TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 13 September 2013

Auawa kwa kuchomwa kisu

Na Mwandishi wetu,
Igunga.

Jeshi la Polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora linamshikilia Bw.Msengi Daudi(33)mkazi wa kitongoji cha Mwayunge mjini Igunga kwa tuhuma ya mauaji.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi wilayani hapa lilisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 5:00 usiku katika kilabu cha pombe za kienyeji cha Gelesoni kilichopo mjini Igunga. 

Lilisema kuwa mtuhumiwa huyo alimchoma kisu mgongoni Bi.Happiness Joseph(45)mkazi wa Mwayunge mjini Igunga.

Nae Mwenyekiti wa kitongoji hicho Bw.Ally Isike alikiri kutokea kwa tukio hilo na kulaani kitendo hicho kuwa ni cha kinyama.

Alisema kuwa mwanamke huyo alikuwa akiuza pombe za kienyeji aina ya wanzuki kilabuni hapo ambapo baadaye kulizuka ugomvi baina yake na mtuhumiwa kitendo kilichopelekea mtuhumiwa kumchoma kisu mgongoni. 

Aliongeza kuwa baada ya kuchomwa kisu alipelekwa katika Hospitali ya wilaya ya Igunga kwa matibabu ambapo hali ilizidi kuwa mbaya na hatimaye kupoteza maisha.

“Nimepokea taarifa hii kwa masikitiko makubwa sana,tukio hili ni la kwanza kutokea katika kitongoji hiki,kitendo hiki kwakweli ni cha kikatili na unyama mkubwa hakipaswi kuvumiliwa, naomba sheria ifuate mkondo wake”.Alisema Isike.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Peter Ouma alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi baina ya mtuhumiwa na marehemu unaodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Pia, Kamanda Ouma aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mtuhumiwa huyo na kusema kuwa upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani ili kujibu tuhuma inayomkabili.

No comments:

Post a Comment