TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 16 July 2012

Serikali Zanzibar yaweka mikakati kupambana na dawa za kulevya


Na Khadija Khamis-Maelezo Zanzibar   

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeandaa mikakati ya kudhibiti dawa za kulevya ili kuweza kupambana na uingizwaji na utumiaji wa dawa hizo nchini .

Akijibu suala la Mhe Ismail Jussa ladhu jimbo la mji mkongwe alietaka kujua hatua gani zinachukuliwa na Serikali kuweza kudhibiti madawa ya kulevya nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais ,Fatma  Abdulhabib Fereji  alisema wizara yake itahakikisha mikakati hiyo inafanyakazi ili kuona Zanzibar inakuwa salama na utumiaji wa dawa za kulevya.

Amesema janga la dawa za kulevya halina mipaka na kuathiri mustakbali wa rasilimali na nguvu kazi ya taifa, hivyo juhudi zinahitaji kuchukuliwa katika kuzuiya matumizi ili kuwaepusha vijana kutumbukia katika janga hilo.

Mh. Fatma amesema katika kipindi cha mwaka 2010 kuanzia novembar hadi disemba ni kesi 67 zilizokamatwa na januari 2011 hadi juni 2011 ni kesi 168 na kuanzia julai 2011 hadi juni 2012 ni kesi  104.

Alieleza kuwa katika harakati hizi za kupambana na udhibiti wa dawa  za kulevya na uhalifu kwa ujumla  umepungua kutokana na kuimarisha ulinzi shirikishi na taasisi za  dola  kufanya doria mitaani pamoja na kuandaliwa kikosi maalum kikosi kazi ambacho hufichua maficho ya watumiaji na wauzaji dawa za kulevya .

Fereji alivitaka vyombo vya dola vilivyopewa majukumu ya kupambana na tatizo hilo kuengeza kasi za utendaji kazi zao ili kunusuru vijana wa taifa letu ambao ni wahanga wakubwa katika janga hili

Waziri huyo alieleza kwamba kwa kutambua mchango wa taasisi zisizo za kiserikali katika suala zima la mapambano dhidi ya dawa za kulevya Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais (OMKR ) kupitia tume ya kuratibu na udhibiti wa dawa za kulevya ilizipatia jumla ya shilling million tisa na laki tisa (9,900,000/-)nyuma tisa za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya dawa ya kulevya (sober house)Unguja na Pemba ambazo zinatumika katika malipo ya kodi za nyumba chakula na vifaa vyengine vidogo vidogo vya nyumbani .

Aidha alisema kuwa Ofisi hiyo imeweza kutoa msaada wa vifaa vya Elektronik ikiwemo Televisheni na Radio kwa Sober house kwa Unguja na Pemba pia imeweza kutoa mafunzo mbali mbali juu ya uongozi ,utunzaji kumbukumbu na fedha yameweza kutolewa kwa viongozi wa makaazi hayo kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uwiano mzuri wa kuweza kukabiliana na vijana ambao wanaoishi huko ili kuweza kutoa huduma zenye kuleta ufanisi

 Waziri huyo alisema kuwa Wizara yake itaendelea kuunga mkono juhudi hizo na kutoa wito kwa taasisi nyengine mbali mbali na jamii kwa ujumla kuendeleza kutoa msukumo wa michango yao ya kuweza kuendeleza mbele harakati hizo .

Source.Full Shangwe Blog

No comments:

Post a Comment