TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday 15 August 2013

Dk. Mukangara alonga na wadau wa filamu nchini

Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fissoo akichangia wakati wa kikao kati ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Fenella Mukangara na Steps.(Picha Na Benedict Liwenga)
Na Benedict Liwenga.
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Fenella Mukangara amekutana na wadau wa Kampuni ya Steps Entertainment  na kuzungumza nao juu ya maendeleo ya Tasnia ya Filamu nchini. 

Ujumbe huo wa Steps ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Dileshi Solanki 
Katika mazungumzo hayo Dkt. Fenella amegusia masuala ya uharamia katika  kazi za filamu nchini na kutia mkazo katika suala zima la maadili. Aidha Waziri ameeleza kuwa kuanza kwa urasimishwaji wa tasnia ya filamu na muziki unaoendelea kutekelezwa nchini kutasaidia sana kuondosha kazi zisizohalali. 
Aidha, Dkt. Fenella amewashauri wadau  wa tasnia ya filamu nchini washirikiane kikamilifu na Serikali katika kuendeleza na kukuza tasnia ya filamu na pia kuhakikisha wasanii wananufaika na jasho lao. Aidha ameeleza umuhimu wa kutoa elimu kwa wadau  na umma kwa ujumla juu ya fursa nyingi zilizopo katika tasnia.
Kwa upande mwingine Waziri Dkt. Fenella ameshauri pia kuwe na majumba maalum kwa ajili ya kuonyeshea sinema ambayo yatakuwa yanazipa kipaumbele filamu za kitanzania  pia amehamasisha wadau wa filamu kuanzisha majumba hayo na ambao tayari wameanzisha kutoa fursa hiyo ili kuziendeleza kazi za filamu za kitanzania.
“Kuwe na majumba ya kuonyeshea sinema ambayo yatakuwa yanazipa kipaumbele filamu za kitanzania”. Alisema Dkt. Fenella.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo alibainisha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la filamu zinazowasilishwa kwa ukaguzi na pia wadau wameanza kutumia stempu za TRA katika kazi za filamu na muziki ili kuzilinda kazi hizo. Stampu zilianza kutolewa tangu mwezi Januari mwaka huu .
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mkuu Bw. Dileshi Solanki wa Kampuni ya Steps Entertainment ameiahidi Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni na Michezo Mhe Dkt Mukangara, kuendelea kuendeleza tasnia ya filamu kwa kushirikiana kikamilifu na serikali na kupiga vita uharamia dhidi ya filamu za kitanzania . Aidha wameiomba serikali kuendelea kuwajengea mazingira mazuri.

(Habari ni kwa hisani ya The goverment blog)

No comments:

Post a Comment