TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Tuesday 14 August 2012

Na Gazeti la Tanzania Daima:Dk. Ulimboka asema anaujua ukweli



Na Ratifa Baranyikwa

HATIMAYE Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, ameibuka toka mafichoni na kuwaambia Watanzania kwamba anayejua mpango mzima wa kumteka, kumtesa na kumpiga ni yeye pekee.

Dk. Ulimboka ambaye juzi alikuwa mafichoni, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na gazeti hili kuhusiana na tukio zima la kutekwa, matibabu yake nchini Afrika Kusini na mambo mengine yaliyojiri wakati akiwa nje.
Huku akiwa makini kuchagua maneno, Dk. Ulimboka alisema waandishi wa habari wasiihoji familia yake wala mtu mwingine yeyote, kwani ukweli wa tukio lake anaujua yeye mwenyewe.

Dk. Ulimboka ambaye tangu arejee amekuwa akiishi kwa kujificha, amewataka Watanzania kuvuta subira kwani anajipa muda wa kueleza ukweli wa tukio la kutekwa kwake.

“Najua waandishi wa habari na Watanzania wengi wanataka kujua ukweli ambao ninao mwenyewe, lakini hakuna sababu ya kuwa na haraka, wakati ukifika nitazungumza yaliyonisibu,” alisema.

Hata hivyo, Dk. Ulimboka ambaye alikuwa kiongozi wa mgomo wa madaktari uliolitikisa taifa hivi karibuni, hivi sasa anaishi kwa hofu na kujificha huku akichagua marafiki wa kukutana na kuzungumza nao.

Kiongozi huyo, yuko makini pia katika kuzungumza na simu, na amekuwa akipokea zile za watu anaowajua tu.

Alipobanwa ili azungumze kwa ufupi juu ya wanaohusika na kutekwa kwake, Dk. Ulimboka alisisitiza kuwa hayuko tayari kueleza ukweli huo kwa sasa na kuongeza kuwa muda ukifika ataeleza kila kitu.

Polisi wapanga kumhoji

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova ametoa kauli inaonesha kwamba vyombo vya usalama vitamuhoji Dk. Ulimboka.

Kova ambaye alikuwa akizungumza na gazeti hili, lililotaka kujua msimamo wa vyombo vya usalama katika kulishughulikia suala la Ulimboka, hasa baada ya kurejea kutoka kwenye matibabu nchini Afrika Kusini, alisema kwamba taratibu za kipelelezi zitafuatwa.

Wakati Kova akizungumza hayo, chanzo kimoja cha habari toka kwa maofisa wa ngazi za juu wa polisi kilidokeza kuwa endapo Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) katika uchunguzi wake atabaini kuwa kuna shahidi muhimu anahitajika, atahojiwa.

Hata hivyo Kova alisisitiza kuwa; “watu wakipeleleza hawasemi ila tambua tu kwamba taratibu za upelelezi zitafuatwa.”

Tayari taarifa na mwenendo wa tukio zima zinaonesha pasipo shaka kuwa, Jeshi la Polisi katika taratibu zake sasa linafikiria kumuita na kumuhoji Dk. Ulimboka ili liweze kuondoa maneno ya kusikia sikia.

Kuhusu kutajwa tajwa kwa mtu anayedaiwa kuwa ni ofisa wa Usalama wa Taifa wa Ikulu, Ramadhan Ingondhur kuwa alihusika na njama za kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka, Kova aliahidi kulizungumzia hilo siku ya Ijumaa.
Mbali na gazeti la MwanaHalisi kumtaja Ramadhan kuwa ndiye mhusika mkubwa wa kutekwa kwa Dk. Ulimboka, mwingine aliyeungana na msimamo huo ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa ambaye aliitaka Idara ya Usalama wa Taifa pamoja na serikali ithibitishe hadharani juu ya mtu anayetajwa kuhusika na tukio hilo.

Dk. Slaa alisema chama chake kitaanzisha harakati za kutaka kujua ukweli wa nani anahusika kumteka Dk. Ulimboka.

Mwanzoni mwa wiki, Dk. Ulimboka alirejea kwa kishindo nchini kutoka Afrika Kusini alikokuwa anatibiwa, na kusema yupo tayari kuendeleza mapambano na kazi baada ya kupona kabisa.

Dk. Ulimboka alikwenda Afrika Kusini Juni 30 mwaka huu kwa ajili ya matibabu baada ya kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Juni 27, 2012.

Aliondoka nchini akiwa kwenye kitanda cha wagonjwa kwa vile alikuwa kwenye hali mbaya kiafya, lakini alirejea akitembea kwa miguu na kuonekana mwenye afya njema.

No comments:

Post a Comment