TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 29 May 2013

Onyo la tume kuhusu mishahara ya wabunge

Tume ya mishahara nchini Kenya, imesema kuwa makarani wa bunge wenye jukumu la kuwalipa mishahara wabunge huenda wakapatikana na hatia ya kutumia vibaya mamlaka yao na kufuja pesa za umma ikiwa watawalipa mishahara ya juu wabunge kinyume na ile iliyoratibiwa na tume hiyo katika gazeti rasmi la serikali.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Sarah Serem ameonya kuwa makarani wa bunge la taifa Justin Bundi na yule wa Senate, Jeremiah Nyegenye huenda wakapatikana na hatia ya matumizi mabaya ya mamlaka ikiwa watakiuka agizo hilo.

"katiba inatupa mamlaka ya kuratibu mishahara ya maafisa wa serikali. Na hivyo ndivyo tulivyofanya,'' alisema mwenyekiti wa tume hiyo Bi Serem.

Bi Serem alisema kuwa tume hiyo ilichapisha mishahara watakayopokea wabunge kwenye gazeti rasmi la serikali kwa nia nzuri.

"SRC haikushurutishwa kuchapisha taarifa hiyo katika gazeti rasmi la serikali. Lakini tuliamua kufanya hivyo kwa njia njema na ili wananchi waweze kupata habari hiyo.'' aliongeza Bi Serem

Tume hiyo hata hivyo iliwapongeza Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kusisitiza kuwa serikali ipunguze matumizi ya pesa za uma.

Bi Serem alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa na wawili hao ili kutenga pesa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Onyo la tume limekuja siku moja baada ya wabunge kupiga kura kupinga tangazo la tume hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu kiwango cha pesa watakachopokea wabunge.

Tangazo hilo lilisema kuwa kila mbunge atapokea shilingi laki tano za Kenya ambazo ni dola elfu sita. Wabunge hao wanapigania kulipwa dola elfu kumi na kuwafanya kuwa miongoni mwa wabunge wanaopokea kiasi kikubwa sana cha mishahara duniani.
Chanzo.Bbc swahili

No comments:

Post a Comment