TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 17 April 2013

Ushahidi Kesi za kubaka/mimba ni Changamoto Handeni

Na Thehabari.com, Handeni

 “KESI nyingi za tuhuma za kubaka na mimba kwa wanafunzi zinazotufikia zinashindwa kufikia hukumu maana mashahidi wanashindwa kuthibitisha pasipo shaka…nyingi zinaharibika sababu hawataki kusema ukweli, hivi karibuni nililazimika kuwaweka ndani wawili (mashahidi) kwa kuwa wanadanganya. 

Unakuta maelezo aliyotoa polisi ni mengine na akifika huku anageuka,” anasema Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi wa Wilaya ya Handeni, Patrick Maligana alipofanya mahojiano na mwandishi wa makala haya hivi karibuni. 

Hakimu Maligana anasema licha ya takwimu zao kuonesha kesi za mimba/kubaka wanafunzi kwa sasa zinapungua bado suala la kuharibika kwa ushaidi wa kesi za mimba ni changamoto. 

Anasema kesi nyingi za wanafunzi zimekuwa zikishindwa kufanikiwa hadi hatua ya hukumu kutokana na mtindo wa kuvuruga ushahidi. 

Anasema awali kikwazo kikubwa kwa kesi kama hizo ilikuwa ni upande wa wazazi na walimu kutotoa ushirikiano wa kutosha kwenye mchakato wa kesi. Lakini walimu na wazazi wameacha usumbufu huo hivyo imebaki kwa wanafunzi pamoja na watuhumiwa ambao mara kadhaa wanakuwa wapenzi wao. Anaongeza kuwa licha ya matukio hayo kupungua changamoto bado zipo.


