|
|
Na Fredy Azzah na Bonifasi Meena
KAMATI iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi
kuchunguza kifo cha mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi
imeweka hadharani ripoti yake inayoeleza madudu yaliyofanywa na pande zote;
polisi na Chadema na kusababisha mauaji hayo.
Wakati hayo yakibainika katika ripoti ya Kamati ya Waziri Nchimbi, Baraza la
Habari Tanzania (MCT) nalo limeanika ripoti yake kuhusu kifo hicho. Ripoti hiyo
inaonyesha kuwa mauaji hayo, yalitokana na uhasama uliopo baina ya polisi
mkoani Iringa na waandishi wa habari wa mkoa huo.
Kamati hizo ziliundwa kwa nyakati tofauti kutokana na vurugu zilizotokea
Septemba 2, mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi wakati
polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la
chama hicho katika kijiji hicho.
Wajumbe katika kamati ya Nchimbi ni Mwenyekiti Jaji Steven Ihema, Makamu
Mwenyekiti, Theophil Makunga na Ofisa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili
Mtambalike.
Wengine ni Ofisa aliyesomea masuala ya milipuko kutoka Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Kanali Wema W. Wapo pamoja na Naibu Kamishna wa Jeshi la
Polisi, Isaya Ngulu.
Kamati ya MCT ilikuwa ikiongozwa na John Mirenyi kutoka MCT, Hawra Shamte
kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini
Iringa, Simon Berege.
Ripoti ya Nchimbi
Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo imesema nguvu iliyotumika na polisi
kuwatawanya wafuasi wa Chadema siku ya tukio, ni kubwa na bomu lililomuua
Mwangosi, lilipigwa kutoka umbali mdogo badala ya mita 80 zinazotakiwa
kitaalamu, tena bila kumwelekezea mtu.
Imesema utaratibu wa matumizi ya bomu hilo unaelekeza kulenga juu usawa wa
nyuzi 45 na umbali wa mita 80 mpaka mita 100.
"Hakukuwa na umuhimu wa kutumia bomu hilo kwa sababu hata ingekuwa kwa
sababu ya kuwakamata watu, tayari askari polisi wapatao sita walikuwapo eneo la
tukio walitosha kwani operesheni haikuwa kubwa," imesema ripoti hiyo
iliyokuwa ikisomwa na Jaji Ihema.
Jaji Ihema alisema kamati imependekeza nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa
ziangaliwe upya kwa kuwa zinatumika kisiasa.
Hata hiyo, Jaji Ihema alisema kinachozungumzwa kuhusu ripoti hiyo ni muhtasari
tu wa ripoti nzima na wamefanya hivyo kuepuka kugusa mambo mengine ambayo
yataingilia mwenendo wa kesi iliyopo mahakamani.
Hata hivyo, akaeleza kuwa ripoti nzima inayoelezea kitu kilichotokea anaijua Dk
Nchimbi ambaye ndiye aliyeunda kamati hiyo.
Jaji Ihema alieleza kuwa kamati yake ilipewa hadidu sita za rejea ambazo ni
kuangalia kama mkusanyiko wa Chadema ulikuwa halali na kama kulikuwa hakuna
uvunjifu wa amani.
“Pia kuangalia kama nguvu iliyotumiwa na polisi ilikuwa sawa, mazingira
yaliyosababisha polisi kutumia nguvu na kusababisha mauaji ya Mwangosi, kama
kuna uhasama kati ya polisi na waandishi Iringa,” alisema Jaji Ihema na
kuongeza;
“Kuangalia kanuni na taratibu za polisi kuzuia mikutano ya siasa na uhusiano wa
Jeshi la Polisi na vyama vya siasa.”
Chadema nao walikuwa tatizo
Jaji Ihema alisema Chadema ndiyo chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani
kijijini Nyololo hasa kutokana na uamuzi wa kung’ang’ania kukusanyika isivyo
halali eneo hilo.
"Ikizingatiwa kuwepo kwa ujumbe wa SMS kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama
hicho Dk Willibrod Slaa uliosema, “IGP nasubiri simu yako. Wajulishe Polisi
wako waandae risasi za kutosha, mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji
na kisha kusherehekea, mjiandae kwa kwenda mahakama ya Hague. Ni afadhali tufe
kuliko manyanyaso haya,” alisema Jaji Ihema na kuendelea.
“Ujumbe huu ukiashiria umwagaji wa damu ni ushaidi tosha kuwepo kwa uvunjifu wa
amani.”
Polisi tatizo
Alisema kuhusu nguvu iliyotumika na polisi, kamati imebaini kuwa ilikuwa ni
kubwa kutokana na maelezo ya viongozi wa kijijini hapo.
“Mwangosi aliuawa wakati amri ya askari kuondoka kwenye eneo la tukio
ilishatolewa,” alisema Jaji Ihema na kuongeza;.
