TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 23 August 2013

Miss Tanzania atoa msaada wa mabati Shinyanga

Miss Tanzania Brigitte Alfred akiwa na baadhi ya wanafunzi walemavu wa ngozi wa shule ya msingi Buhangija wakinyanyua moja kati ya mabati 200 aliyonunua kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wavulana katika shule hiyo.(Na Mpiga picha wetu)

Miss Tanzania 2012 Brigette Alfred aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa bweni la wavulana shule ya msingi Buhangija akiwa pamoja na afisa elimu wa manispaa ya Shinyanga Honoratha Ruhumbika.(Na Mpiga picha wetu)


Na Mwandishi wetu
MREMBO wa Tanzania, Brigitte Alfred ameanza  ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (albino) katika wilaya ya Shinyanga wanaoishi  katika shule maalum ya Buhangija.

Tayari mrembo huyo ameweka jiwe la msingi na kupandisha ukuta sambamba na kukabidhi mabati 200 kwa ajili ya kujengea paa la bweni hilo la wavulana lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 50.

Makabidhiano hayo yalifanywa na mrembo huyo kwa katika hafla fupi iliyohudhuriwa na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi, Afisa elimu wa Manispaa ya Shinyanga Honoratha Ruhumbika na walimu wa shule hiyo wakiongozwa na mwalimu mkuu, Peter Ajali.


Briggite alisema kuwa ameamua kutimiza ahadi yake aliyoitoa mwezi Aprili mwaka huu alipotembelea Shinyanga kwa kazi za jamii na kuona changamoto za watoto wanaosoma katika shule hiyo.

Alisema kuwa mpango huo upo katika mpango wa Miss Tanzania ujulikano kwa jina la Urembo wenye malengo maalum (Beauty with Purpose) na yeye kuamua kufanya kwa vitendo.

“Ni faraja kwangu kuona kuwa ninatimiza ahadi yangu, nawashukuru wote walionisaidia  ikiwa pamoja na familia yangu, na ninaomba wengine wanisaidie kwani kuna changamoto nyingi katika ujenzi na kazi za jamii kwa ujumla,” alisema Brigitte.

Alisema kuwa amepania kuweka historia katika fani hiyo kwani anaamini ujenzi au jengo hilo litakuwa kumbukumbu kubwa kwake tena kwa vizazi na vizazi.

Brigitte pia aliwataka wanafunzi hao kutokata tamaa hata kwa wale wasiokuwa karibu na familia zao na kwamba wamtegemee zaidi Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye ndiye mfariji kwa wanyonge huku akiwahimiza kuzingatia zaidi elimu kwani ndiyo msingi wa maisha yao.

“Nilipata msukumo wa kuisaidia shule hii hususani katika ujenzi wa bweni  hilo kutokana na ujio wake wa mwezi Aprili mwaka huu shuleni hapo na kujionea adha wanayopata watoto hao kutokana na msongamano mkubwa mabwenini,” alisema.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi alimpongeza Brigitte kwa moyo huo wa kujitolea na kuwataka warembo wengine kuiga mfano wake.

Nyamubi alisema kuwa alichokifanya Brigitte ni jambo la kukumbukwa na ni msaada mkubwa kwa jamii hasa kwa watu wenye ulemabu wa ngozi.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba wazazi wa watoto hao kuwa na tabia ya kuwatembelea watoto wao mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuwachuku wakati wa likizo.

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo Peter Ajali alisema kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo la msongamano mabweni  kwani kuna jumla ya watoto 247 huku mabweni yaliyopo yana uwezo wa kukaa watoto 148 tu.

No comments:

Post a Comment