TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Tuesday, 10 July 2012

Wananchi wa mikoa ya Kaskazini walizwa na bidhaa feki

Chama cha Wadau wa Nishati Jadidifu (TAREA) kimewatahadharisha wananchi kuwa makini dhidi ya udanganyifu unaofanywa na Kampuni Feki ya solar inayojulikana kama Solar Afrique ambayo imekuwa ikiuza bidhaa feki katika mikoa ya Kaskazini.

Tahadhari hiyo imetolewa na  Katibu Mtendaji wa TAREA Injinia Mathew Matimbwi baada kupata taarifa ya wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro, Manyara  na Arusha kulizwa hasa baada kuuziwa vifaa vinavyojulikana kama solar panel na baadaye kugundua kuwa havifanyi kazi.

Akizungumza na blogu hii jijini Dar es Salaam Matimbwi alisema alipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema ambaye alikuwa ni mwakilishi wa wananchi wa kijiji cha Magadini Simanjiro ambaye alikujana risiti mbili zenye anwani ya Kampunii hiyo akitafuta ilipo kampuni ya Solar Afrique ili waweze kurudishiwa fedha zao.

Msamaria huyo ambaye ni mwalimu wa shule ya Msingi Emmanuel Madauda alisema wananchi hao walipouziwa walielezwa wavichaji vifaa hivyo kwa masaa manane kisha wavitumie lakini walivyofanya hivyo na kuvijaribisha vikawa havifanyi kazi.

Alisema mfanyabiashara aliyewauzia alijitambulisha kwa jina moja la Bernad  ambapo alitoa namba zake za simu na akidai kampuni hiyo iko Ubungo Plaza na Mwanza lakini Mwalimu huyo alipoenda kuitafuta Ubungo Plaza akaelezwa hakuna Ofisi za kampuni hiyo katika Ofisi za Ubungo Plaza kumbe ilikuwa ni danganya toto.

“Jambo la ajabu mfanyabiashara huyo akipigiwa simu hapokei inaita tu na kukata na namba za simu za kampuni zinazoonekana kwenye risiti ambazo amekuwa akizitoa pia hazipokelewi,” alisema Injinia Matimbwi.

Hata hivyo, baada ya Mwalimu huyo kufuatilia pale Ubungo Plaza alielezwa hakuna Kampuni kama hiyo na hivyo kupewa orodha na kampuni zilizoko pale na ndipo kuelekezwa akaulizie TAREA ili wamsaidie.

Mwalimu huyo alibeba risiti mbili zenye majina ya wananchi waliouziwa vifaa hivyo feki  kama ushahidi ili aje kuulizia kwenye kampunii hiyo ikiwezekana warudishe fedha zao.

Kwa mujibu wa Mwalimu Madauda alisema  Bernad ambaye ndiye mfanyabiashara huhisiwa kwamba ni raia wa Kenya kutokana na lafudhi ambayo alikuwa akiongea ila amekuwa akiuza bidhaa hizo nchini kwa madai kuwa ni za hapa nchini wakati hiyo Kampuni haipo.

Matimbwe alisema mbaya zaidi vifaa hivyo wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa wakiuziwa kwa bei ya shilingi 40,000 wakielezwa ni bei ya promosheni lakini ukweli haviuzwi kwa bei hiyo wala haviuzwi kimoja kimoja kama ambavyo wananchi wameuziwa.

Alisema kutokana na tukio hilo wananchi wanatakiwa kujifunza kutokana na makosa na kwamba watazungumza na tume ya ushindani ili kushughulia tatizo hilo ili ikiwezekana wahusika wachukuliwe hatua kwa kuuza bidhaa feki.

No comments:

Post a Comment