TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 19 June 2013

Ongezeko la wakimbizi duniani lazidi kushika kasi




 WAKATI dunia inaadhimisha siku ya wakimbizi duniani leo, Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi(UNHCR) limesema bado kuna ongezeko la idadi kubwa ya wakimbizi au wakimbizi wa ndani duniani huku  Tanzania idadi hiyo ikiwa imepungua.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwakilishi wa UNHCR nchini Joyce Mendes-Cole alisema ripoti ya shirika hilo imeonyesha ongezeko la wakimbizi kutoka wakimbizi milioni 42.5 mwaka 2011 hadi kufikia milioni 45.2 mwishoni mwa mwaka jana.


Alisema  “kati ya  idadi hiyo yaani milioni 45.2,  kuna idadi ya wakimbizi milioni 15.4 wakati  wanaotafuta makazi wapo 937,000 na watu milioni 28.8 ni wale wanaondoka kwenye makazi yao na kukimbilia katika maeneo mengine ndani ya nchi yao kutokana na sababu mbalimbali,”.


Cole alisema sababu kubwa inayochangia ongezeko hilo ni vita ambapo asilimia 55 ya wakimbizi wote  wanatoka katika nchi za Afghanistan, Somalia, Iraq, Syria na Sudan.

Kwa upande wa Tanzania, alieleza kuwa idadi ya wakimbizi imepungua tofauti na siku za nyuma kutoka wakimbizi waliokuwepo 700,000 hadi kubakia 102,000 hivi leo.


Alisema wakimbizi wengi waliokuwepo nchini tayari walisharudishwa makwao na wengine 16,000 walitafutiwa makazi katika nchi nyingine. 


Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi  ya tano duniani yenye kambi kubwa ya kuwahifadhi wakimbizi inayofahamika kama  Nyarugusu ambapo ina jumla ya wakimbizi  68,000, wengi wakitokea Jamhuri ya Kongo ambayo ni nchi ya sita inayotoa  idadi kubwa ya wakimbizi.


Cole alisema changamoto kubwa iliyojitokeza ni kuhusiana na wakimbizi wa Burundi wapatao 162,000 waliopewa hadhi ya uraia wa Tanzania kama wakulima katika mkoa wa Tabora na Katavi  mwaka 2009/2010 kuwa bado hawajapewa nafasi ya umiliki wa ardhi. 
Kutokana na changamoto hiyo, alisema ni muhimu hatua ichukuliwe  mapema ili kuwaruhusu kuishi kwa haki na amani.

No comments:

Post a Comment