Takwimu za kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2012 zinaonesha mahakama hiyo ilipokea kesi 10 za tuhuma za mimba/kubaka kwa wanafunzi, huku kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2013 ni jumla ya kesi sita tu zimepokelewa katika mahakama hiyo. Anasema kesi sita za mwisho kupokelewa zipo katika hatua anuai.
Zuber Chembera ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Handeni (OCD), akizungumza na mwandishi wa makala haya ofisini kwake, anakiri kupungua kwa matukio ya kesi za mimba/kubakwa kwa wanafunzi Wilaya ya Handeni kutokana na takwimu zao.
Anasema kwa mwaka 2012 hadi mwezi Novemba walikuwa na jumla ya matukio ya kesi kama hizo 66, lakini kwa mwaka huu (Machi, 2013) kuna jumla ya matukio ya kesi kama hizo 14 tu yalioripotiwa.
Anasema elimu inayotolewa na Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto Kituo cha Handeni imesaidia. “Kesi zinazotufikia hapa huku zikiwa na ushaidi wa kutosha tunazipeleka mahakamani, zile zinazokuwa hazina ushaidi wa kutosha tunajaribu kuzifuatilia kiuchunguzi kwa mujibu wa taratibu zetu. Lengo letu kupitia Dawati la Jinsia na Watoto ni kuhakikisha tunapunguza kama sio kumaliza kabisa vitendo hivyo.
Anasema maranyingi ushahidi wa kesi kama hizo pia umekuwa ukiharibiwa na wahusika kabla ya kufika mahakamani, wanaweza baada ya kesi kufunguliwa wakashawishiana na kukaa nje bila ya sisi kujua na hivyo kupotea wote.
Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Nadhiru Kinyama anasema idadi ya matukio ya mimba shuleni hapo inapungua kwa sasa tofauti na ilivyokuwa hapo awali, lakini si kwamba matukio hayo yamekoma kabisa.
“Matukio ya mimba kimsingi kwa sasa yanapungua…lakini si kwamba yamekwisha kabisa, tatizo kubwa ni malezi katika familia pamoja na vishawishi vingine,” anasema mwalimu huyo akizungumza shuleni Komnyang’anyo.
Napingana kwa mtazamo mwingine kwamba umbali wa makazi kwa wanafunzi unachangia mimba…nasema hivyo kwa kuwa kwa mwaka jana mwishoni kuna mfano mzuri, shuleni kwetu yupo mwanafunzi (wa kidato cha pili ‘C’) ambaye anahudumiwa kila kitu na pia yu-karibu na shule lakini amejikuta akipewa mimba na kukatishwa masomo.
Mwanafunzi huyu pia huwezi kumuingiza katika kundi la wanafunzi wenye mazingira magumu ya maisha katika familia zao, nasema hivyo kwa kuwa huyu analipiwa kila kitu, anapewa matumizi yote yanayoitajika na shirika moja linalosaidia wanafunzi wa kike lakini ameshindwa kuendelea baada ya kupewa mimba.
Kesi hii tayari ipo kwenye Serikali ya kijiji kwa hatua zaidi baada ya sisi kutoa taarifa. Sasa watu wanachukulia hatua si kama ilivyokuwa hapo nyuma.Tangu amekuwa huyu Mkuu wa Wilaya mpya (Muhingo Rweyemamu) wananchi wanatoa ushirikiano kwa kesi kama hizi. Kimsingi ujenzi wa mabweni itakuwa hauweni kwa wanafunzi ambao kwa sasa wanatokea vijiji vya mbali kuja shuleni, vijiji hivyo ni pamoja na Bangu, Kwamagome na Kwakonje.
Mazungumzo ya wanafunzi Hamad Ngomero kidato III, Salome Kalage kidato cha IV, Michael Richard kidato cha I, Mwajuma  Munga kidato cha II, Mwajabu Fungo kidato I na Farid Iddy kidato cha IV - wote kutoka Shule ya Sekondari Komnyang’anyo wanakubali kwa pamoja uwepo wa matukio ya mimba, japokuwa kwa sasa ni kwa kiwango kidogo.
Mwajuma Munga anasema matukio hayo bado yapo lakini yamepungua si kama ilivyokuwa hapo nyuma. Naye Salome Kalage anasema mfano kuanzia mwezi Januari 2013 anawajua wanafunzi watatu ambao wamepata mimba na kuachishwa shule. Anawataja wanafunzi hao ni pamoja na Kuruthumu Omar (IV), Elizabeth Hamis (IV) na Docas (III).
Kwa upande wake mwanafunzi Hamad Ngomero anasema tamaa za starehe na hali ngumu ya maisha katika familia kaadhaa wilayani Handeni ndiyo inayowaponza wanafunzi wa kike na hata kujikuta wakitiwa mimba na kukatishwa masomo.
Martin Mwingo ni Mwaliku Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Kileleni; ujio wa Mkuu wa Mkoa mpya Handeni umeanza kuonesha mafanikio kwa upande wa matukio ya mimba kwa wanafunzi. “DC (Mkuu wa Wilaya) wasasa anajitahidi sana kupitia kampeni yake ya “Niache Nisome” anafuatilia kesi za mimba na kuhakikisha wahusika wanapata adhabu kwa mujibu wa sheria…mfano sasa hivi tuna kesi moja tumeletewa hizi ni juhudi za Mkuu wa Wilaya,” anasema Mwingo.
Kesi zinapungua mfano mwaka jana tulikuwa na kesi mbili za mimba lakini mwaka huu (2013) hadi sasa hatujapata kesi ya mimba…lakini pamoja na hayo malezi ya watoto kwa wazazi bado ni tatizo, mtoto ananyenyekea kea mzazi wake tu dharau kwa watu wengine-haya si malezi. Zamani mtoto anaweza kuadhibiwa na mkubwa yeyote ilimradi awe amekosa, lakini sasa sivyo.