"Kamati imebaini kuwa ushirikiano wa polisi na waandishi wa habari mkoani
Iringa si mzuri hivyo ikapendekeza uangaliwe." Pia uhusiano kati ya polisi
na baadhi ya vyama vya siasa hauridhishi, hivyo ni muhimu kukawa na jukwaa la
kushughilikia hali hiyo, alisema Jaji Ihema.
Mapendekezo
Alisema kamati imeshauri kuwa sheria zinazotoa mamlaka za kuchunguza matukio ya
vifo kwenye mkusanyiko ziangaliwe kwa kuwa lililotokea Nyololo lina ushahidi wa
kutosha.
Jaji Ihema alisema kwa kuwa Jeshi la Polisi litabaki kuwa mlinzi wa wananchi,
siasa za ubabe na uhasama ziachwe.
Aliendelea kusema kuwa kamati inapendekeza utulivu uendelee kuwepo ili kuweza
kuondoa purukushani na pia viongozi waelimishwe juu ya umuhimu wa kutii
sheria.
“Kuwepo na programu mahususi ya uzalendo na kukuza maadili, elimu ya uraia
iimarishwe na mafunzo ya JKT yarudishwe mapema,” alisema.
Mapendekezo mengine ni kuboresha ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa
kuanzisha ofisi wilayani na mikoani kwa kuwa imelemewa
“Kwa upande wa vyama vya siasa viongozi wajifunze kuwa wavumilivu na kutii
sheria,” alisema Jaji Ihema.
Polisi ambao walihusika katika kumpiga marehemu Daud Mwangosi kabla.
Ripoti ya MCT
Ripoti ya Timu Maalumu iliyoundwa na MCT na TEF, kuchunguza tukio hilo imesema
mauaji hayo yalifanywa makusudi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi wa
Iringa, Michael Kamuhanda.
“Matokeo ya uchunguzi ya mazingira yaliyopelekea mauaji ya Daudi Mwangosi,
awali ya yote umethibitisha polisi kwa makusudi kabisa waliwashughulikia
waandishi wa habari wa Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za Chadema
katika Kijiji cha Nyololo,” inasema na kuongeza:
“Pia Daudi Mwangosi aliuawa mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa
moja kwa moja wa RPC Michael Kamuhanda. Matokeo haya yanathibitishwa na maelezo
pamoja na ushahidi uliokusanywa kwa kutumia picha za video na ushahidi mwingine
muhimu wa taarifa za vyombo vya habari.”
Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga aliyesoma ripoti hiyo alisema kuwa utafiti huo
ulibaini kuwa taarifa za mauaji wa Mwangosi zimekuwa zikikinzana kuanzia hatua
za awali jitihada za kuficha ukweli zilipojidhihirisha.
Ikifafanua juu ya uhusiano mbaya kati ya viongozi wa Serikali ya Mkoa huo
na Jeshi la Polisi dhidi ya waandishi, ilisema baadhi ya waandishi
waliwahi kupigwa na kuharibiwa vyombo vyao vya kazi.
“Novemba 2011, mwandishi Laurent Mkumbata anayefanya kazi ITV, alipigwa vibaya
na kamera yake ilivunjwa kwa makusudi na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (OCD) wa
Iringa Mohamed Semunyu wakati akiwa kazini,” ilisema:
“Waandishi wa habari wa Iringa pia, walitendewa vibaya na viongozi wa mkoa
wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mwishoni mwa Februari 2011. Waandishi katika
ziara hiyo walilazimika kulala kwenye basi walilosafiria kutokana na viongozi
kupuuza kuwapatia hoteli ya kulala.”
Kwa mujibu wa Mukajanga, Machi sita mwaka huu, polisi mkoani Iringa waliwapa
Klabu ya Waandishi wa Habari Iringa (IPC), kibali cha kufanya maandamano ya
amani kulalamikia kukua kwa uhusiano usio mzuri kati ya waandishi wa habari na
viongozi wa mkoa.
Mukajanga alisema tukio hilo waliwalenga zaidi waandishi wa Iringa ambao
walikuwa wanawafahamu zaidi na kuwaacha wale waliotoka Dar es Salaam.
Kabla ya kusomwa kwa ripoti hiyo, Mukajanga alitahadharisha juu ya tabia
aliyosema imeibuka ya watu kufungwa midomo kwa kisingizio cha kuwa kesi ipo
mahakamani.
Alisema kwamba, ana imani kuwa mahakimu na majaji nchini, ni watu wenye sifa
ambao wanaweza kufanya shughuli zao kwa kuzingatia ushahidi unaotolewa
mahakamani bila ya kuathiriwa na maneno ya mitaani. Soma muhtasari wa ripoti ya
Kamati ya Nchimbi….
|
No comments:
Post a Comment