TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Tuesday 14 August 2012

Tanzania iahirishe kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Peter Kallaghe (wa katikati mwenye suti) akiwa na wawakilishi wa Tanzania wa Michezo ya Olimpiki ya London 2012. [Picha kwa heshima ya Kamati ya Olimpiki ya Tanzania]

Tanzania inapaswa kuchukua mapumziko ya muda na kusitisha ushiriki wake katika Michezo ya Olimpiki ili kuandaa kwa ufanisi kizazi kipya kijacho cha wanamichezo, wachambuzi wa michezo wasema.

Katika michezo ya Olimpiki ya London, iliyomalizika Jumapili (tarehe 12 Agosti), wanariadha saba wa Tanzania waliiwakilisha Tanzania, na hakuna hata mmoja aliyeshinda medali. Tanzania imeshinda medali mbili katika mashindano ya Olimpiki, zote huko Moscow mwaka 1980.
Faustine Mussa na Samson Ramadhani walishiriki katika mbio za marathoni za wanaume lakini walishindwa kupanda jukwaa la zawadi. Mussa alimaliza nafasi ya 33 alitumia muda wa saa 2, dakika 17 na sekunde 39, wakati Ramadhani alimaliza wa 66 kwa muda wa saa 2 dakika 24, sekunde 53. Mwanamarathoni wa tatu, Mohamed Ikoki Msandeki, alijitoa kwenye mashindano siku moja, kwa kusema alikuwa mgonjwa.
Mkimbiaji wa mbio za kati Zakia Mrisho alimaliza wa 16 katika mbio za mita 5,000 kwa kutumia muda wa dakika 15 na sekunde 39.58. Naye mwogeleaji Ammaar Ghadiyali alitokea wa tatu katika kundi lake na mwogeleaji Magdalena Moshi alitokea wa 7 katika kundi , lakini wote walishindwa kuendelea zaidi. Bondia Suleiman Kidunda alipoteza raundi zote tatu kwenye mashindano ya uzito wa wastani.

Matayarisho mabovu na ukosefu wa uongozi

Mwandishi wa habari za michezo Grace Hoka anasema michezo ya Tanzania inahitaji kugeuzwa kabisa kiasi kwamba serikali ingesitisha ushiriki wa kimataifa katika michezo yote kwa muda wa amiaka 10 ili kukuza michezo ipasavyo nchini na kutoa mafunzo makubwa kwa wanariadha wenye kuleta matumaini.
"Tunapaswa kuzifumua timu zote za taifa, mashirika yote ya michezo ya taifa na kila kitu kinachohusiana na michezo na kuanza kuwafunza watoto wadogo. Baada ya miaka 10, tutakuwa na timu nzuri kuliko wakati wowote," Hoka aliiambia Sabahi.
Anasema matayarisho mabovu ya wanariadha na ukosefu wa uongozi kutoka kwa mameneja katika mashirika ya michezo ndio sababu kubwa ya utendaji wa Tanzania wa kuvunja moyo katika michezo ya Olimpiki mwaka huu.
Anasema serikali ingechukua uongozi kutoka mashirika ya michezo, hata kama ni kwa muda, kama ilivyofanya kwa timu ya taifa ya mpira tangu mwaka 2007.
Zaidi ya hayo, alisema hata kama itakuwa ghali zaidi, wakimbiaji wa marathoni wanapaswa kufanya mazoezi huko Arusha au Mbeya, ambako kuna mwinuko wa juu kuliko ilivyo Dar es Salaam.
Wanamichezo wa Tanzania wanaonekana wenye akili za kushiriki tu katika michezo ya Olimpiki, na wala sio kushinda, anasema Cyprian Maro, mkuu wa elimu ya viungo na sayansi ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
"Nadhani suluhisho pekee ni kuzigeuza mashirika ya michezo, kuwapatia mafunzo kizazi kipya na kurejea kujiunga tena na mashindano ya kimataifa baada ya miaka nane," maro aliiambia Sabahi.
Maro alisema serikali imejaribu kuipiga jeki michezo kupitia mabadiliko ya sera.
Mwaka 2008, serikali ilirejesha michezo katika mtaala wa shule za umma, baada ya kuusimamisha mwaka 1990. Pia inagharimia programu za maalumu za miaka miwili katika vyuo 11 kuandaa walimu wa elimu ya viungo na makocha katika shule za sekondari. Shule za umma huajiri wahitimu kutoka mpango wa mafunzo mara moja baada ya wao kupata mafunzo ya stashahada.
Hata hivyo, juhudi hizi hazioneshi kwa mafanikio ya timu kwa sababu mashirika ya michezo, kama vile Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC) na Chama cha Wanariadha cha Tanzania, hawasimamii vyema mafunzo ya wanamichezo.
Maro alisema mashirika ya michezo pia yanahitaji kupewa mafunzo ili kuwa na stadi zinazofaa za uendeshaji.
"Uwezo wa viongozi wa mashirika ya michezo ni mdogo sana," aliiambia Sabahi. "Wanaweza wakaweka rekodi za riadha na masumbwi, lakini hii haitoshi. Lazima wawe na uwezo wa kuandika mapendekezo ya gharama na kupanga michezo, badala ya kungojea serikali."
Msaada zaidi wa serikali uhitajika
Katibu Mkuu wa TOC Juma Ikangaa, mshindi wa medali ya fedha katika marathoni ya Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1982, aliilaumu serikali kwa kutowekeza katika michezo, na kusema kuwa mengi yanahitajika kufanywa ikiwa Tanzania ina ndoto za mafanikio.
Alisema serikali haitoi msaada unaohitajika kwa TOC ili kuwatayarisha wanariadha kwa viwango vinavyokubalika.
"Hatuwezi kuwa na programu bila ya pesa. [Kambi za mafunzo zinahitaji] pesa na hizi lazima zitoke serikalini kama ilivyo kwa nchi nyengine," Ikangaa alisema.
Alisema wafadhili watakuja mara pale michezo yatakuwa na mafanikio , kwa hivyo serikali inahitaji kuwekeza mtaji wa awali.
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni Amos Makala alielezea majuto ya serikali kwa utendaji wa wanariadha wa Tanzania katika Olimpiki, lakini aliwahamasisha Watanzania kucheza michezo zaidi ili kuwa na fursa bora kwenye michezo siku za usoni.
Bila ya shaka, matokeo ni mabaya, lakini hatupaswi kuvunjika moyo," Makala aliiambia Sabahi. "Tujipange wenyewe ili kushiriki katika michezo mingi zaidi kuliko tulivyofanya mara hii. Tujaribu michezo mengine zaidi ya riadha, kuogelea na ndondi."
Makala alisema Tanzania wana vipaji na wanaweza kufanya vizuri zaidi katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2016 huko Brazili ikiwa watafanya mafunzo na ikiwa TOC itapangwa bora zaidi.
"Ninawata Waanzania wawe wabunifu ili kuweza kupata medali zaidi katika michezo ijayo," alisema.

Source:Swahilivilla Blog

No comments:

Post a Comment