TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 21 November 2012

Uharamia, Usafirishaji wa Binadamu tatizo nchi za SADC


Uharamia na biashara ya usafirishaji wa binadamu ni changamoto inayotafutiwa ufumbuzi na vyombo vya Usalama vya Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na Usalama cha SADC,  Kanali Gerson Sangiza  alisema  dunia kwa ujumla bado inaangalia namna  ya kutatua tatizo hilo.
 
Alisema ufumbuzi wa suala hilo ni mgumu  kutokana  na ukweli kwamba maharamia na wale wanaojihusisha na biashara ya uuzaji wa binadamu hushirikiana kwa karibu na kwa siri na  wananchi wa nchi husika. "Tatizo ni kwamba wananchi ndiyo wanaoendesha vitendo hivyo kwa hiyo namna ya kuwakamata inakuwa ni shida" Alisema Kanali Sangiza.
 
Mkuu huyo aliongeza kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na taasisi zinazoshughulikia masuala hayo unahitajika. Mpaka sasa nia na madhumuni ya biashara hiyo ya uuzaji wa binadamu bado haijajulikana 
 na wale waliokamatwa wakijihusisha na bado wanashikiliwa.
 
"Inasikitisha kuona binadamu wengi wanasafirishwa kutoka Somalia kupitia Kenya, Tanzania, Malawi na kupelekwa Afrika ya Kusini ambapo mpaka sasa Afrika kusini ina wahamiaji haramu milioni tano", alisema kanali Sangiza.
 
Mkuu huyo wa kitengo cha Ulinzi na Usalama cha SADC alisema pamoja na tatizo la uharamia na usafirishaji wa binadamu, nchi wanachama wa Jumuiya hiyo pia zinakabiliwa na changamoto ya matishio ya kufanyika kwa vitendo vya kigaidi ambavyo vinahatarisha uhusiano kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea.
 
  SADC kupitia chombo chake cha Ulinzi na Usalama imeandaa mikakati maalumu kuhakikisha kwamba nchi wanachama wa jumuiya hiyo hazisumbuliwi na matatizo ya uharamia na usafirishaji wa binadamu. Katika hatua ya kukabiliana na changamoto hizo, wakuu wa Polisi wa nchi  zote 15 za SADC walikutana mwezi Septemba Zanzibar ili kujadili mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama likiwemo tatizo la uharamia na biashara ya usafirishaji wa binadamu.

No comments:

Post a Comment