Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan(Picha Dw swahili)
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ametangaza hali ya hatari katika
majimbo matatu nchini humo, na kuamrisha wanajeshi zaidi wapelekwe
katika majimbo hayo ili kukabiliana na kundi la Kiislamu la Boko Haram.
Kundi lenye msimamo mkali wa dini ya Kiislam la Boko Haram limezidisha
mashambulizi dhidi ya vyombo vya usalama na shabaha za serikali katika
ngome yake kaskazini-mashariki mwezi huu, hali iliyomlaazimu rais
Jonathan kutangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Yobe na
Adamawa.
Wanajeshi wa Nigeria wakisimama wakati wa gwaride katika kijiji cha Baga, nje ya Maiduguri, jimboni Borno Mei 13.2013.
"Baada ya mashauriano mapana, na kwa kutumia mamlaka niliyonayo chini ya
vifungu vya ibara ya tatu, kifungu kidogo nambari moja cha katiba ya
Nigeria ya mwaka 1999 kama ilivyofanyiwa marekebisho, natangaza hali ya
hatari katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa," alisema rais Jonathan
katika hotub yake iliyotangazwa moja kwa moja na vituo vya redio na
televisheni.
Mgogoro wa viongozi wa kaskazini
Rais Jonathan pia alimuagiza mkuu wa majeshi nchini humo kupeleka vikosi
zaidi katika majimbo hayo, katika hatua ambayo inaweza kumtumbukiza
katika mgogoro na magavana wenye nguvu na viongozi wa kaskazini, ambao
tayari ana uhusiano wa mashaka nao. Siku ya Jumatatu, jukwa la magavana
wa Nigeria, ambalo linawakilisha magavana wa majimbo 36 ya nchi hiyo
walimuonya Jonathan dhidi ya kuweka utawala wa hatari kama jawabu kwa
uasi wa Boko Haram.
Maagizo yake yanafuatia ushahidi unaoongezeka kuwa kundi la Boko Haram
sasa linadhibiti maeneo kaskazini-mashariki, karibu na ziwa Chad, ambako
maafisa wa serikali wameripotiwa kukimbia. Duru za usalama zinasema
kundi hilo linadhibiti angalau maeneo 10 ya utawala katika jimbo la
Borno, ambalo ndiyo kitovu cha uasi wake.
Boko Haram yadhibiti maeneo kaskazini
Wapiganaji kadhaa wa kundi hilo wakiwa katika mabasi na magari
yaliyofungiwa bunduki za rasharasha yaliuzingira mji wa Bama jimboni
Borno wiki iliyopita, na kuwaachia wafungwa zaidi ya 100, na kuua watu
55 wengi wao wakiwa maafisa wa polisi na wanajeshi.
Na siku kadhaa kabla, watu kadhaa waliuawa katika kijiji cha uvuvi cha
Baga ambacho pia kiko jimboni Borno karibu na ziwa Chad, wakati kijiji
hicho kilipovamiwa na vikosi vya Nigeria, Niger na Chad vikiwasaka
wapiganaji wa Boko Haram. Wenyeji wa kijiji hicho walisema wanajeshi hao
walihusika na mauaji makubwa ya raia.
Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shekau.
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau alisema katika mkanda wa
video wiki hii kuwa kundi lake limewateka wanawake na watoto wengi
katika ulipizaji dhidi ya vikosi vya usalama, ambavyo alisema
vinawashikilia wake na watoto wa wanachama wa kundi hilo pasipo na kosa
lolote. Shekau pia alikataa pendekezo la rais Jonathan la kutoa msamaha
kwa wapiganaji wa kundi, hali ambayo yumkini imechochea amri hii ya hali
ya hatari.
Kumekuwepo na ongezeko la vurugu katika majimbo mengine ya Nigeria,
ambapo maafisa 46 wa polisi waliuawa na watu wenye silaha katika
shambulio la kuvizia katika jimbo la kati la Nassarawa wiki iliyopita,
ambapo maafisa walililaum kundi la madhehebu ambalo halihusiki na Boko
haramu.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef
Chanzo:DW swahili
| | | | | | | | | |
|
|
No comments:
Post a Comment