TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 21 June 2013

Wanaharakati Waichambua Bajeti Mpya ya Serikali 2013-14


Mchambuzi wa Sera kutoka asasi ya TOWSF, Badi Darusi akizungumza leo katika mkutano huo, Kulia ni Marcelina Kibena mkazi wa Morogoro

Baadhi ya wanahabari na wanaharakati wa kijinsia wakiwa katika mkutano huo
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wanaharakati ngazi ya jamii kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Pwani, Shinyanga na wadau wengi wa mtandao huo wameichambua bajeti mpya iliyosomwa hivi karibuni bungeni na kuainisha masuala anuai ndani ya bajeti hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosomwa na Marcelina Kibena mkulima mkazi wa Morogoro, wanaharakati hao wa ngazi ya jamii kwa upande mmoja wameridhishwa na kitendo cha Serikali kutambua kasoro zilizokuwepo maeneo mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato na usimamizi wake kama vile mfumo wa ukusanyaji kodi ambapo kwa sasa imerdhamiria kufanya maboresho ya sheria anuai za kodi.

Hata hivyo wameainisha mapungufu mengi ambayo yamejitokeza katika bajeti mpya na kuainisha maoni yao ikiwa ni pamoja na kuitaka Serikali iunde mfumo  shirikishi na endelevu utakaoweza kutengeneza bajeti ya taifa kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi wote wanawake na wanaume na makundi mengine yaliyoko pembezoni.


"...Mikakati ya kilimo ilenge kuboresha na kuthamini hali ya wakulima wadogo. Maendeleo ya kilimo yazingatie kuboresha hali ya wakulima wadogo ambayo kwa sasa bado ni duni...Kukua kwa uchumi wa nchi kuende  sanjari na kupunguza umaskini kwa wananchi wote  wanawake na wanaume na makundi mengine yaliyoko pembezoni," alisema Kibena akizungumza na wanahabari kwa niaba ya wanaharakati wote.

Aliongeza katika mapendekezo yao wanashauri sekta ya afya iwe ni kipaumbele cha bajeti na serikali itenge 15%  ya bajeti kufuata azimio la Abuja, kwani hiyo ni moja ya sekta ya msingi na muhimu kwa ustawi wa jamii yote, hususan wanawake na nguvukazi ya taifa zima.

Walishauri kuwepo na uwajibikaji zaidi katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali ikiwemo kuondoa misamaha ya kodi isiyokuwa na tija na Upunguzaji wa utegemezi wa bajeti ya ili kupunguza mzigo wa kulipa deni na kuelekeza rasilimali kwa maendeleo ya watu. 

"Bajeti imeainisha mapato ya sh. za Kitanzania trilioni 18.2. Kati ya hizo matumizi ya kawaida ni sh. trilioni 12.6 wakati sh. trilioni 5.6 ni matumizi ya maendeleo. Tumeshangazwa kuona deni la taifa ambalo ni sh. za Kitanzania trilioni 23.6, likiongezeka na kuwa kubwa kuliko bajeti ya taifa. Katika bajeti kiasi cha sh. trilion 6.7, ambayo ni sawa na asilimia 36.8 ya mapato ya bajeti inategemea mikopo na misaada kutoka kwa wahisani na wafadhilii mbalimbali."

"Bajeti imeanisha kiasi cha sh. bilioni 383.4 kama mapato kutoka halmashauri. Hii ina maana kwamba kwa idadi ya halmashauri za wilaya ambazo ni 152 wastani wa kila halmashauri ni kukusanya sh. bilioni 2.5. Je, huu ndio uwezo halisi wa halmashauri katika ukusanyaji wa mapato ukizingatia rasilimali na vyanzo vya mapato vilivyopo katika wilaya hizo? Tunahoji iko wapi mikakati ya kukusanya kodi kupitia vyanzo vya halmashauri ili kupunguza utegemezi wa mapato kutoka serikali kuu na pia halmashauri kuweza kuwahudumia wananchi wao?"

"Ni jambo la kusikitisha kuwa vyanzo vikuu vya mapato ni kodi zinazowagusa wananchi wa kawaida kama pombe, sigara, mafuta na simu na ndio tunazotegemea kuendesha maendeleo. Tunashauri serikali kutafuta vyanzo vya kodi visivyo wakandamiza wananchi wa vipato vya chini na kuanza kuondoa misamaha ya kodi isiyo na tija k.m kwenye kampuni za madini na gesi, kampuni za simu (k.m. huduma za milio na miziki ya simu), mahoteli ya watalii na vitalu vya kuwindia wanyama." Alisema Kibena
akifafanua zaidi.

Aidha aliongeza kuwa juhudu za kurekebisha sheria za kodi zinapaswa ziendane na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa kodi kutoka makampuni ya simu, mahoteli ya kitalii, bandari, nyumba za kulala wageni na usafiri wa ndege na treni huku ukiwepo mfumo wa utumiaji bora wa kodi zinazokusanywa na kuwawajibisha vikali wale wanaothibitishwa kuwa wamefanya ubadhirifu.

"Kuna ukinzani kati ya bajeti ya maji ambayo imeainisha bajeti nzima kuwa shilingi bilioni 300 na nyongeza ya shilling bilioni 184.3 ambayo jumla shilling billion 400, wakati hotuba ya bajeti iliosomwa na wizara ya fedha iliosomwa na waziri wa fedha ni shilling billion 747.6. Tunahoji ipi bajeti sahihi ya maji kati ya ile iliyosomwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Waziri wa Fedha?

"Ongezeko la upatikanaji wa maji safi, salama na ya kutosha kutoka 53.74% kufikia 56.57% ya watu waishio vijijini kutoka mwaka 2005 kufikia mwaka 2012 kama ilivyotamkwa katika mpango wa maendeleo wa 2013/14 (kifungu na. 65) ni ongezeko dogo katika kipindi cha miaka saba. Linatutia mashaka kuhusu kufikia upatikanaji wa maji kwa umbali wa meta 400 kufuatana na sera ya maji na umwagiliaji ya mwaka 2002. Hali hii itaendelea kuwafanya wanawake kuendelea kuhangaika kutafuta maji kwa umbali na muda na kuathiri shughuli za kiuchumi."

"Katika vipaumbele vilivyoainishwa bajeti ya sekta ya afya haijawekwa kama kipaumbele, wakati moja ya vipaumbele vya mpango wa maendeleo wa miaka mitano ni pamoja na kuimarisha rasilimali watu. Swali la kujiuliza ni je afya siyo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi hii?. Pia bajeti ya afya ni sh. trilioni 1.5 (11%) ya bajeti ya taifa hailingani na Azimio la Maputo linalotaka kila nchi ilioridhia mkataba huo itenge asilimia 15% ya bajeti kuu kwa ajili ya afya."

Naye Mchambuzi wa Sera kutoka asasi ya TOWSF, Badi Darusi akifafanua zaidi juu ya tamko hilo, alisema kwa mtazamo huo wa kimapungufu kadhaa kwenye bajeti mpya inaendeleza ubaguzi wa kijinsia na kuongeza matabaka kati ya maskini na matajiri, mijini na vijijini, wanawake na wanaume, vijana kwa wazee; hivyo, kusisitiza ipo haja kudai bajeti inayozingatia mahitaji ya wananchi na usawa na kijinsia.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com

No comments:

Post a Comment