TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 8 March 2013

Na Gazeti la HabariLeo:Mkwe auawa akidai mahari

 Na Samson Chacha
KWA kawaida mkwe ni mtu anayeheshimiwa katika ukoo, lakini kilichotokea wilayani hapa ni cha kushitua na kustaajabisha.

Mkazi wa Kijiji cha Genkuru, Marwa George (38), anadaiwa kuuawa kwa kuchomwa mkuki kwenye paja la kushoto na baba mkwe, John Mhabe (67).

Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika Kijiji cha Kitawasi, anakoishi baba mkwe huyo, baada ya George kwenda kudai mahari aliyotoa ili kuoa kwenye nyumba hiyo.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa Maalumu wa Tarime Rorya, Justus Kamugisha, alisema jana kuwa George alipooa, alitoa mahari ya ng’ombe 10.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, miaka mitatu iliyopita, George alikimbiwa na mkewe huyo ambaye jina lake halijapatikana, kutokana na migogoro ya ndani, ambayo haikufafanuliwa na inasemekana, alikwenda Geita na kujiunga na wachimbaji wadogo wa dhahabu.
Alisema baada ya kukimbiwa na mkewe, George alikwenda kudai ng’ombe aliotoa kama mahari na alipofika nyumbani kwa baba mkwe, moja kwa moja aliingia zizini na kuchagua ng’ombe.
Inadaiwa alichagua mafahari watano na kuwatoa zizini ingawa baadhi ya mashuhuda wakati akiwatoa mafahari hao walimsihi kuacha kitendo hicho, lakini alikaidi na kuwaswaga kuelekea kwake.
Wakati akiondoka nao, inadaiwa baba mkwe alikasirika na kuchukua mkuki na kumchoma kwenye paja la kushoto na kumsababishia kuvuja damu nyingi na kufariki dunia.
Kamanda Kamugisha alisema Polisi inamshikilia mtuhumiwa huyo na baada ya mahojiano, anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji.
Tayari mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa na ndugu zake kwa mazishi kijijini kwake Genkuru.
Kamanda Kamugisha alitaka wananchi kutojichukulia sheria mkononi, badala yake wafuate sheria na kupunguza hasira wakati wakitaka kuchukua uamuzi.
Aliwataka kama watashindwa kudhibiti hasira, washirikishe wana ndugu badala ya kujiamulia, ili kuepuka maafa kama hayo.

ZAIDI NUNUA HABARILEO

No comments:

Post a Comment