TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 2 July 2012

Idara Yagawa Vitambulisho Zaidi ya 10,578

Na Mwantanga Ame

JUMLA ya Wazanzibari 10,578 wamepatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi baada ya kukamilisha masharti ya kisheria ya kuweza kupata vitambulisho hivyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, aliyasema hayo jana wakati akisoma hotuba ya bajeti ya Mapato na Matumizi ya Ofisi kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Waziri Mwinyihaji, alisema ndani ya kipindi cha mwaka huu wa fedha Wazanzibari 10.578 wamefanyiwa usajili kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Alisema katika usajili huo jumla ya vitambulisho vipya 3,923 vilitengenezwa baada viliopo kumaliza muda wake wa matumizi huku wafanyakazi wa serikali waliopatiwa huduma hiyo walifikia 10,393.

Alisema hivi sasa Idara hiyo pia imeshaandaa rasimu kwa ajili ya kuifanyia marekebisho sheria namba 7 ya 2005 ikiwa ni hatua ya kutoa vitambulisho kwa wageni wanaoishi hapa nchini.

Alisema rasimu hiyo tayari imeshapitishwa na Baraza la Mapinduzi na hivi sasa inasubiri kufikishwa katika Baraza la Wawakilishi ili kuweza kuanza kujadiliwa.

Alisema tangu mfumo huo kuanza kutumika Idara hiyo imeweza kuhakikisha inatimiza masharti ya kimataifa kwa mara ya sita mfululizo na imeweza kushinda kufikia viwango bora duniani.

Alisema kwa ujao wa fedha itaendelea kusajili Wazanzibari 10,500 wanaotimiza masharti ya usajili na kuwapatia vitambulisho pamoja kutengeza vitambulisho kwa waliomaliza muda.

Akizungumzia juu ya Idara ya Usalama Kazini (GSO), Waziri huyo alisema jumla ya wafanyakazi 554 kutoka katika taasisi mbali mbali za serikali walifanyiwa upekuzi na taasisi 12 zilikaguliwa kuangalia utunzaji wa siri za seriakali.

Akizungumzia Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa shughuli za Wazanzibari Wanaoishi Nchi Nje, alisema kimeweza kufanya ziara mbali mabali katika nchi za falme za kiarabu kwa Oman na Dubai ikiwa ni hatua kukutana na Wazanzibari ili kuwashajiisha katika kushiriki kuchangia maendeleo ya Zanzibar

Akizungumzia juu ya mradi wa mageuzi ya Serikali za Mitaa Waziri huyo alisema sera yake imekamilika baada kupitishwa kwa wadau tofauti zikiwemo taasisi binafsi ikiwa ni hatua ya kupata maoni yao.

Aidha, upande wa uratibu wa Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Waziri huyo, alisema tayari kuna mradi ambao utahusisha ujenzi wa misingi ya maji ya mvua kwa ajili ya maandalizi ya kutafuta mkandarasi ataeifanya kazi hiyo ambayo inatarajiwa kuyanufaisha maeneo ya ziwa la Sebleni, Ziwa la Mtumwajeni na Ziwa la kwa binti Amrani.

Maziwa mengine yatayofaidika na mradi huo Waziri huyo alisema ni la Mantenga, Kwamtipura, Kilima hewa karakana, Sogea, Mpendae, Jang’ombe, Uwanja wa Demokrasia na Shauri Moyo.
kwa habari zaidi swahilivilla.blogspot.com

No comments:

Post a Comment