Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limeeleza kusikitishwa na hali iliyopo sasa ya wasanii kuzipa kisogo Sanaa
zingine na kung’ang’ania filamu na muziki pekee hali inayowafanya wengi wao
kubaki wakihangaika na kulalama.
Akizungumza wiki hii kwenye programu
ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika makao makuu ya Basata, Katibu Mtendaji wa
BASATA Ghonche Materego alisema kuwa, ni jambo la kushangaza kuona wasanii
wakifunga milango yote katika sekta ya Sanaa na kubaki wakihangaika na
madirisha mawili tu ya filamu na muziki.
“Ndugu zangu hebu tujiulize tu,
Sanaa ni pana sana na ina fursa nyingi katika kutupa ajira na kuzalisha kipato
kwa vijana wengi lakini kwa nini wote tunang’ang’ana na filamu na muziki pekee?
Fursa nyingine tunamwachia nani? Alihoji Materego.
Alisema kuwa, tatizo lililopo
sasa ni kwa vijana kusukumwa na fedha tu badala ya msukumo wa kisanaa hali
ambayo imezifanya Sanaa zingine hususan za maonesho na ufundi kupigwa kumbo
kutokana na matunda yake kuhitaji muda mrefu na juhudi.
Kwa mujibu wa Materego, ni wakati
sasa wa Wasanii kufungua fursa walizozifunga katika fani nyingine za Sanaa
vinginevyo haitawezekana kwa wasanii wote kutegemea milango ya filamu na muziki
pekee katika kujiajiri bali fikra tofauti zinahitajika
“Haiwezekani tutegemee filamu na
muziki pekee, hatutafika. Ni lazima tugeukie fursa zingine katika Sanaa. Sekta
yetu ni pana na ina fursa nyingi sana ambazo zimekaa tu zinatusubili. Sisi
ndiyo tutazifanya zipendwe na zituingizie kipato” alisisitiza Materego.
Kuhusu wasanii kujitokeza katika
masuala mbalimbali yanayowahusu, Materego alisema, kumekuwa na tatizo ambapo
katika makongamano, semina na mikutano mbalimbali wasanii wanayoitwa wamekuwa
wakijitokeza kwa uchache au kutokuonekana kabisa.
“Mambo mengi yanajitokeza kuhusu
wasanii na sekta ya Sanaa kwa ujumla, wasanii wetu wamekuwa wazito sana
kushiriki. Hili nalo ni tatizo ni lazima tubadilike tujitokeze katika mambo
yote yanayotuhusu” alieleza Materego.
Awali akiwasilisha mada kuhusu
Tasnia ya Ubunifu na Mchango wake katika Ajira nchini, Mkurugenzi wa Idara ya
Mfuko na Uwezeshaji kutoka BASATA, Charles Ruyembe alisema kuwa, muda umefika
sasa wa somo la Sanaa kuanza kufundishwa mashuleni na kutahiniwa kama masomo
mengine kwani kwa sasa ni fani inayoajiri vijana wengi.
No comments:
Post a Comment