P.O.B.O.X 79235 DAR ES SALAAM
KONGAMANO JUU YA MASUALA YA HAKI ZA WANAWAKE NA KATIBA
TAMKO
Sisi, wanawake kutoka asasi zisizo za kiserikali na
mitandao inayoshughulikia masuala ya kijamii kutoka mikoa 19 ya bara na
visiwani, tumekutana katika hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam mnamo Oktoba 22
hadi 24 kujadili haki za wanawake katika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Tunatambua kuwa wanawake wanaendelea kuhusishwa katika mchakato wa
kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya ulioanza mwaka huu. Mkutano huu ni
muendelezo wa harakati za kuhakikisha kwamba wanawake wanatoa sauti ya pamoja
ya kudai Katiba mpya izingatie masuala ya kijinsia.
Katiba ikiri kuwa imetokana na muafaka wa kitaifa uliyopata ridhaa ya mwanamke na mwanaume, hivyo wote wana haki ya kuwa na katiba, kuijua na kuitumia kama sheria mama ya ulinzi wa haki zao.
- Katiba
iwe na sura (chapters) maalum zinazoweka bayana haki za wanawake, haki za
watoto, na haki za makundi yenye mahitaji maalum.
- Katiba iandikwe
kwa lugha nyepesi na ya kueleweka kwa makundi yote, ikiwa ni pamoja na
kuzingatia watu wenye ulemavu, na vipengele vyote vizingatie mtazamo wa
kijinsia.
- Katiba
iunde chombo maalum kitakachosimamia haki za wanawake katika maeneo yote
ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
- Katiba
ibatilishe sheria zote zinazokinzana na haki za msingi za wanawake na
watoto wa kike hususani kubatilisha sheria na mila zote za ubaguzi wa
jinsia katika masuala ya ndoa, mirathi, haki za kumiliki. Kwa mantiki hii, Katiba ibainishe kwa
uwazi wajibu wa serikali wa kuchukua hatua zote za kisera na sheria ili
kulinda na kuhifadhi haki za wanawake katika maeneo hayo.
- Katiba
iwajibishe serikali kutekeleza mikataba yote iliyoridhia kuhusu haki za
wanawake na walemavu (CEDAW, CRC, ILO Convention). Mikataba hii itambulike
kuwa ni sheria za nchi ili kuepusha ucheleweshaji wa kutafsri au kuruhusu
uchakachuaji wa mikataba hii katika sheria za nchi.
- Katiba
iweke misingi ya kulinda utu wa mwanamke dhidi ya uonevu na ukatili wa
jinsia ndani ya ndoa na kwenye jamii, ikiwa ni pamoja na kukataza ubakaji
ndani ya ndoa, kukataza mila zinazomdhalilisha mwanamke, (tohara,
kurithiwa bila hiari) na kubainisha haki sawa ndani ya ndoa, kukataza ndoa
za utotoni za watoto wa kike. Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za
kisera na kisheria kuimarisha utekelezaji wa haki hizi.
- Katiba
iwajibishe serikali kuchukua hatua za kisera na kisheria kulinda haki za
msingi za walemavu, na wazee ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi,
kuheshimiwa, kupata taarifa, kufikia huduma, na haki ya ajira. Pia Katiba
iwajibishe serikali kuchukua hatua za kisera na sheria pamoja na kusimamia
utekelezaji wa haki za watoto wa kike na kiume katika masuala ya elimu,
huduma kuwafikia walengwa, ulinzi na heshima ya utu wao.
- Katiba
ikiri kwamba ardhi ya Tanzania ni mali ya Watanzania - wanawake na wanaume
na iwajibishe serikali kuchukua hatua za kisera na sheria zitakazoweka
misingi ya kumwezesha mwanamke kumiliki na kunufaika na utajiri huu wa
taifa letu kwa njia zifuatazo: (i) kuzuia uuzaji wa ardhi ya familia bila
ridhaa ya wanafamilia wote, (ii) kuzuia uporaji wa ardhi unaofanywa na
wawekezaji wa ndani na nje (iii)
kuwawezesha wanawake kupata taarifa za kuwekeza katika sekta mbalimbali za
taifa, (iv) kuzingatia mchango wa wanawake katika kilimo ikiwa ni pamoja
na kulinda haki zao katika sekta hii.
- Katiba
mpya ibainishe misingi itakayozuia kuhodhiwa kwa madaraka katika mihimili
mikuu ya utawala kwa jinsia moja. Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za
kisera na sheria ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa misingi ya haki
na kwa uwiano sawa katika uongozi wa mihimili mikuu, ngazi zote za
uongozi, na mashirika ya umma na binafsi: kwa mfano,
Ø
Taasisi ya Urais, Makamu,
Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Spika na Naibu Spika, wakuu wa mikoa na wilaya,
bodi za mashirika ya umma, na viongozi wa mashirika haya.
Ø Serikali iwajibishe mashirika binafsi kuzingatia msingi
wa usawa.
- Katiba
mpya iimarishe haki zilizopo za kufikiwa na kufaidi huduma za msingi kama
vile maji safi na salama, uhakika wa upatikanaji wa chakula, makazi bora,
elimu, hifadhi ya jamii pamoja na kusisitiza wajibu wa serikali wa
kuhakikisha huduma hizi za msingi zinawafikia wanawake wote wa Tanzania.
- Katiba
itambue wajibu mkubwa anaobeba mwanamke wakiwemo wanawake walemavu, katika
kuendeleza kizazi cha taifa bila kupewa nyenzo na bila ulinzi wa afya
yake. Serikali ipewe jukumu la kuchukua hatua za kisera na sheria,
kuhakikisha uwekezaji katika afya ya uzazi, pamoja na kuzingatia haki ya
mwanamke ya maamuzi ya msingi kuhusu afya ya uzazi na uzazi salama.
- Katiba
mpya itambue mchango mkubwa wa mwanamke katika kukuza na kuendeleza kizazi
cha taifa, na mchango huu uthaminishwe na kujumuishwa katika mfumo wa pato
la taifa.
- Katiba
itambue kwamba elimu ni haki ya mwanamke na mwanaume, na iwajibishe
serikali kuhakikisha kila raia anapata elimu hadi kikomo cha uwezo wake,
na pia kuchukua hatua za kisera na sheria za kuhakikisha utekelezaji huu.
Serikali iwajibishwe kuchukua hatua za makusudi za kuhakikisha kuweka
mitaala yenye kujenga dhana ya usawa wa wanawake inatekelezwa nchini kote.
Imetolewa
24 Oktoba 2012, Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment