TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday, 6 May 2013

Uongozi mpya Chaneta wakabidhiwa Ofisi


UONGOZI mpya wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) umekabidhiwa  vifaa na mali zote za  Ofisi hiyo, na uongozi uliomaliza muda wake  chini ya Mwenyekiti mstaafu Anna Bayi huku kukiwa hakuna Ofisi.

Makabidhiano ya vifaa na mali za Ofisi yalifanyika jana katika uwanja mkubwa wa Taifa, huku viongozi wapya wakiwa na changamoto ya kutafuta Ofisi ya kufanyia kazi zao, baada ya kuelezwa kuwa Ofisi iliyokuwa ikitumika mwanzo kwa shughuli za Chama hicho mkataba wake umekwisha.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu mstaafu wa Chaneta Rose Mkisi alitaja mali alizokabidhi kwa uongozi mpya kuwa ni pamoja na  Gari aina ya Noah, akaunti mbili moja ikiwa chini ya Chaneta na nyingine ikiwa chini ya mke wa Waziri Mkuu Tunu Pinda ambazo zote zina kiasi cha shilingi laki  3 kwa 3.

Vifaa vingine vilivyokabidhiwa ni pamoja na meza mbili, komputa moja, Ups 1, wireless 1, saa ya ukutani, heater, mipira, jezi za netiboli, saa ya ukutani, tuzo mbalimbali, vikombe vine vya klabu bingwa ambavyo vilikuwa nje ya ofisi na vifaa vingine mbalimbali.

Akizungumza wakati anakabidhi vifaa hivyo, Mwenyekiti mstaafu wa Chaneta Anna Bayi alisema anawashukuru watanzania, viongozi mbalimbali akiwemo mke wa Rais Mama Salma Kikwete, mke wa Waziri Mkuu Tunu Pinda kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha timu ya netboli taifa kushiriki michezo ya ndani na kimataifa kwa mafanikio makubwa.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi bega kwa bega na Chama cha Netiboli na kufanikiwa kupata  ubingwa wa pili Afrika mwaka jana, lakini pia waliweza kusaidia timu ya netiboli kwenda kushiriki katika mashindano ya kimataifa Singapore mwaka jana.

“Tunawashukuru watanzania, viongozi wetu wamekuwa wakifanya kazi nasi bega kwa bega katika kuhakikisha mchezo wa netiboli unafahamika sio tu upande wa Tanzania peke yake bali pia tumeweza kwenda hadi ngazi ya kimataifa,”alisema.

Bayi alisema timu ya netiboli ilishika nafasi ya pili katika mashindano ya netiboli Afrika, lakini pia waliwezesha nchi kushika nafasi ya 11 duniani kutokana na mchezo huo.

Akipokea vifaa hivyo, Mwenyekiti mpya wa Chaneta Anna Kibira aliahidi watanzania kuwa ataendeleza juhudi zilizoachwa na uongozi uliopita, na kuongeza kuwa kama kuna mabaya atayaacha kama yalivyo.

Hata hivyo, alisema atazungumza na Baraza la Michezo Tanzania(BMT) ili kumpa mwongozo wa nini afanye ili aweze kutafuta Ofisi mapema iwezekavyo kwa ajili ya kuanza kazi haraka.

Chaneta ilifanya uchaguzi wake mkuu April 20, mwaka huu mjini Dodoma na kupata uongozi mpya ulio chini ya Mwenyekiti wake Anna Kibira.

No comments:

Post a Comment