaza na kukuza uwezo katika sekta hizo Tanzania, na kwa kusaidia sekta hii itasaidia katika harakati za kupunguza umaskini,”alisema.

Alisema mradi huo wa miaka mitatu utasaidia kutangaza na kuwezesha mazingira mazuri ya ubunifu, ushirikiano na kubadilishana uzoefu na vikundi mbalimbali katika shughuli za muziki, sanaa, ubunifu, fasheni, filamu, video, uigizaji na picha na hivyo kuwainua kimaisha na kusaidia kupunguza umaskini.

Pamoja na hayo, inakadiriwa kuwa mwaka 2010  mapato yaliyokusanywa kwenye sekta ya muziki ilikuwa shilingi bilioni 222 lakini kutokana na kutotekelezwa kwa sheria ya hati miliki ipasavyo serikali imekuwa ikipoteza mapato kiasi cha shilingi bilioni 20 kutokana na sekta hiyo.

Ofisa Muidhinishaji wa mfuko wa Maendeleo ya Ulaya  kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi Samwel Marwa  alisema hayo jana kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na  Umoja wa Ulaya kwa wadau wa viwanda vya ubunifu na utamaduni kujifunza jinsi ya kuandaa mapendekezo yao kwa ajili ya kuomba za maendeleo ya sekta hiyo.

Alisema kama sheria ya hati miliki ingekuwa inatekelezwa vizuri wadau wa muziki  na pia serikali ingenufaika kwa kiasi kikubwa  kwa kupata mapato mengi ambayo yangesaidia kukuza uchumi wa  nchi.

“Zipo fursa nzuri kupitia sekta hii tatizo ni kwamba hata watu walioajiriwa katika muziki na sanaa kwa ujumla hawajajiweka kibiashara, wanashindwa kuzilinda kazi zao hivyo zinaibwa ovyo kwa hiyo kupitia mradi wa Umoja wa Ulaya wa kukuza utamaduni na ubunifu tutarekebisha matatizo hayo,” alisema.

Alisema Umoja wa Ulaya tayari umesaini Euro 2.5 sawa na  shilingi Bilioni tano na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kusaidia sekta ya utamaduni ili kuleta ubunifu mpya utakaowasaidia wahusika katika sekta na kuleta mabadiliko yatakayosaidia pia serikali kukuza mapato yake.






No comments:

Post a Comment