TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 27 August 2012

Na Gazeti la Tz Daima: CHADEMA wambana Nape

• Mwenyewe apanga kujibu mapigo yao leo

Na Shehe Semtawa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimempa siku saba Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuomba radhi na kulipa fidia ya sh bilioni tatu kufuatia madai yake ya uzushi na uongo kuwa CHADEMA kimekuwa kikipokea mabilioni ya shilingi kutoka nje.

Msimamo wa CHADEMA ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, akisema kuwa wameanza kuchukua hatua za kisheria kuhusu madai hayo yaliyotolewa Agosti 12, mwaka huu.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema kutokana madai hayo ya kukifedhehesha chama hicho chenye heshima na hadhi mbele ya Watanzania, Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA iliagiza wanasheria wamwandikie barua Nape ya kumtaka kuwaomba radhi kwa kutumia njia ile ile aliyotumia kufanya propaganda chafu za kukikashifu chama chao.

Alisema, kuwa Nape alilenga kuifitinisha CHADEMA kwa umma wa Watanzania akizusha kuwa upo uwezekano wa chama hicho kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani.

“Izingatiwe kuwa matamshi yake yalitangazwa na vyombo vya habari vya kielekroniki, ikiwemo vituo vya televisheni, redio na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii Agosti 12, mwaka huu na katika kurasa za mbele za magazeti mbalimbali Agosti 13, mwaka huu,” alisema.

Mnyika aliongeza kuwa, tayari chama chake kimemwandikia Nape barua ya kisheria Agosti 24, mwaka huu, kikimtaka aombe radhi na kulipa fidia ya sh bilioni tatu kwa matamshi hayo ya uzushi na uongo.

Kwamba matamshi hayo yana maana ya kuwapotosha yakidai kuwa CHADEMA inawalaghai wananchi, ina viongozi wasio waaminifu na kwamba iko tayari kuuza nchi kwa uroho wa madaraka.

“Kipaumbele cha CHADEMA katika suala hili, ni kuombwa radhi, hata hivyo kiwango cha fidia ya fedha kwa fedheha kilichotakiwa ni fundisho kuwa uzushi na uongo unagharimu.

“Ikumbukwe kwamba Agosti 12, mwaka huu, nilitoa kauli ya awali baada ya mkutano wa Nape na waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine, nilieleza kwamba tutatoa tamko la kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa kamili aliyoitoa,” alisema Mnyika.

Alibainisha kuwa, katika kauli hiyo alitoa wito kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kueleza Watanzania iwapo propaganda hizo chafu zina baraka zake, hivyo ukimya wake mpaka sasa kuhusu matamshi hayo, unaifanya CHADEMA kuwa na imani yenye shaka kwamba Nape hakutumwa na chama chake kutoa matamshi aliyoyatoa.

“Kutokana na ukimya wa Mwenyekiti wa CCM, tunachukua fursa hiyo kuutaarifu umma kwamba asipotekeleza matakwa hayo ndani ya siku saba kuanzia tarehe hiyo aliyopokea barua, hatua nyingine ya kumfikisha Mahakama Kuu itaanzishwa ili aweze kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema.

Alipotafutwa na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana ili kueleza kama amepokea barua hiyo ya CHADEMA, Nape alizungumza kwa kifupi akisema, “andika hayo maelezo yao mimi nitawajibu leo”.

No comments:

Post a Comment