TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 13 September 2013

Wahamiaji wasio halali wanaswa

Na Mwandishi wetu,
Igunga.

Watu 11 wanaodaiwa kuwa ni wahamiaji haramu wamenaswa na Jeshi la Polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na jeshi hilo zinasema kuwa wahamiaji hao haramu walinaswa katika juhudi za oparesheni iliyoanzishwa na kikosi cha usalama barabarani ambapo walifanikiwa kuwakamata watu hao.

Aidha jeshi hilo la Polisi lilisema kuwa wahamiaji hao haramu walikamatwa Septemba 13 mwaka huu majira ya saa 3:00 asubuhi katika kijiji cha mgongoro kata ya Igunga wilayani hapa na kikosi cha usalama barabarani ambacho kilikua kinaongozwa na mkuu wa kikosi hicho wilaya ya Igunga Bw.Ame Alawi.


Jeshi hilo la polisi liliongeza kuwa wahamiaji hao haramu walikuwa kwenye gari dogo aina ya Hiace lenye namba za usajili T 287 ASK ambayo ilikuwa imekodiwa na watu hao.

Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na dreva Edward John(27)mkazi wa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambapo wahamiaji hao haramu walikuwa wanatokea Nzega kwenda jijini Dar es salaam.

Baada ya kuhojiwa na polisi walidai kuwa ni familia moja ambapo katika safari hiyo walikuwa wakiongozwa na mwenyeji wao Bi.Anna Gigwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi wilaya ya Igunga Bw.Abeid Maige aliwataja majina wahamiaji hao kuwa ni Gaudensia January(22)mkazi wa Mwenge jijini Dar es salaam, Benard Simon(43)mkazi wa Bagamoyo.

Alisema kuwa wengine ni Uwezo Rwanzila(30)mkazi wa Dar es salaam,Meshack Asher(19)mkazi wa Dar es salaam,Mwamvua Saidi(28)mkazi wa Kibondo,Modester Rwanzima(23)mkazi wa Dar es salaam.

 Wengine ni Shadrack Jonasi(23)mkazi wa Dar es salaam,Samwel January(25)mkazi wa Ussoke Tabora pamoja na Amoni January(27)mkazi wa Dar es salaam.

Alisema kuwa watu hao bado wanaendelea kuhojiwa na polisi na kuongeza kuwa wamefanya mawasiliano na Ofisi ya uhamiaji iliyoko Nzega ili waweze kuja Igunga kwa ajili ya mahojiano zaidi.


No comments:

Post a Comment