Makamu wa Rais wa Mchezo wa Ngumi za Ridhaa Tanzania Michael Changarawe kulia akikabidhi kombe katika moja ya matukio ya mchezo huo. |
Makamu wa Rais wa Mchezo wa ngumi za Ridhaa Tanzania
Michael Changarawe amesema baada ya Selemani Kidunda kuchaguliwa kushiriki
mashindano ya Olympic yatakayofanyika London mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu
ni jukumu la taifa kumtengenezea mazingira mazuri ya kumjenga.
Selemani Kidunda alikuwa ni miongoni wa wachezaji
wanne wa ngumi wa Tanzania walioshiriki mashindano ya Afrika kufuzu kwenda
Olympic nchini Uingereza yaliyofanyika nchini Cansablanca April 28 hadi Mei 7
ambapo alishindwa na mpinzani wake kutoka Morocco baada ya kushika nafasi ya
tano.
Hata hivyo, Kidunda
baadaye alijadiliwa na kuchaguliwa kuwa miongoni mwa watakaoenda
kushiriki mashindano hayo ambapo kwa Afrika Mashariki ni wawili tu waliofuzu
huku mmoja akitoka nchini Kenya.
Changarawe alisema Kidunda kabla hajaenda katika
mashindano hayo ya kimataifa anatakiwa awekwe sehemu nzuri na kupewa chakula
kitakachomjenga mwili ambapo anashauri
ni vema kambi yake ikawa na watu sita.
“Ili Kidunda aweze kuandaliwa vizuri kushiriki
mashindano hayo naona kuna umuhimu katika kambi yake kuwe na Makocha wawili mmoja wa ufundi na mmoja wa
conditioning, daktari mmoja kwa ajili ya matibabu na wachezaji wengine wawili
wenye uzito kilo 75 na 69,”alisema
Changarawe.
Naye mwalimu wa Kidunda ambaye alikuwa kwenye
msafara huo Remmy Ngabo alisema kilichosababisha washindwe katika mashindano
hayo ya Afrika ni kutokuwa na mashindano
ya kimataifa ya mara kwa mara.
Alisema Kidunda ni mchezaji mzuri hivyo anahitajika
kuandaliwa mapema kwa maana ya kujengwa na kutafutiwa mazingira mazuri
yatakayomwezesha kuipeperusha bendera ya Tanzania Kimataifa.
Kwa upande wake Selemani Kidunda alisema “nashukuru
mashindano ya dunia niko peke yangu upande wa Tanzania, nilipigana sana sema tu
waarabu walikuwa wanatoa pointi kwa kupeana lakini zaidi naomba watanzania
waniunge mkono ili nijiandae vyema,”.
Awali, Kabla ya mchezaji huyo kuchaguliwa kwenda
kushiriki mashindano ya Afrika kulikuwa na kambi tatu Tanzania za kuwachagua
mabondia bora ambazo ni Jkt, Ngome na Magereza na jumla ya mabondia 52 walijitokeza na 10
walichaguliwa na baadaye kutokana na ukosefu wa fedha walichaguliwa 4 ambao
walikuwa ni Victor Njaiti, Abdallah Kassim, Selemani Kidunda na Amilian
Patrick.
No comments:
Post a Comment