TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday, 20 September 2012

Na Gazeti la Tz Daima: JK anoa panga CCM

• Wabunge walioweka saini kumng’oa Pinda kukatwa NEC

Na Mwandishi wetu
PANGA la vikao vya juu vya mchujo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), limenolewa.
Vikao hivyo vya mwisho vya mchujo ambavyo vitaendeshwa na Mwenyekiti wake taifa, Rais Jakaya Kikwete, vinatarajia kuanza rasmi Septemba 21 na 26.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa wakati vikao hivyo vikianza, CCM imepanga mkakati mzito kukata majina ya baadhi ya wagombea uongozi ambao pia ni wabunge ndani ya Bunge la Muungano.

Kundi lingine la walengwa wa mkakati ule ni la viongozi wa CCM hasa wenyeviti wa mikoa na wilaya waliokuwa wakiendeleza makundi na malumbano na kusababisha kuporomoka kwa hadhi ya chama hicho.

Habari zaidi kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa NEC imepanga kufanya maamuzi magumu ya kuwakata baadhi ya wagombea waliokuwa wakiandamwa na tuhuma za ufisadi hata kama watakuwa wamepita bila kupingwa au kupitishwa na vikao vya chini.

Tayari Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, mmoja kati ya makada wanaoandamwa kwa tuhuma za ufisadi, amepita bila kupingwa wakati majeruhi mwingine wa ufisadi, Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, amepitishwa na vikao vya chini, sasa wanasubiri idhini ya NEC.

Duru za siasa kutoka ndani ya CCM, zinasema kuwa wabunge wanaolengwa kwenye panga hilo ni wale waliokuwa kimbelembele kuikosoa serikali bungeni na kufikia hatua ya kusaini majina yao kwenye fomu zilizokuwa zikipitishwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ili kupata saini 70 za kumng’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Tayari athari za saini za kutaka kumng’oa Waziri Pinda zimeshaonekana kwa Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ambaye hivi karibuni alienguliwa katika kikao cha mchujo wilayani na yeye kutahadharisha kama jina lake halitapitishwa NEC, ndani ya CCM patachimbika.

Mkono ambaye ni wakili maarufu nchini, aliwania nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazee taifa. Wengine waliowania nafasi hiyo ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Joson Rweikiza, Matha Mlata na Salum Chicago.

Waliopendekezwa na vikao vya chini kuwania kiti hicho ni Abdallah Bulembo, Matha Mlata na Halima Mamuya.

Kwa upande wa Umoja wa Wanawake, waliopendekezwa ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango na Mayrose Kavura Majinge.

Mbunge mwingine aliyekwishaenguliwa na vikao vya chini ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, ambaye alikuwa akichuana vikali na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.

“Tunaambiwa wabunge wengi walioomba NEC watakatwa hasa wale waliotaka kumng’oa Pinda na sababu ya pili ni kwamba wabunge wana nafasi kumi za NEC ndani ya Bunge, hivyo hawana sababu ya kuwania NEC nje ya Bunge,” alisema mtoa habari wetu.

Mkono, Nagu na wengine waliopendekezwa kuachwa na vikao vya chini, sasa wanategemea kudra za NEC.

Mkoani Shinyanga, taarifa zinasema kuwa mgawanyiko umetokea baada ya kuwapo taarifa kwamba kuna mpango wa kulikata jina la mwenyekiti wa sasa wa CCM mkoa huo, Khamis Mgeja.
Habari zinasema kuwa mkakati huo unapangwa na vigogo wa CCM kutoka ofisi ndogo ya makao makuu, Lumumba, jijini Dar es Salaam na kumhusisha mtoto wa kigogo.


Hatua hiyo imedaiwa kuwa ni moja ya mikakati ya viongozi hao kupanga safu ya uongozi mwaka 2015 ambapo Mgeja anatajwa kuwa mmoja wa watu anaopingana nao hivyo kuwa kikwazo katika kufanikisha mipango yao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wana CCM mjini hapa, inadaiwa kwamba vigogo hao hivi sasa wanajitahidi kuwashawishi wajumbe wa vikao vya juu ili kuhakikisha jina la Mgeja linakatwa na linabakizwa la mtu ambaye ni chaguo lao.

Yapo madai kwamba mkakati wa vigogo hao unaungwa mkono na baadhi ya wabunge wa CCM mkoani Shinyanga ambao hawamuungi mkono Mgeja.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamewaeleza waandishi wa habari mjini Shinyanga kwamba tayari kuna vikao vingi vya usiku vinavyofanywa na mawakala wa vigogo hao kwa lengo la kuhakikisha Mgeja hachaguliwi hata kama NEC itakuwa imerejesha jina lake.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mmoja wa wagombea ambaye alipata fununu za jina lake kupendekezwa kuwa miongoni mwa wagombea nafasi ya uenyekiti wa mkoa, aliamua kufanya sherehe kubwa katika moja ya baa eneo la Lubaga ambako alisikika akitamba kwamba yeye ni chaguo la Rais Jakaya Kikwete.

No comments:

Post a Comment