“Mi nashangaa kila uchao watu wanang’ang’ania haki za watoto wasiadhibiwe uweke utaratibu wa kutoa adhabu lakini nashangaa kwanini wasitaje na wajibu wa mtoto hili ni muhimu…tusing’ang’anie haki za mwananafunzi tu tuoneshe na wajibu wake pia,” anasema Mwalimu Mwingo.
Anasema pamoja na juhudi hizo bado utandawazi unaathiri nidhamu za wanafunzi, umiliki wa simu za mkononi matumizi mabaya ya mitandao kama tovuti nayo yanawaharibu wanafunzi, ipo haja ya Serikali kuingilia na kupiga marufuku wanafunzi kumiliki simu shuleni maana simu inamambo mengi sasa.
Hussen Kigoma ni mwanafunzi wa kidato cha III, katika moja ya shule za kata Wilaya ya Handeni ambazo ndizo zimezokuwa na changamoto anuai. Anasema ipo haja ya kuwa na utaratibu wa kuwapima vipimo vya ujauzito mara kwa mara wanafunzi wa kike.
“Sasa hivi wapo ambao wanapata na kutoa mimba hizo bila uongozi wa shule kujua…sasa hivi tunawajua wanafunzi wawili ambao walipata mimba mwaka huu shuleni kwetu. Mfano Joyce Gasper na Jesca Paul wote wa kidato cha nne wamepata mimba…huenda mwaka huu mimba zikaongezeka zaidi,” anasema Hussein Kigoma.
 Eliakimu Kapele ni Makamu wa Shule ya Sekondari Kivesa; anasema linapungu tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma. Mfano mwaka jana tulikuwa na matukio mengi ya kesi za mimba kwa wanafunzi, lakini hadi muda huu kwa 2013 tunayo matukio mawili tu. Na hatu zinachukuliwa maana msukumo unaanzia kutoka kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Hii inatokana na Mkuu wa Wilaya wa sasa Muhingo Rweyemamu ametia mkazo sana masuala ya mimba kwa wanafunzi, watu wamekuwa makini na wafuatiliaji.
“Mfano sasa mimba inapotokea kuanzia mzazi wa mtoto aliyetiwa mimba, mtoto mwenyewe na mtuhumiwa wote wanashikiliwa…mi naamini kama adhabu hizi zitaendelea kutolewa ipasavyo watu watanyooka tu,” anasema mwalimu Kapele.
Hata hivyo mwalimu huyo anashauri mabadiliko ya sheria na kanuni za utoro shuleni, anasema maamuzi yamekuwa na mkanganyiko. Mfano kanuni za shule zinaelekeza kuwa mwanafunzi asipo hudhuria shule kwa siku 90 afukuzwe shule. Hili kwa sasa halifanyiki maana limekaa kisiasa zaidi…wanafunzi wanatoroka hatua zinachukuliwa kwa mujibu wa maelekezo lakini baadaye wanarejeshwa kuja kufanya mitihani, hili ni tatizo.
“Inatokea mwanafunzi anabeba mimba na baadaye anarudi shuleni baada ya kujifungua, mwanafunzi kama huyu ni tatizo hawezi kuwa na vurugu sana kinidhamu na wakati mwingine anawavuruga hata wenzake maana anakuwa hana maadili.”
Shule yetu inautaratibu mzuri wa kuhakikisha muda wote unaofaa wanafunzi wanakuwa darasani kupata kilichowaleta hapa shuleni. Lakini huwezi kuamini kuna baadhi ya wanafunzi muda wote wapo huku vichochoroni wanajificha hawaji shuleni, utoro umekithiri! Lakini hawa huenda wakaruhusiwa kuja kufanya mitihani hapo baadaye.
Kanuni za shule mara kadhaa zimewekwa pembeni na siasa kuingizwa kwenye kanuni hizo, hali hii inawapa wanafunzi kiburi na uhuru mkubwa-huwenda wanadhani kufanya hivi ni kuwasaidia lakini ukweli ni kwamba wanawaharibu.
Ofisa Elimu Wilaya ya Handeni, Mgaza Muchiwa anakiri kuwepo na mabadiliko makubwa ya utoro wa mimba ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka jana. “Kimsingi huko nyuma utoro hasa wa mimba ulikithiri kwa wanafunzi wa Sekondari na Msingi, lakini hali ya sasa ni tofauti. Kuna mabadiliko kampeni ya ‘Niache Nisome’ imesaidia sana…kwa sasa wengi wanaohusika na kuwatia mimba wanafunzi wanapelekwa mahakamani,” anasema Muchiwa.
Anasema zoezi la kamatakamata lililokwenda sambamba na kampeni ya ‘Niache Nisome’ na watu hufikishwa kwenye hatua mbalimbali limesaidia hivyo mambo yanabadilika. Kwa mantiki hiyo waweza kuona kuanzia Januari 2013 hadi sasa (Machi) sijapokea kesi hata moja ya mimba.
Tunachokifanya sasa ni kutoa elimu zaidi kwenye mikutanyiko ya jamii kupitia viongozi wa ngazi mbalimbali za halmashauri, ili kuhakikisha tunafanikiwa zaidi tumeanza mkakati wa kuwajengea uwezo wananchi na shule. Hii ni kukabiliana na baa la njaa ambalo limekuwa likijitokeza mara kadhaa.
“Unajua mtu anapokuwa na njaa kushawishika ni rahisi…na Handeni kuna njaa sasa hali kama hii yaweza kuathiri pia sekta ya elimu, tumejipanga kuimarisha kilimo cha mazao kama mahindi na mtama shuleni ili wanafunzi wawe na uhakika wa chakula wawapo shuleni,” anasema Ofisa Elimu huyo wa Wilaya ya Handeni.
Ofisa Elimu Taaluma, Basil Mrutu anasema kwa mwaka jana kwa mujibu wa takwimu zao walikuwa na ripoti za mimba 26 kwa Wilaya nzima, lakini tangu Oktoba 2012 hadi sasa hawajapata kesi za matukio ya mimba.
Simon Mdaki ni Mkuu wa Idara ya Sekondari Wilaya ya Handeni; anasema kuwa “Halmashauri imeandaa matrekta 7 ambayo shule zitapewa kipaumbele cha kuyatumia ili kuweza kuendesha kilimo kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TAMWA

No comments:

Post a Comment